Uamuzi kesi ya kina Mdee Januari 15
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Januari 15, mwaka huu, itatoa uamuzi katika kesi inayomkabili
Mbunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chadema, Halima Mdee (35) na wenzake
wanane wa kufuta shtaka la pili linalowakabili washtakiwa hao ama la.
Uamuzi huo ulipaswa kutolewa jana na Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda uliahirishwa.
Washtakiwa
hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi
ya kufanya mkusanyiko usio halali. Wakili anayewatetea, Peter Kibatala
aliiomba mahakama kulifuta shtaka hilo la pili katika kesi hiyo kwa
madai kuwa lina upungufu wa kisheria.
Shtaka
linaloombwa kufutwa ni la kufanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la
kutembea kwenda kwenye Ofisi ya Rais kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16.
Kwa upande wa
wakili wa Serikali, Mohammed Salum, aliiomba mahakama kulitupilia mbali
ombi hilo kwa madai kuwa hakuna madhara ama upungufu katika shtaka hilo
na siyo lazima kila kifungu kitajwe.
Awali, washtakiwa
hao walipokuwa wakisomewa maelezo yao ya awali mahakamani hapo,
waliyakubali kuwa ni maelezo yao binafsi na kuyakana mashtaka yote
yanayowakabili mahakamani hapo.
Washtakiwa wengine ni
pamoja na Rose Moshi, Renina Peter, Anna Linjewile, Mwanne Kassim,
Sophia Fangel, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatu Mmari. Kwa pamoja
wanadaiwa kuwa Oktoba 4, 2014, katika Mtaa wa Ufipa, bila kuwa na
uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa
Polisi, Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
Ilidaiwa
kuwa, washitakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 124
cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.