Warudia njiani wakienda kula Mwaka Mpya kwa Lowassa

Arusha. Baadhi ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wamerudia njiani baada ya kupata taarifa za kutokuwapo kwa sherehe ya kupokea mwaka mpya ambayo hufanyika kila mwaka nyumbani kwake Monduli ikijumuisha mamia ya watu kutoka ndani na nje ya nchi.
Lowassa amekuwa akifanya sherehe hiyo kwa zaidi ya miaka mitano lakini mwaka huu hakufanya kutokana na kutumia adhabu ya CCM.
Msaidizi wa Lowassa, Aboubakar Liongo alisema jana kuwa mwaka huu, sherehe hazikufanyika kutokana na Lowassa kuwa katika adhabu ya CCM inayomzuia kukutana na idadi kubwa ya watu ili kuepuka kuonekana ni sehemu ya kampeni.
Lowassa anatumikia adhabu ya miezi 12 ya kutoshiriki masuala yanayoashiria kampeni itakayomalizika mwezi ujao.
Wengine katika kifungo hicho, ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Alisema kama kuna watu waliofika Monduli, walikuwa hawana taarifa za kutokuwapo sherehe hiyo ambayo wameizoea kila mwaka.
Katika sherehe kama hii mwaka jana, Lowassa alitangaza kuanza safari ya matumaini ambayo alieleza itawezesha kupatikana huduma bora za afya na elimu bure. Hata hivyo, alisema safari hiyo imejaa miba na mabonde na kuwataka wanaomuunga mkono, kusimama kuhesabiwa. Tamko hilo, lilizua mjadala nchi nzima na baadhi wakahusisha na safari ya urais.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja katika hotuba yake, alipinga tabia ya baadhi ya wanasiasa kutaka kuwachagulia marafiki.
Mmoja ya wananchi waliokuwa safarini kwenda Monduli, John Kaaya mkazi wa Arumeru, alisema walikuwa hawana taarifa za kutokuwapo kwa sherehe hiyo ambayo alisema amekuwa akiihudhuria kwa miaka miwili
Powered by Blogger.