Hukumu CCM ndani ya saa 72
ADVERTISEMENT
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM, itakuwa na vikao vizito
kuanzia Jumatatu kujadili masuala mbalimbali yanayokikabili chama hicho.
Mambo
makubwa yanayotarajiwa kuchukua nafasi katika vikao hivyo vitakavyoanza
saa 72 zijazo ni kuwajadili wanachama wake ambao baadhi ni mawaziri
waliokumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na tathmini ya
wanachama wake sita walio katika adhabu ya mwaka mmoja baada ya kutiwa
hatiani kwa kudaiwa kufanya kampeni za urais kabla ya muda.
Pia
kamati hiyo, inatarajia kutumia vikao hivyo kuangalia namna ya kupata
wagombea watakaokubalika na wananchi kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha
Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Akiwa
katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kuipa CCM ushindi kwenye
uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tanga hivi karibuni, Katibu Mkuu wa
CCM, Abdurahman Kinana alisema chama hicho kitaanza rasmi vikao vyake
vya ngazi ya Taifa kupitia masuala mbalimbali yanayokihusu.
Alipoulizwa
kuhusu agenda hizo katika vikao hivyo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye alikuja juu na kusema hakuna kitu kama hicho...
“Hata mkiiandika vibaya CCM, itashinda tu,” na kisha kukata simu. Hata
hivyo, habari zilizopatikana jana jioni kutoka ndani ya CCM, zinasema
kuwa sekretarieti ya chama hicho, inakutana leo mjini Dodoma kuandaa
ajenda za kikao hicho kitakachoanza Jumatatu ijayo.
Mawaziri
waliokumbwa na kashfa ya escrow ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya
CCM.
Profesa Tibaijuka tayari ameondolewa kwenye
nafasi yake ya uwaziri baada ya kukiri kupewa Sh1.6 bilioni na
Mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalila.
Wengine
waliotajwa kupewa mgawo na Rugemalila ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na
Katiba, William Ngeleja.
Pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo yupo katika uchunguzi kuhusiana na kashfa hiyo.
Mbali
na wahusika wa Akaunti ya Escrow, kikao hicho cha Kamati Kuu ya CCM
kitachunguza maadili ya viongozi wakiwamo waliokumbwa na zuio la
kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa
ikifuatiliwa.
Watakaojadiliwa ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine
ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira na
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja.
Kinana akiwa Tanga
alikaririwa akisema: “Wiki ijayo tunaanza kukaa vikao vya kupimana sisi
viongozi juu ya uadilifu wetu ndani ya Serikali, tunataka kuwa na
viongozi wenye kujua Watanzania wanataka nini na uadilifu wao usiwe hata
na chembe ya shaka.”
Alisema salamu za CCM kwa
Watanzania kwa mwaka 2015 ni ahadi ya kuweka mkazo katika maadili kwa
viongozi wake na kwamba itafanya tathmini kwa lengo la kujipanga kwa
uchaguzi mkuu ujao.
“Watanzania wanataka viongozi
wasiokuwa na urasimu umangimeza, wenye mlolongo wa itifaki na wanaoweza
kushuka chini,” alisema Kinana.
Msingi wa hukumu
Kikao
cha tathmini cha wiki ijayo ni mfululizo wa baada ya kikao cha mwisho
cha Agosti mwaka jana kilichokutana chini ya Mwenyekiti wake, Philip
Mangula kupitia taarifa za utekelezaji wa adhabu kwa makada sita wa
chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais kabla ya wakati.
Kufanyika
kwa kikao hicho kulitokana na agizo la Mangula ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa CCM, alilolitoa Februari 8, mwaka jana akizitaka ofisi
zote za ngazi ya mikoa na wilaya kufungua mafaili kupitia mienendo ya
wagombea walioanza kampeni za uchaguzi wa kuteuliwa kugombea urais kabla
ya wakati. Makada hao waliozuiwa kujihusisha na kampeni kwa miezi 12 na
adhabu zao zinamalizika Februari 18.
Hatua ya kufanyia
tathmini hiyo ni kutokana na kuelezwa kuwa pamoja na adhabu hiyo,
baadhi yao walikuwa wakikiuka na kuendelea na mikakati ya kampeni kwa
kukusanya watu wa kupanga nini cha kufanya tayari kwa uchaguzi wa mwaka
huu.
Katika kikao hicho cha Kamati Ndogo ya Maadili na
Nidhamu, ilielezwa kuwa katika kipindi cha miezi kadhaa, timu za maofisa
usalama wa chama zilisambazwa mikoa yote na kukusanya taarifa za makada
hao.
Kikao kama hicho cha Kamati Kuu kilikutana Julai
16, mwaka jana na kupokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa
CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kuwania urais.
Kutokana
na hali hiyo, Kamati Kuu iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na
kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada hao sita.
Siku
moja baadaye, Julai 17, mwaka jana, Nape alisema endapo Kamati ya
Usalama na Maadili itabaini kama makada hao walikiuka mwenendo wa
utekelezaji wa adhabu waliyopewa, watapoteza sifa... “Baada ya
kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili
wasipoteze nia ya kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na
taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo.