Lema naye ‘apanda kizimbani’ Hai
Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema (wa pili kushoto) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai juzi baada ya kutoa ushahidi katika kesi ya utapeli inayomkabili Adam Abeid. Picha na Dionis Nyato.
Hai. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amedai mshtakiwa
aliyejifanya Jaji mstaafu, Barnabas Samatta, alimtisha kuwa
angehakikisha anashindwa katika rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge.
Lema alidai kuwa baada ya kutotoa ushirikiano, mtu huyo alimtisha kuwa atahakikisha jimbo hilo linarudi CCM.
Lema
alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya
Hai, Denis Mpelembwa katika kesi ya kutaka kuwatapeli viongozi wa
Chadema.
Mbunge huyo alitoa ushahidi siku moja baada ya
Jaji huyo mstaafu kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Mbali ya
Samatta shahidi mwingine, Profesa Abdallah Safari alitoa ushahidi.
Kesi
hiyo inamkabili Adam Abeid, ambaye wakati kosa hilo linadaiwa kutendeka
kwa kutumia simu, alikuwa ni mtahiniwa binafsi (private candidate) wa
mtihani wa Taifa wa kidato cha sita.
Lema, mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, alitoa ushahidi wake juzi kwa kuongozwa na
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(Takukuru), Susan Kimaro.
Alisema mara tu baada ya
kuvuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha 2012, alipokea taarifa
kutoka kwa John Heche kuwa alikuwa akitafutwa na Wakili wa Chadema,
Profesa Abdallah Safari.
“Nilimtafuta Profesa Safari
akaniambia natafutwa na Jaji Samatta, akanipa namba yake nikampigia,
lakini hakupokea akanitumia ujumbe yuko kwenye kikao nitume meseji,”
alidai Lema.
Lema alidai baadaye mtu huyo aliyejitambulisha kama
‘Jaji Samatta’ alimtumia meseji akimpa pole kwa kuvuliwa ubunge na
kuahidi angemsaidia na kila alipojaribu kumpigia alikuwa akitaka
wawasiliane kwa meseji.
Aprili 12, 2012, Lema alidai
kutumiwa meseji na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa iliyokuwa
imetumwa kwake na mtu huyo aliyekuwa akijifanya Jaji Samatta ikisomeka:
“Mheshimiwa
Slaa kesho nakwenda Dar kuonana na Chande ili tufanye mazungumzo ana
kwa ana tujue nini kitaendelea, hivyo naomba unigharimie mafuta ya
kwenda Dar.”
Lema alidai ujumbe huo ulimtia shaka
kwamba wanayewasiliana naye siyo Jaji Samatta, bali ni tapeli na
kumtumia meseji: “Wewe ni tapeli na tutakukamata.”
Lema
alisema kuwa mshtakiwa alimtumia ujumbe: “Umeamua kuniita tapeli, poa
nitahakikisha rufaa yako unashindwa na nitafanya juu chini CCM ichukue
dola yetu.”
Lema alidai kumjibu mtu huyo kuwa mkono wa
sheria uko nyuma yake, naye akamjibu kuwa labda Tundu Lissu awe hakimu
na yeye (Lema) awe ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na mahakama iwe
nchini Kenya.
“Ilipofikia hapo ndipo sasa tutakubaliana
kumtaarifu rasmi Jaji Samatta kwamba kuna mtu anatumia jina lake vibaya
na kutoa taarifa Takukuru,” alisema.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 14 mwaka huu.