Jaji Manento: Sitasahau mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi




 
 Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento
Dar es Salaam. Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento amesema jambo kubwa alilolipitia wakati wa uongozi wake lilikuwa ni kifo cha mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi baada ya kupigwa bomu na polisi, mkoani Iringa mwaka 2012.
Alisema jambo hilo lilikuwa kubwa kwa wananchi kuliko lilivyopokelewa na Serikali. Alisisitiza kuwa tume yake ilitoa taarifa ya kifo hicho ikiwa na mapendekezo na kuikabidhi Serikali. Jambo la kushangaza, alisema mapendekezo yao hayajatekelezwa mpaka leo.
“Hili jambo kwangu lilikuwa kubwa. Tume tulifuatilia tukio lile na kubaini kuwa Mwangosi alipigwa bomu na polisi. Tulitoa mapendekezo yetu, lakini mpaka leo hakuna utekelezaji wake,” alisema Manento ambaye pia ni Jaji Kiongozi mstaafu.
Aliongeza kuwa sasa ni kazi ya Nyanduga kufuatilia utekelezaji wa maazimio yale ili kuhakikisha haki inatendeka na kujenga imani ya tume kwa wananchi.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 129 (1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora namba saba ya mwaka 2001.
Jukumu kubwa la tume hii ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo, tume imepewa mamlaka ya kupokea malalamiko kutoka sehemu mbalimbali na kuanzisha uchunguzi wake yenyewe kama itaona kuna ukiukwaji wa haki.
Tume ya Haki za Binadamu ilitoa mapendekezo matano wakati wa taarifa yake juu ya kifo cha Mwangosi. Baadhi ya mapendekezo hayo yalikuwa ni: elimu ya vyama vya siasa na sheria ya polisi kuhusu vyama vya siasa kutolewa kwa askari polisi, ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.
Maoni mengine yalikuwa ni: Jeshi la polisi na msajili wa vyama vya siasa kuepuka kufanya maamuzi ambayo yatasababisha hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanatekeleza majukumu yao.
Kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya, zilitakiwa kuwa makini na vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.
Pia, tume ilipendekeza kuheshimiwa na kulindwa kwa misingi ya demokrasia ya vyama vingi nchini.
Awali, Rais Kikwete alimwapisha Msajili wa Mahakama ya Rufani, Katarina Revocati ambaye aliahidi kuendeleza nguvu iliyoanzishwa ya kuleta mabadiliko katika mhimili wa Mahakama na kuufanya utende kazi zake kwa ufanisi.
“Baada ya mabadiliko ya sheria, ofisi ya msajili imebaki na kazi ya kushughulikia mashauri tu. Kuanzia mwaka jana majaji walianza kuzunguka mikoani kusikiliza kesi za muda mrefu. Nina tumaini nitasaidia kuongeza nguvu katika mpango huo,” alisema.
Alitaja changamoto kubwa iliyo mbele yake kuwa ni mlundikano wa kesi nchi nzima bila kusikilizwa.
Alisema hatua zimeshachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo na kuwa majaji walianza na mikoa ya Tabora na Dar es Salaam.
Naye mwenyekiti mpya wa tume hiyo, Bahame Nyanduga alisema tume itashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na asasi za kiraia katika kusimamia haki za binadamu hasa mwaka huu wa uchaguzi mkuu.
Nyanduga aliyasema hayo jana baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam kushika wadhifa huo. Sambamba naye, pia aliapishwa Makamu Mwenyekiti, Iddi Mapuri na makamishna wanne ambao ni Mohamed Hamad, Kelvin Mandopi, Rehema Ntimizi na Salma Hassan.
“Katika uongozi wangu, nitashirikiana na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na utawala bora ili kujenga jamii ya Watanzania katika msingi wa haki na usawa.
Powered by Blogger.