Vita ya urais yashika kasi mtandaoni, wanaotajwa wafuangua akaunti za kuwanadi
Wakati safari ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ikipamba moto, kumeibuka makundi ya watu
Ikulu ya Tanzania
Ikulu ya Tanzania
Dar es Salaam. Wakati safari ya kuelekea kwenye Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba mwaka huu ikipamba moto, kumeibuka makundi ya watu
yaliyofungia akaunti katika mitandao ya kijamii yakiwaunga mkono baadhi
ya wanasiasa waliotangaza au wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea urais ya
kuwashambulia washindani wao.
Kila kundi limejipatia
wafuasi wengi ambao wanaonyesha kumkubali mwanasiasa husika wanayedhani
anafaa kuwa rais wa Tanzania endapo atapitishwa na chama chake na
kupigiwa kura na wananchi.
Hata hivyo, wasomi na
wachambuzi wanaonya kuwa pamoja na njia hii kuwa ya haraka kuwafikia
wapigakura walio wengi ambao ni vijana na wanawake, inatakiwa kutumika
kwa uangalifu la sivyo inaweza kusababisha machafuko.
Makundi yenyewe
Makundi
hayo, mengi yakipatikana katika mitandao ya Facebook, Twitter na
WhatsApp yanafanya kazi ya kuwanadi wanasiasa na kubainisha shughuli
mbalimbali wanazozifanya kila siku wawapo katika ziara zao za binafsi,
za kiserikali au kichama katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi
ya kurasa za makundi hayo zenye wafuasi wengi ni pamoja na ule wa ‘Team
Lowassa’, kundi linalomuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
ambao hadi jana ulikuwa na wafuasi 46,124 ambao wanaweza kupata habari
mbalimbali zinazomhusu kiongozi huyo.
Hata hivyo,
mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu, hivi karibuni
alikaririwa na gazeti hili akiikana moja ya akaunti za Twitter iliyokuwa
imechapisha taarifa zilizomkariri akizungumzia suala la ufisadi wa
escrow.
Akizungumzia kurasa hizo, Msaidizi wa Lowassa,
Abubakar Liongo alisema akaunti hizo zinatengenezwa na marafiki na
kusisitiza kwamba kiongozi huyo hahusiki nazo kwa namna yoyote.
“Hawa
ni marafiki tu, huwezi kuwazuia kufanya wanachotaka kufanya, sisi
tumeshatoa taarifa kuwa hizi hatuhusiki nazo,” alisema Liongo.
Kundi
jingine linajitambulisha kama ‘Team Hamis Kigwangalla’ linalomuunga
mkono Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla na mpaka kufikia jana
lilikuwa na wafuasi 9,893. Hili ni kundi la pili kuwa na wafuasi wengi
katika mtandao wa Facebook baada ya lile la Team Lowassa.
Ukurasa
mwingine umeanzishwa na watu wanaomuunga mkono Mbunge wa Bumbuli na
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Ukurasa huu umepewa jina ‘January Makamba – The next President’ na hadi
jana ulikuwa na wafuasi 7,075.
Wanasiasa wengine
wanaohusishwa na mitandao hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye mbali na akaunti yake kwenye
WhatsApp, ukurasa wa marafiki zake kwenye Facebook wenye jina la
‘Bernard Membe Fans Page’ umefikisha wafuasi 5,120.
Kundi
la wafuasi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa linafuatia.
Kundi hilo lililoanzisha mtandao uliopewa jina ‘Dr Slaa Team Winner –
2013/2015’ hadi jana lilikuwa na wafuasi 4,337.
Vilevile,
lipo kundi jingine linalomuunga mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na ambalo ukurasa wake uitwao
‘Wasira wa Watanzania (WWW)’ lina wafuasi 3,524.
Pia
upo ukurasa wa “Marafiki wa Samwel Sitta’ katika Facebook wenye
mashabiki 2,238 wanaomuunga mkono Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Katika
mtandao wa Twitter, wanasiasa hao na wengine hawako nyuma, karibu kila
mmoja ana akaunti binafsi huku wafuasi wao wakipata nafasi ya kusoma
yale wanayoyaandika wakati wowote.
Miongoni mwa wanasiasa wenye wafuasi wengi ni Zitto
Kabwe ambaye watu 208,294 wanafuatilia hoja zake na wakati mwingine
kujibizana.
Anayefuata ni Makamba mwenye wafuasi
151,822, Bernard Membe (45,889) na Dk Slaa (40,830). Lazaro Nyalandu
aliyetangaza wiki iliyopita kuingia katika mbio za kusaka urais, akaunti
yake ya Twitter inafuatiliwa na watu 36,726.
Wengine
katika mkondo huo ni Dk Khamis Kigwangalla (26,322), William Ngeleja
(11,110), Anna Tibaijuka (8,053), Freeman Mbowe (4,162), Asha-rose
Migiro (4,736), Edward Lowassa (2,123), Stephen Wasira (750) na Dk
Emmanuel Nchimbi (515).
Ni dhahiri kuwa wanasiasa
vijana ndiyo wanaotumia zaidi mitandao ya kijamii na kuwa na wafuasi
wengi ambao wengi wao pia ni vijana.
Maoni ya wachambuzi
Baadhi
ya wasomi nchini wameelezea kuwa si jambo baya kutumia mitandao ya
kijamii kujinadi kwa wananchi. Hata hivyo, wameonyesha wasiwasi kwa
jinsi inavyotumika na kuwa inaweza kusababisha machafuko.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kadri muda
unavyokwenda, ndivyo jamii inavyobadilika na mabadiliko haya yanahusisha
pia matumizi ya mitandao ya kijamii.
Salim alisema
vijana na wanawake ambao ndiyo idadi kubwa ya wapiga kura, sasa
wanatumia mitandao ya kijamii. Alisisitiza kuwa hii ndiyo sababu pekee
iliyowasukuma wanasiasa kuanza kutumia mitandao ya kijamii.
“Mitandao
hii inawasaidia wanasiasa kujitangaza kwa wananchi, pia haina gharama
kwao. Tulizoea kuona wanasiasa wakipita mitaani kutoa zawadi na kujinadi
kwa wananchi kipindi cha uchaguzi, sasa ni rahisi,” alisema.
Hata
hivyo, Salim alionya kuwa mitandao ya kijamii isipodhibitiwa
kikamilifu, inaweza kusababisha machafuko ya kisiasa kama ilivyotokea
katika nchi za Tunisia na Libya na kusababisha mapigano ya wenyewe kwa
wenyewe ambayo yanaendelea mpaka sasa.
“Tuliona pia
wakati wa sakata la escrow, watu walianza kuunda baraza la mawaziri
mtandaoni kabla hata Rais hajasema chochote. Sasa hii ni hatari, wakati
mwingine inaweza kujenga chuki,” alisema.
Alisema
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni, Ukawa
hawakutumia nguvu kubwa kwa sababu walishajenga ngome kwenye mitandao ya
kijamii.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Richard Mbunda alisema sasa hivi mitandao ya kijamii ni sehemu
ya maisha ya Watanzania. Hivyo, inakuwa rahisi kwa wanasiasa kuwafikia
wengi ndani ya muda mfupi kwa njia hiyo.
Alisema uzuri
wa mitandao ya kijamii ni kuwa wanasiasa wanapata nafasi ya kujitangaza
na wananchi pia wanapata kuwafahamu na kuwapima kama wanaweza kuongoza
Taifa hili.
Aliuangana na Salim akisema kuwa Tanzania
haina udhibiti mzuri wa mitandao ya kijamii, jambo linaloweza
kusababisha chuki na mifarakano miongoni mwa wanajamii.
“Si
kila linaloanzishwa ni jema asilimia 100, wengine wanatumia mitandao ya
kijamii kuwachafua wengine, hasa mahasimu wao kisiasa,” alisema Mbunda
na kuitaka Serikali kuwa na udhibiti wa mitandao hiyo hasa wakati huu
kuelekea Uchaguzi Mkuu.