‘Zungu la unga’ auawa mahakamani akijaribu kuwatoroka askari
>Ilikuwa kama sinema. Raia wa Sierra Leon, Abdul Koroma (33) aliyekuwa akikabiliwa kesi ya
Dar es Salaam. Ilikuwa kama sinema. Raia wa
Sierra Leon, Abdul Koroma (33) aliyekuwa akikabiliwa kesi ya kuingiza
dawa za kulevya nchini zenye thamani ya Sh61.4 milioni alipouawa kwa
risasi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akijaribu kutoroka
chini ya ulinzi wa askari wa Magereza.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.45 asubuhi baada Koroma kutoka katika Gereza la Keko na kufikishwa mahakamani.
Mashuhuda
wa tukio la kuuawa kwa mshtakiwa huyo ambaye alikamatwa na dawa hizo
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Brazil,
walisema kabla ya kifo chake alimwomba askari ampeleke chooni.
Bila
kutaja majina, walisema akiwa chooni, Koroma alivua suruali yake ya
jeans na kuitumia kutoroka kwa kujikinga na chupa zilizozunguka ukuta wa
eneo la choo hicho na kuruka upande wa pili na kutimua mbio.
Walisema
alikimbia akiwa amevaa kaptula akipita katika kichochoro kilichopo
kati ya Mahakama hiyo na mgawahawa uliopo ndani ya uzio.
Mmoja wa askari Magereza alimuona na kuwaeleza wenzake ndipo walipoanza kumkimbiza.
Walisema Koroma alitahadharishwa kusimama kwa hiari yake kwa kupiga risasi moja hewani, lakini Koroma hakutii amri.
Wakati yote hayo yakiendelea, askari Magereza aliyekuwa na silaha alilazimika kumpiga risasi ya shingo na kufa papo hapo.
Mmoja wa askari alisema iwapo askari huyo asingekuwa mwangalifu kwa kuipiga risasi hiyo, angesababisha madhara kwa watu wengine.
Saa
moja baada ya tukio hilo lilotokea saa mbili asubuhi, polisi walifika
eneo hilo wakiwa na magari matatu aina ya Landrover Defender na moja
aina ya Noah zote zikiwa zimebeba askari waliokuwa wamevalia kiraia
pamoja na machela na kuunasua mwili wa marehemu juu ya uzio na kuondoka
nao.
Pamoja na tukio hilo, kesi yake namba 21 ya mwaka
2013 iliyofikishwa mahakamani hapo Desemba 2, 2013 ambayo hadi jana
upelelezi wake ulikuwa haujakamilika, iliendelea.
Kesi
hiyo jana ilitajwa mbele ya Hakimu Hellen Liwa na Wakili wa Serikali,
Leonard Challo alitoa taarifa mahakamani hapo kuhusu tukio hilo.
Alisema wanasubiri hati ya kifo cha ili wafunge faili la mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.