Wabunge wawalipua mawaziri
Waziri
wa Fedha, Saada Mkuya akimsikiliza mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya
aliyetaka waziri huyo afukuzwe kazi kwa sababu amevunja katiba. Picha
na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Bunge limeendelea kuwa moto kwa viongozi wakati
wabunge wakiwalipua mawaziri, huku wakimtaka Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya kufukuzwa kutokana na kukiuka Katiba na kumrushia bomu Lazaro
Nyalandu kuwa anazunguka nje ya nchi na msichana kwa madai ya kutangaza
utalii.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pia
alikumbana na kadhia hiyo wakati alipodaiwa kuwa anahusika kwenye kila
mikataba mibomu, jambo lililosababisha mwanasheria huyo mkuu wa zamani
kuingilia kati akitaka “kuheshimiana”.
Wabunge
walifanya hivyo jana bungeni mjini Dodoma wakati wakichangia taarifa za
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC) ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka 2014.
Mkuya
alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali kuonyesha kuwa Serikali ilitumia fedha zilizotengwa
kwa ajili ya matumizi mengine, kitendo kinachomaanisha kuwa alivunja
Katiba.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa viti maalumu
(CCM), Ester Bulaya alisema Bunge limekuwa likitunga sheria na wao kama
viongozi lazima waonyeshe mfano wa kufuata sheria.
“Fedha
ambazo ziko kwenye ring fence (mfuko maalumu), hazitakiwi kutumika kwa
matumizi mengine kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa Katiba, Waziri
umevunja Katiba kwa mujibu wa ibara ya 135 na ibara ya 136 ni Tanzania
peke yake (Waziri Mkuya) unabaki salama. Hupaswi hata kupewa heshima ya
kujiuzulu, unafukuzwa kazi,” alisema Bulaya.
Bulaya,
ambaye amekuwa mmoja wa wabunge wachache kutoka chama tawala wanaoihoji
Serikali, alisema wizara hiyo imeshindwa kukata fedha kwa ajili ya chai,
suti na sambusa na badala yake inakata fedha zilizokuwa ziende kupeleka
umeme vijijini.
Alisema fedha hizo zimetengwa ili kuwezesha Watanzania ambao ni masikini kutumia vibatari.
Bulaya
alikuwa akizungumzia Sh180.7 bilioni zilizokusanywa kulipia gharama za
mradi kutokana na mauzo ya mafuta ili ziweze kupeleka umeme vijijini.
Ripoti
inaonyesha kuwa, kati ya fedha hizo, Sh144.2 bilioni ndizo
zilizopelekwa kwenye mfuko wa umeme vijijini ikiwa ni pungufu ya Sh36.5
bilioni.
Wakati wa kuhitimisha mjadala wa ripoti hizo,
Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Mwigulu Nchemba alikiri kuwa wizara
iliyumba katika eneo hilo kutokana na hali ya kifedha ya Serikali.
“Mwaka
huu ni hapa tu ambako tuliyumba, (katika) eneo hili la matumizi ya
fedha za miradi,” alisema Mwigulu na kuongeza kuwa wizara yake inaandaa
utaratibu utakaowezesha makosa hayo kutojirudia.
Hata
hivyo, alisema mwaka jana wizara ilitoa Sh500 bilioni katika mwezi wa
kwanza tangu kupitishwa kwa bajeti, jambo ambalo alisema lilishangaza
wengi.
“Kuna baadhi ya watu wamesema miradi mingine
ilipata sifuri. Ukweli ni kwamba ile ambayo ilipata sifuri ni kutokana
na fedha hizo kutegemewa kutoka kwa nchi wafadhili,” alisema. “Lakini
miradi mingi ilipata fedha kwa kuwa tulilipa Sh500 bilioni mwezi wa
kwanza baada ya bajeti.”
Alishauri wabunge kumpongeza
Waziri Mkuu kwa maeleo kuwa amefanya mengi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha
utaratibu wa kutaka fedha za miradi zisitolewe hadi wahusika
watakapotoa maelezo ya matumizi ya fedha na kwamba amejiondolea hata
mamlaka ya kusamehe kodi ili kuwezesha fedha zinazopatikana ziende
kwenye miradi ya maendeleo.
Awali, katika mjadala huo,
wabunge wengi waliilaumu Wizara ya Fedha kwa kutumia fedha za miradi kwa
ajili ya shughuli nyingine na kukopa fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya
jamii na kutorudiusha.
Walisema vitendo hivyo
vinaifanya taasisi hizo kushindwa kujiendesha wakati miradi ya maendeleo
ikishindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa fedha.
Pamoja
na Waziri Nchemba kutoa maelezo ya jinsi miradi hiyo ilivyokwama,
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema kuwa siyo kweli kwamba Serikali
imechukua hatua na kwamba ahadi ya Waziri Mkuya kuwa ataunda kikosi kazi
kwa ajili ya kushughulia matatizo hayo, haitoi matumaini kwa kuwa hiyo
itakuwa ya kumi.
“Serikali haina nidhamu ya kulipa,”
alisema Zitto na kutoa mfano wa fedha zilizochukuliwa kutoka Bima ya
Afya kwa ajili ya kununua magari ya polisi ambazo hazijalipwa hadi leo.
“Magari
ya polisi na Bima ya Afya vina uhusiano gani?” alihoji na kuongeza kuwa
tabia hiyo inadhoofisha mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo inatoa fedha
ambazo ni malipo ya pensheni.
“Hii inafanyika kwa
mifuko yote ya NSSF, PSPF na PPF. Deni sasa ni Sh1.8 trilioni na fedha
hizi ni za kuwalipa wastaafu… Kuna mfuko mmoja ambao technically
(kitaalamu) ni bankrupt ( umefilisika).”
Pia, alisema
wakati wa kuidhinisha fedha za mradi wa vitambulisho, Bunge
liliidhinisha Sh52 bilioni. Lakini Bunge lilipomaliza vikao, Serikali
ikaenda kuzikopa.
Utoro wa mawaziri
Mapema jana asubuhi wakati Bulaya akiongea hayo, kulikuwa na mawaziri wasiozidi tisa, kati yao wanne wakiwa manaibu.
Waliokuwapo
bungeni ni Mhagama, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano), Samia Suluhu, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), Binilith Mahenge, Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji,
Christopher Chiza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Mawaziri wengine ni
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose
Migiro, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Dk
Mary Nagu na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia.
Manaibu alikuwa ni
Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk
Makongoro Mahanga, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi.
Hali
akijua hayo, Bulaya alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama kugeuka na kuangalia idadi ya
mawaziri ambao wapo bungeni.
Baadaye aliendelea kusema
kuwa wabunge wamekuwa wakiongea mambo mazuri kama hayo, lakini mawaziri
hawako bungeni na badala wanakuwapo wachache.
Mbunge wa
Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema inasikitisha kwamba hata
wanamitindo sasa wanaanza kufikiria kuwa marais.
Alisema
hali hiyo inasababishwa na wanavyokaa katika Baraza la Mawaziri,
akieleza kuwa mawazo yao mawaziri hayaonyeshi ubunifu wa kubadilisha
nchi.
Lema alisema ndiyo maana Serikali imeshindwa kuwekeza katika miradi ya maji ambayo ingeweza kuleta fedha nchini.
Alisema
Serikali imeshindwa pia kupata Sh20 bilioni kwa ajili ya kufufua
kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre kilichopo mjini Arusha.
“Mara nyingi hii husababishwa na tabia ya mawaziri ambao
mnapokutana kwenye vikao vyenu, mara nyingi mnakwenda kutafuta group
picture (picha za pamoja) badala ya kushauri namna gani ya kupeleka nchi
hii mbele,” alisema mbunge huyo machachari.
“Ndiyo
maana mnashinda kwenye (mitandao wa kijamii ya) instagram, facebook na
Jamii Forums… mnapiga picha za kung’aa kwa sababu katika vikao vyenu vya
kufanya uamuzi, mnajadili mambo ambayo hayana kina cha mawazo. Ndiyo
maana nchi hii inakufa.”
Alisema viongozi wengi wanakosa ubunifu wa kuiendeza nchi hii.
“Angalia
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikwenda kutangaza
utalii nje ya nchi akiwa ameongozana na (mwigizaji maarufu wa filamu wa
Tanzania) Anti Ezekiel,” alisema na kuongeza kuwa waziri huyo hashindi
ofisini kwa kisingizio cha kutangaza utalii.
Alisema
mbuga za wanyama zipo nchini, lakini waziri huyo amekuwa akishinda Ulaya
na kuongeza kuwa sekta ya utalii ingetengenezewa mikakati, ingeweza
kuendesha nchi.
Chagonja atuhumiwa
Lema
alisema hata juzi wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe
anashambuliwa na wabunge kuhusu kilichodaiwa unyanyasaji wa polisi,
alimfuata, akamweleza kuwa tatizo siyo yeye bali ni nchi imekuwa kama
gheto.
“Leo Jeshi la Polisi, leo (Kamishna wa
Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul) Chagonja haamini kama
Rais ameshafanya Uteuzi wa IGP. Jeshi la Polisi limepasuka ma-RPC
(makamanda wa polisi wa mikoa) wanalalamika. Chagonja haamini kama Rais
ameshafanya uteuzi,” alisema.
“Kwa hiyo anafanya
sabotage (hujuma). Hata hizi bunduki zinazoibwa inaweza kuwa ni mkakati
wa Chagonja kumhujumu IGP. Chikawe anajua, watu wote wanajua lakini kila
mtu anasema polepole hii nchi kama gheto (neno linalotumika kumaanisha
nyumba ya mabachela) hujui Serikali ipo wapi.”
Mvutano wa Lissu na Mwanasheria Mkuu
Katika
sakata jingine bungeni jana asubuhi, Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu alisema katika sakata la uchotwaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow watu walioshtakiwa hadi sasa ni wale wenye
nyadhifa ndogo.
Alisema kuwa watu wamechukua mabilioni
ya fedha, lakini waliochukuliwa hatua katika sakata hilo ni wale
waliopatiwa Sh80 milioni.
Alisema Bunge lilipendekeza
majaji waliotajwa katika sakata hilo wachukuliwe hatua, lakini hadi leo
bado hawajachukuliwa hatua. Alisema Rais Jakaya Kikwete anasema hatua za
kuwachukulia majaji hao zianzie mahakamani.
“Huyu Rais
anashauriwa na nani? Katiba yetu inasema wazi kabisa ibara 113 na 120A2
kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya nidhamu kwa majaji, huyu anayesema
mamlaka ya nidhamu hayaanzii kwake ni nani?”alihoji.
Hata
hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alimkatisha kwa
kumpa taarifa kuwa suala hilo lilitolewa mwongozo na Spika kuwa hoja
ikitolewa bungeni haiwezi kurejea tena bungeni hadi baada ya miezi 12.
Hata
hivyo, suala hilo linaweza kurejea tena bungeni kama hoja mahususi.
“Lakini pia Serikali ilete taarifa ya utekelezaji kabla ya Bunge la
bajeti ambalo halijafika,” alisema.
Alisema kanuni haziruhusu kumhusisha Rais na ujengaji wa hoja kwa namna ya kejeli.
Akiendelea
na hoja zake, Lissu aliendelea kusema amepata taarifa ya ‘mrithi’ wa
Jaji Fredrick Werema. Hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu,
kuingilia kati na kumtaka Lissu kutotaja mambo ya urithi.
Hata hivyo, Lissu alisema hoja yake ya msingi Taifa linaharibiwa na ukosefu wa uwajibikaji.
Alisema wanaotakiwa kuadhibiwa na Rais hawaadhibu na kwamba hoja yake siyo kumkejeli Rais.
Alisema
imeonekana katika kamati kuwa majaji wamechukua rushwa, lakini Rais
amekuwa akikimbia na kushindwa kutimiza wajibu wake kikatiba.
Hali hiyo, ilimfanya Masaju kuomba tena taarifa na kusema:
“Ibara
ya 112 inaunda Tume ya Utumishi wa Mahakama 113 inaeleza majukumu ya
Tume ya Utumishi wa Mahakama… Moja wapo majukumu ni kumshauri Rais
kuhusu nidhamu ya majaji, hivyo Rais hawezi kuchukua hatua bila kupata
ushauri huo,” alisema.
Alisema Rais hawezi kuchukua
hatua bila tume ya utumishi kulifanyia kazi na kisha kumpelekea Rais
mapendekezo ambayo ndiyo yatafanyiwa uamuzi.
Mgawo wa Zanzibar waingizwa
Habibu Mnyaa (Mkanyageni-CUF), alilamikia tatizo la fedha za mafuta wanazokatwa pande zote kushindwa kwenda upande wa Zanzibar.
“Nahitaji
majibu ya waziri ni kwanini mpaka sasa hata shilingi moja haijapelekwa
huko…Tukilalamika mnasema Wazanzibari ni wakorofi. Hii ndiyo hali
inayotufanya tuone uonevu wa misingi ya serikali tatu na kutoona umuhimu
wa muungano,”alisema.
Kamati ya Uongozi
Kamati ya Uongozi ya Bunge imeamua kuwa kuanzia sasa halitajadili jambo lolote lililo mahakamani kama ilivyokuwa awali.
Msimamo
huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu baada ya
kikao cha Kamati ya Uongozi kilichokaa kujadili jambo hilo.
Zungu
alitoa tamko hilo baada ya jana asubuhi mbunge wa viti maalumu, Suzan
Lyimo kuomba mwongozo wa kwa nini suala la Uda linakatazwa kujadiliwa
wakati lipo kwenye ripoti za kamati.
Juzi, Spika Anne
Makinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju
kuzuia kujadiliwa suala la Uda kutokana na kuwapo kwa kesi mbili
mahakamani.
Jana baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi,
Zungu alisema: “Tumekubaliana kwamba suala lolote ambalo lipo mahakamani
halitajadiliwa hapa bungeni kipindi hiki,” alisema Zungu na kuongeza:
“Tusiingilie kabisa jambo hilo na huo ndiyo mwongozo kuhusu ombi la
Suzan Lyimo.”