Pinda aionya CCM uteuzi wa wagombea
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda akifurahi na wananchi wa Halmashauri ya Nsimbo,
Wilaya ya Mlele baada ya kuwasili kwenye viwanja vya halmashauri hiyo
kuhutubia mkutano wa hadhara akiwa kwenye ziara katika jimbo lake la
uchaguzi. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Katavi. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezitaka ngazi mbalimbali
za uteuzi wa wagombea wa CCM kuwapa wananchi nafasi kuchagua watu
wanaowataka ili kuepuka kupoteza viti katika uchaguzi.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akiwahutubia maelfu ya
wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mikutano
wa Kashaulili, Mpanda mkoani hapa.
Pia alitumia
mkutano huo kuaga jimboni humo akisema muda wa kuendelea kuwa Mbunge wa
Katavi umetosha na sasa anatafuta kitu kingine cha kufanya.
Kwa
mara ya kwanza, Pinda alichaguliwa kuwa Mbunge wa Mpanda Mashariki
(sasa Katavi) mwaka 2000 na ameongoza jimbo hilo kwa mihula mitatu.
Kuhusu uteuzi
Akizungumzia
uteuzi wa wagombea mbalimbali, Pinda aliwaasa viongozi wa CCM kuwateua
watu wanaofaa kugombea uongozi kwenye nafasi mbalimbali wale ambao
wanakubalika na wananchi na wawape nafasi wananchi kuchagua mtu
wanayemtaka.
Alisema haifai CCM kuwalazimisha kwa
kuwachagulia wananchi kiongozi wasiyemtaka... “Kumekuwa na tabia ya
kuteua watu ambao hawakubaliki kwa wananchi na matokeo yake watu hao
wamekuwa wakishindwa kwenye uchaguzi... acheni chuki, msiteue watu
kuwania uongozi kwa ajili ya kupewa pesa na urafiki,” alisema.
Pinda
aliyetangaza ni ya kuwania urais kimyakimya, aliwataka Watanzania
kutowachagua watu wanaotaka kiti hicho na vile vya ubunge na udiwani kwa
kutanguliza fedha.
“Watu hao wanaotafuta uongozi kwa
kutoa rushwa kwa wananchi ni hatari, kuweni makini kwa kuchagua viongozi
waadilifu watakaoongoza kwa kutanguliza mbele utaifa kuliko masilahi
yao binafsi.
“Wako watu wanaotaka uongozi kwa kuhonga
wapigakura, watu wa namna hiyo hawafai kuwa wagombea wa urais, ubunge na
udiwani kwa kuwa si waadilifu na wakishapata uongozi kamwe hawezi
kuwajali wananchi kwanza watataka kurudisha fedha walizotoa.
“Hakikisheni
mnachagua viongozi ambao wanaweza kuwaongoza kwenye maeneo yenu na siyo
vinginevyo, achaneni na watu wanaowapa pesa hao hawatawapeleka kokote
badala yake watakuwa viongozi wabinafsi kwa kutanguliza masilahi yao
mbele na kuwasahau wananchi waliowaweka madarakani,” alisema Pinda.
Alisema:
“Watu wanaotaka uongozi kwa fedha, wanapowaletea hizo pesa kuleni
lakini mhakikishe wakati wa uchaguzi hamwapigii kura.”
Huku
akishangiliwa na wananchi hao kwa makofi na vigelegele, alisisitiza:
“Ukitaka kumchagua mtu mwenye sifa za kuwa rais wa nchi hii, chagueni
mtu ambaye hatoi rushwa kwa wananchi, mwadilifu, mnyenyekevu na
mchapakazi. Hata watu wanaotaka ubunge na udiwani hakikisheni
hamwachagui wanaotaka uongozi kwa rushwa, chagueni viongozi
watakaowaongoza vizuri kwenye maeneo yenu.”
Viongozi wa dini
Waziri
Mkuu aliwataka viongozi wa dini kuachana na masuala ya kuhubiri siasa
wanapokuwa kwenye nyumba za ibada na badala yake wafanye kazi
wanayotakiwa kufanya ya kuhubiria neno la Mungu.
“Kumeanza
kusikika maneno kuwa viongozi wa dini wanaendeleza chuki kwa kuhubiri
siasa kwenye nyumba za ibada badala ya kutenda kazi zao za kuwapa neno
la Mungu waumini wao.
“Viongozi hawa wajibu wao ni
kufanya kazi ya kuwaongoza waumini kwa kuwahubiria neno la Mungu kuliko
kutumia nyumba za ibada kuhubiri siasa, kufanya hivyo ni kukiuka maadili
ya kazi zao.
“Kama wanataka kufanya siasa waje hapa
majukwaani tupambane sawasawa... kama mtu anaweza aje apambane hapa,”
alisema Waziri Mkuu.
Alisema viongozi wa dini washirikiane na Serikali na chama hasa tawala (CCM), katika kuhubiri upendo na amani lakini si siasa.
“Ninaogopa
kuona kiongozi wa dini anakwenda kanisani kisha anasema chagueni Chama
cha Mapinduzi, ni hatari. Nafasi walizonazo ni za kidini na zinatakiwa
kuheshimiwa,” alisema na kuongeza kuwa kuacha hayo yakiendelea ni hatari
kwa Taifa kwani na kunaweza kuleta mgogoro katika jamii.
Waziri
Mkuu leo anakamilisha ziara yake mkoani Katavi kwa kufanya mkutano wa
hadhara kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ifukutwa, Mpanda.