Askofu Nzigilwa: Rugemalira alitoa fedha za matoleo
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa
Dar es Salaam. Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Eusebius Nzigilwa amevunja ukimya akisema ni kweli alipokea
Sh40.4 milioni kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP, James Rugemalira
zikiwa matoleo ya kusaidia uendeshaji wa kanisa.
Askofu
Nzigilwa ni mmoja wa watu waliopata fedha kutoka kwa Rugemalira
anayehusishwa kugawa kwa watu mbalimbali mabilioni ya shilingi
yanayohusishwa na fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow
wakiwamo wabunge, mawaziri na viongozi wa dini.
Tayari
baadhi ya viongozi wa Serikali wamewajibika kwa ama kutumia vibaya
madaraka yao au kupokea fedha hizo kinyume cha sheria ya maadili ya
viongozi wa umma.
Kupitia taarifa yake ya kurasa tatu
kwa vyombo vya habari, Askofu Nzigilwa alielezea uhusiano wake na
familia ya Rugemalira ulivyoanza na jinsi ambavyo amekuwa akitoa sadaka
na michango mbalimbali ya hali na mali.
“Kanisa
linategemezwa na nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliongoza kupitia michango
ya watu. Hivyo, kwa waumini kutoa michango na matoleo kwa kanisa na
watumishi wake ni jambo la kawaida katika desturi za imani yetu tangu
nyakati za mitume,” alisema askofu huyo.
Alisema
uhusiano wake na familia ya Rugemalira ulianza mwaka 2008 alipopangiwa
katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu, Makongo Juu
akiwa Paroko Msaidizi, Rugemalira akiwa muumini katika parokia hiyo.
Alisema
akiwa katika parokia hiyo, walikuwa na ujenzi wa nyumba ya mapadri na
mikakati ya ujenzi wa kanisa jipya la parokia hiyo na katika shughuli
zote hizo, Rugemalira na waumini wengine walikuwa ni wachangiaji wazuri.
“Hata
baada ya kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi tumekuwa tunashirikiana na
kuwasiliana na familia ya Rugemalira katika masuala mbalimbali ya
kikanisa na kijamii,” alisema.
Mamilioni yaingia
Kuhusu
fedha hizo, Askofu Nzigilwa alisema katika moja ya mawasiliano yao
Februari mwaka jana, Rugemalira alimuomba namba ya akaunti yake ya Benki
ya Mkombozi ili aweke matoleo yake... “Kwa kuniomba akaunti hiyo
nilijua anataka kuweka matoleo ya fedha; lakini kiasi alichokuwa amenuia
kukiweka sikukijua mpaka nilipoangalia Bank Statement na kuona kampuni
ya VIP Engineering imeingiza Sh40.4 milioni katika akaunti hiyo Februari
27, 2014.
“Niliwasiliana na Ndugu Rugemalira na
kumwambia nimeona kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yangu; naye
akaniambia hayo ni matoleo ambayo anaamini yatasaidia katika shughuli
zetu za kitume na kichungaji. Nikamshukuru kwa ukarimu huo mkubwa,”
alisema.
Alisema matoleo hayo yalipokewa kwa moyo
mnyofu kutoka kwa mtu anayefahamika kwa ukarimu wake katika kusaidia
Kanisa na watumishi wake.
“Biashara na kampuni
anazomiliki Rugemalira kwa mujibu wa sheria za nchi haviwezi kumpa shaka
mtu anayemfahamu uwezo wake au kampuni yake kutoa mchango mkubwa kama
huo.”
Kazi za matoleo
Huku
akisema tangu apokee fedha hizo hakuna mamlaka yoyote iliyowahi kumhoji
Askofu Nzigilwa alisema matoleo ya waumini hutumika katika shughuli na
uendeshaji wa jimbo, parokia na taasisi zake; katika miradi maalumu
iliyokusudiwa na pia kwa kadri ya matakwa na lengo la mtoaji.