Makundi ya urais CCM yaitafuna jumuiya ya wanafunzi wa vyuo

Mwenyekiti wa Taasisi za Elimu ya juu nchini(TAHLISO), Musa Mdede akizungumza na wanafunzi kuelezea furaha yake ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo mwaka jana.

Dar es Salaam. Mbio za urais 2015 zinaendelea kushika kasi. Wanasiasa wanapigana vikumbo kutafuta kuungwa mkono na vyama vyao kwa nia ya kuendelea kushika dola kwa wale waliopo madarakani na waliopo nje wakijaribu kujiimarisha kwa kujiongezea wafuasi ili waweze kupata ridhaa ya kuongoza.
Vita vya wazi ni baina ya chama tawala cha CCM na kambi ya upinzani kupitia ushirikiano wao walioupa jina la Ukawa.
Kwa ujumla wanasiasa kutoka makundi haya wameelekeza nguvu zao katika kusaka uungwaji mkono kwa vijana kwa kile wanachoeleza kuwa ndilo kundi pekee lenye uwezo wa kushawishi idadi kubwa ya watu wa kada zote kwa lengo la kujizolea ushindi katika chaguzi zijazo.
Eneo pekee lenye vijana wa kada na hulka tofauti ni ndani ya jumuiya za wanafunzi nchini. Na kutokana na ukweli huo, tayari CCM imepiga hodi ndani ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu nchini (Tahliso), kutafuta kuungwa mkono.
Hatua ya CCM kujipenyeza katika jumuiya hiyo ya wanafunzi, imesababisha mpasuko mkubwa uliopo kwa viongozi na wajumbe wa Tahliso na wanafunzi kwa ujumla wake.
Katika kudhihirisha hilo, uongozi wa Tahliso chini ya uenyekiti wa Musa Mdede imemuondoa madarakani makamu mwenyekiti, katibu mkuu, naibu katibu na mwenyekiti wa Baraza Kuu la Tahliso (seneti) kwa madai ya kukiuka maadili ya uongozi.
Mwananchi ilifanya mahojiano maalumu na Mdede kutaka kujua nini sababu za hali iliyosababisha kufanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa jumuiya hiyo ya wanafunzi.
Swali: Kuna ukweli gani kuhusu madai kuwa baadhi ya viongozi Tahliso wamevuliwa madaraka?
Jibu: Ni kweli. Wapo baadhi ya viongozi wa jumuiya hii ambao tumewavua uongozi. Sababu ya kufanya hivyo ni kuwa walikosa uvumilivu na hawakutambua majukumu yao ndani ya Tahliso.
Tumebaini siyo mara moja kuwa miongoni mwa viongozi wanafunzi waliotekwa na makundi yanayompigia kampeni za urais mmoja kati ya vigogo wa CCM yumo ndani ya Tahliso. Tulishasema kampeni hizo wafanye nje na siyo kuzileta kwa wanachama wa Tahliso.
Julai 31, mwaka huu tuliwakuta wakishiriki mkutano na kigogo huyo katika Hoteli ya Valley View hapa jijini Dar es Salaam. Kundi jingine likawachukua wenyeviti 10 wa vyuo mbalimbali na kushawishiwa watangaze mbele ya vyombo vya habari kwamba jumuiya ya Tahliso haina uongozi.
Baadhi yao, wakapewa tisheti zenye ujumbe wa kumpigia kampeni kigogo huyo, hali ambayo ilikuwa kinyume na Sheria ya Vyuo Vikuu ya 2005 pamoja na Katiba ya Tahliso.
Swali: Nguvu hiyo ya makundi ya urais imefanikiwa kwa kiwango gani kupenyeza makucha yake ndani ya Tahliso?
Jibu: Makundi hayo yameingia na mpaka sasa kati ya vyuo 44, nusu ya marais wa vyuo vikuu ndani ya Tahliso wameshatekwa na makundi ya urais CCM, hali inayochangia kuzorotesha upiganiaji wa haki za wanafunzi.
CCM imekuwa na kamati yake ya uratibu wa uchaguzi wa vyuo vikuu nchini ambayo inaipa baraka zote kutoka Kamati Kuu ya CCM. Kwa taarifa za uhakika, CCM imekuwa na mkakati wa kupitisha wagombea wa urais ili kujenga ushawishi wake kwa vijana.
Hatua hiyo inaathiri kwa kiwango kikubwa sana jumuiya ya Tahliso katika utendaji wake kwani umoja unakosekana, kauli ya pamoja inapotea hata tunapohitaji kupigania mikopo au madai yoyote.
Swali: Kwani kuna dhambi gani kwa viongozi kuwa wafuasi au wenye mapenzi na vyama vya siasa, Inadaiwa hata wewe ni mfuasi wa Chadema?
Jibu: Ni sawa na ifahamike kuwa siyo dhambi kuwa mwanachama wa kisiasa na tofauti zetu tunaheshimiana, lakini dhambi kubwa ni kuendesha siasa za makundi ya urais ndani ya himaya ya chuo au ushawishi kwa wanachama wa Tahliso.
Mimi nimechaguliwa kisheria na nimeapa kuendesha Tahliso kwa mujibu wa katiba. Nina muda wa mwaka mmoja, lakini sijawahi kushawishi wanachama waingie Chadema.
Kinachonisikitisha zaidi, nimekuwa nikishinikizwa na kushawishiwa kuunga mkono makundi hayo na kutoa matamko ya kubadili msimamo au kuunga mkono kundi fulani, lakini wakati wote nimekuwa nikiwakatalia.
Viongozi wote tunazo itikadi zetu lakini tumekula kiapo cha kutoingiza kampeni za vyama vyetu ndani ya Tahliso.
Swali: Kutokana na uamuzi huo, changamoto gani ulizokutana nazo ukiwa kiongozi wa Tahliso mpaka sasa?
Jibu: Zipo changamoto na vikwazo vingi. Ukiachana na makundi ya urais, nimewahi kulazimishwa nitoe kauli ya kukemea uamuzi wa kundi la Ukawa baada ya kutoka nje ya Bunge wakati wa mjadala wa Katiba, lakini nilikataa.
Haikuishia hapo wiki chache baadaye nikafuatwa na kundi la wanasiasa fulani wakaniambia niunge mkono Serikali mbili zilizopendekezwa kwenye Katiba pia nilikataa. Nikaalikwa siku ya uzinduzi wa Katiba hiyo inayopendekezwa, lakini nikakataa.
Sababu za kukataa ilikuwa ni kuepuka mtego wa kuingia kwenye mkumbo wa kuitumbukiza Tahliso kwenye mikono ya wanasiasa. Ningeweza kutenda dhambi kubwa sana ambayo ingenilazimu kutubu wakati athari ikiwa imeshatokea. Ifahamike kamba, Tahliso ni jumuiya iliyoanzishwa kwa ajili ya kutetea masilahi ya wanafunzi wa vyuo na siyo kuendesha harakati za vyama vyetu ndani ya Vyuo.
Swali: Kama uliweza kukwepa mishale hiyo, ungeshindwa vipi kupenyeza ushawishi wako wa Chadema?
Jibu: Kama ningethubutu kufanya hivyo basi nisingekuwa madarakani mpaka sasa. Tahliso ni jumuiya kubwa na ni hatari kujiingiza sana katika itikadi za kisiasa. Lakini hatima yangu inatokana na kujikita zaidi kutetea madai ya wanafunzi na siyo kukimbizana na siasa.
Swali: Kwa mazingira hayo, unadhani hakuna hofu yoyote ya kupinduliwa kwenye nafasi yako?
Jibu: Sihofii kundi lolote kwani mimi ni mwenyekiti niliyechaguliwa kwa demokrasia na kuapishwa kihalali Julai 17, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Blue Peal jijini Dar es Salaam.
Pamoja na hilo, kwa sasa nimebakiza mwaka wa mwisho katika masomo yangu ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Bugando, jijini Mwanza, hivyo inawezekana nikagombea uchaguzi ujao wa Agosti 2015 au nisigombee kabisa.
Swali: Kitu gani ambacho unatakiwa ukifanye kwa sasa ili kuondoa mzimu huo wa makundi ya urais?
Jibu: Tahliso itaendelea kuwapo na hatua zinaoendelea kwa sasa ni kupigania harakati za wanafunzi waliokosa mikopo kupitia kampeni mpya ya ‘Bring Our Loan’ tukimaanisha tupewe mikopo, tuliyoizindua hivi karibuni.
Kuhusu makundi ya urais ndani ya Tahliso kwa sasa hayana nafasi tena hivyo ni vyema wanachama wote wa jumuiya hiyo wakajikita zaidi katika harakati za kupigania masilahi ya wanafunzi.
Powered by Blogger.