Serikali yaikaba koo IPTL mahakamani

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju (kulia) akimsikiliza mwanasheria wa Kampuni ya IPTL, Melickzedek  Lutema baada ya kuahirishwa kwa kesi  iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Serikali imewasilisha ombi la kutaka mahakama itupilie mbali maombi ya walalamikaji katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow ya kuzuia utekelezaji wa maazimio ya Bunge.
Kesi ya kuzuia utekelezaji huo ilifunguliwa na kampuni za Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Pan African Power Solution pamoja na mwenyekiti mtendaji wa kampuni hizo, Singh Seth dhidi ya Waziri Mkuu na Spika wa Bunge.
Sambamba na kesi hiyo namba 59 ya mwaka 2014, pia walalamikaji hao walifungua maombi ya zuio la muda la utekelezaji ili kusubiri uamuzi wa kesi hiyo ya kikatiba na wakiainisha hoja tano, zitakazofafanuliwa wakati za usikilizwaji.
Katika hoja zake za pingamizi, Serikali inadai kuwa maombi hayo hayana mashiko kwa kuwa yanakiuka Ibara ya 63 na ya 100 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 5 cha Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge.
Katika hoja nyingine, Serikali inadai kuwa maombi hayo yameambatanishwa na hati ya kiapo chenye kasoro za kisheria.
Hoja nyingine ni kwamba maombi hayo ni batili kwa kuwa hayakuainisha kifungu cha sheria kinachosimamia.
Pingamizi hilo lilitarajiwa kusikilizwa jana na jopo la majaji watatu, Agustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Gadi Mjemas na Stellah Mugasha, lakini usikilizwaji huo ulikwama baada ya mawakili wawili wa IPTL kushindwa kufika mahakamani.
Mmoja wa mawakili wanaotetea walalamikaji, Melickzedek Lutema aliieleza Mahakama kuwa kiongozi wa jopo la mawakili wa IPTL, Joseph Makandege ni mgonjwa.
Lutema pia alisema  wakili mwingine, Gabriel Mnyele alisafiri kwenda Mpanda na alitarajiwa kuwasili juzi, lakini alikosa usafiri.
Aliiomba kesi hiyo iahirishwe ili awasiliane wenzake.
Mahakama ilikubaliana na ombi hilo na kuamua kuwa pingamizi hilo litasikilizwa na jaji mmoja.
Baada ya mawakili wa pande zote kukubaliana, Jaji Mwarija alisema suala hilo litapelekwa kwa Jaji Kiongozi ili ateue jaji atakayesikiliza pingamizi hilo na tarehe ya usikilizwaji watajulishwa. Kesi hiyo itatajwa  Januari 13, 2015.
Powered by Blogger.