Mwaka wa uchaguzi,Kikwete atoa salamu za mwisho za mwaka
>Mwaka wa uchaguzi umeingia. Usiku wa kuamkia leo, Watanzania wameupokea mwaka mpya 2015 huku
Dar es Salaam. Mwaka wa uchaguzi umeingia.
Usiku wa kuamkia leo, Watanzania wameupokea mwaka mpya 2015 huku
tafakari kubwa ikiwa ni matukio makubwa yatakayotokea mwaka huu, ukiwamo
Uchaguzi Mkuu na kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Mbali
na uchaguzi wa rais wa awamu ya tano, wananchi wataamua ama kuipitisha
au kuikataa Katiba Inayopendekezwa, mambo ambayo wasomi, wanasiasa na
wanaharakati wameonya kuwa yanatakiwa kuendeshwa na kusimamiwa kwa
weledi na umakini mkubwa.
Vilevile, kutokana na matukio
hayo kugharimu fedha nyingi, wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa mwaka
huu utakuwa mgumu na itakaowalazimu Watanzania kufunga mikanda zaidi.
Pia,
macho na masikio ya wananchi yako kwa vyama vya upinzani ambavyo
vimeungana na kuzaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuona kama
vitasimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi za ubunge na
udiwani kama vilivyokubaliana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa
mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Maandalizi ya uchaguzi
huo yanaanza mwezi huu kwa wapigakura kuandikishwa upya katika Daftari
la Kudumu la Wapigakura, ambalo tangu mwaka 2009 halijawahi kuboreshwa
na hivyo kusababisha wengi kushindwa kupiga kura katika uchaguzi wowote
uliofanyika baada ya 2010.
Pengine jambo ambalo
linasubiriwa kwa hamu na wananchi ukiacha Uchaguzi Mkuu na Katiba Mpya
ambayo kampeni zake zitaanza Aprili 30, ni mchakato wa ndani ya vyama
vya siasa wa kupata wagombea urais, hasa kutokana na mvutano ulioanza
kujitokeza ndani ya CCM na mvutano unaotarajiwa ndani ya Ukawa.
Matukio
Tukio
litakaloanza mwaka huu ni lile la Januari 30 la uandikishaji katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao utakamilika Aprili 28 ukifanywa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kulingana na
uandikishaji wa majaribio uliofanyika katika majimbo matatu ya Kawe,
Kilombero na Katavi, shughuli yenyewe inatarajiwa kuvuta hisia na hamasa
za Watanzania wengi hasa kutokana na muda, matatizo ya kukwama kwa
mashine za kielektroniki (BVR) na wingi wa watu waliojitokeza.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ametangaza tarehe ya upigaji Kura ya Maoni kuwa ni Aprili 30.
Februari
mwaka huu, CCM imeahidi kutoa msimamo wake kuhusu wanachama wake
walioanza kufanya kampeni mapema kujihusisha na vitendo vilivyokiuka
maadili ndani ya chama na jamii. Huenda chama hicho kikawaengua baadhi
yao kwa kuongeza muda wa onyo hivyo kujikuta wakishindwa kuwania nafasi
hiyo, iwapo watabainika kuendelea kukiuka maadili ya chama, licha ya
awali kuonywa na kupewa adhabu ya kutojihusisha na masuala hayo mpaka
baada ya miezi 12.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye; mawaziri Bernard Membe (Mambo ya Nje), Stephen Wasira (Ofisi ya
Rais, Uhusiano na Uratibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Mei utakuwa na tukio la aina
yake pale Ukawa na CCM pamoja na vyama vingine vitakapokuwa vikiteua
wagombea urais, ikiwa ni baada ya wengi waliojitokeza kuchujwa katika
vikao vya ndani vya vyama hivyo.
Juni mwaka huu, Rais
Kikwete atalivunja Bunge baada ya kumalizika kwa Mkutano la Bajeti
utakaoanza Aprili mwaka huu, ukiwa tayari umepitisha bajeti ya Serikali
ambayo sehemu yake itatumiwa na Serikali mpya ya awamu ya tano. Pamoja
na kwamba siyo utaratibu wa kikanuni, lakini kwa utamaduni wa Bunge la
Tanzania, Rais Kikwete anaweza kutoa hotuba ya kulivunja Bunge.
Miezi
inayotarajiwa kuwa na changamoto kubwa ni kuanzia Julai hadi Oktoba
ambayo itakuwa ya kampeni za uchaguzi ambao wagombea urais, ubunge na
udiwani watakuwa wakinadi sera zao.
Mwishoni mwa
Oktoba, ndipo utakapofanyika Uchaguzi Mkuu na Tanzania kupata rais mpya
ambaye mpaka sasa ni vigumu kutabiri atakuwa nani na atatoka chama gani.
Hali hiyo inatokana na CCM hadi sasa kuwa na makada zaidi ya 14
wanaotajwa kuutaka urais wakiwamo wanne ambao tayari wametangaza nia ya
kugombea nafasi hiyo. Kwa upinzani, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD vinavyounda Ukawa ndiyo wanaopewa nafasi za kugombea
nafasi hiyo. Hao ni Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willbrod Slaa, James
Mbatia na Freeman Mbowe huku vyama vyenyewe vikisema vinaweza hata
kumpata mtu nje ya muungano huo.
Uchambuzi wa kisomi
Mhadhiri
katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam (Tudarco), Lois- Singa
Metili alisema mwaka 2015 ni kipindi cha mpito ambacho endapo mambo yote
yaliyopangwa yatakwenda sawa, miaka inayofuata itakuwa mizuri kwa
Watanzania.
“Hatujui kura za hapana au za ndiyo kwenye
Kura za Maoni ya Katiba zitakuwa ngapi, hatujui kama NEC itapewa meno ya
kutosha ya kusimamia uchaguzi ili tupate rais kwa njia ya haki.
Alisisitiza kuwa iwapo haki itatumika katika kupitisha
mambo hayo, nchi itajenga msingi imara kwa maendeleo ya watu wake kwa
miaka mingi ijayo.
Alisema kwa kuwa Tanzania mwaka 2014
ilitajwa vibaya kwenye vyombo vya habari vya Magharibi, ikihusishwa na
kashfa za rushwa, inabidi taasisi zote nchini kurekebisha kasoro hiyo.
Kuhusu
siasa, Metili alisema CCM itakuwa na kibarua cha kumpata mgombea mwenye
sifa atakayekubalika kwa wananchi. Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kutokana na mwaka 2015 kukabiliwa na
mambo mazito ya kitaifa yanayohitaji fedha nyingi, Serikali itakuwa
katika wakati mgumu kifedha.
Dk Ngowi aliutaja mwaka
huu kuwa ni wa kipekee kwa kuwa licha ya kuhitaji fedha nyingi,
utaongezewa maumivu na hatua ya wahisani kukataa kutoa msaada kwa sababu
ya kashfa ya escrow iliyotokea mwishoni mwa 2014.
Alieleza
kuwa ingawa maisha ya wananchi yanaweza yasibadilike sana, lakini
Serikali itahitaji kujipanga upya katika kukusanya fedha.
Uchambuzi
wa Dk Ngowi unaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),
David Kafulila aliyesema mwaka huu uchumi wa nchi utaporomoka kwa sababu
ipo katika mahitaji makubwa ya fedha za uchaguzi, uandikishaji
Vitambulisho vya Taifa na vya kupigia kura sambamba na upigaji wa kura
ya maoni kupitisha Katiba Mpya.
“Uchumi unakua lakini
maendeleo ya uchumi hayaonekani kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha
za umma pamoja na uchumi kukuzwa na sekta za madini, utalii, mawasiliano
ambazo hazibebi watu wengi kama ilivyo katika kilimo, mifugo na uvuvi,”
alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema licha ya mwaka
huu kuwa na mambo mengi muhimu, Serikali haionekani kuchukua hatua za
dharura.
Dk Kijo- Bisimba alisema ili taratibu ziende
kama zilivyopangwa, ilitakiwa hadi sasa nakala za Katiba Inayopendekezwa
ziwe zimeshasambazwa kwa wananchi, lakini hilo linaonekana kusuasua.
“Maboresho
ya Daftari la Wapigakura yalitakiwa yawe tayari, lakini mamlaka
hazijajipanga kama ulivyoona kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa,”
alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Watanzania wanaingia
mwaka mpya wakiwa wamechanganyikiwa, hawajui nani anasema ukweli kuhusu
fedha za escrow kama zilikuwa ni za umma au la... “Bunge lilisema fedha
zile ni za umma, lakini huyu mwingine naye kasema siyo fedha za
umma.”Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (Duce), Dk Aneth
Komba alisema; “Ninachokiona mwaka huu utakuwa mfupi sana kutokana na
mambo kuwa mengi.”
JK atoa salamu za mwisho za mwaka akiwa Rais
Rais
Jakaya Kikwete jana alitoa salamu zake za Mwaka Mpya kwa mara ya mwisho
katika utawala wake huku akisema mwakani atakuwa akifuatilia salamu
kama hizo kupitia televisheni na redio akiwa kijijini kwake Msoga mkoani
Pwani.
Katika hotuba hiyo yenye maneno 5,988 iliyojaa
mapitio ya mambo mbalimbali ya mwaka 2014, Rais Kikwete alisema wakati
Rais wa awamu ya tano akitoa zake za kwanza za mwaka mpya, yeye atakuwa
raia wa kawaida na itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa.
Sanjari
na hayo, Rais aliwaagiza viongozi wa Serikali wanaowawekea vikwazo
wafanyabiashara wanaouza mazao nchi za nje kuacha vitendo hivyo ili
kuwawezesha wafanyabiashara hao kutimiza azma yao.
Alisema
uzalishaji mazao mwaka huu umeongezeka hadi tani milioni 16.2
ukilinganisha na tani milioni 14.38 za mwaka 2013 na kwamba Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) si mnunuzi wa mazao yote hayo, hivyo
mengine yatanunuliwa na wafanyabishara wanaotakiwa kushawishiwa
kuyanunua kwa wingi.
“Jambo muhimu ninalopenda
kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo
ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya
hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo,” alisema Rais
Kikwete.
Aliwataka Watanzania kujiandikisha katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura kwani kushindwa kufanya hivyo
kutawanyima fursa ya kupiga kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa
pamoja na Uchaguzi Mkuu.
Nyongeza na Nuzulack Dawsen