CCM yalaani vurugu kuapishwa kwa viongozi Serikali za mitaa
Katibu wa NEC; Itikadi na Uenezi CCM taifa Nape Nnauye
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani vikali vurugu
zilizofanywa na wafuasi wa Chadema na CUF kwa viongozi wa serikali za
mitaa katika maeneo kadhaa nchini ikiwemo mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam
na Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa
NEC; Itikadi na Uenezi CCM taifa, Nape Nnauye amesema vurugu hizo mbali
na kuhatarisha na kuharibu mali pia zilizosababisha baadhi ya viongozi
wa CCM kujeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali.
Amesema
vurugu hizo zimetokea katika mkoa wa Mwanza ambapo Christopher Mgeta
kutoka Mtaa wa Ibungilo na Pascal Charles wa Mtaa wa Kitangiri A katika
wilaya ya Ilemela walivamiwa na kupigwa wakati wa kuapishwa.
Alieleza
kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Sultan Jeta wa mtaa wa Ukwamani
katika jimbo la Kawe alifanyiwa fujo na wafuasi hao na Mtaa wa Msisiri A
Kata ya Mwananyamala katika Jimbo la Kinondoni Juma Mbena alipigwa na
kuvunjwa mkono.
“Katika Manispaa ya Ilala, wafuasi wa
vyama vya upinzani walifanya vurugu wakati wa kuapishwa kwa viongozi wa
serikali za Mitaa, jambo lililopelekea zoezi hilo kuahirishwa.
Nnauye amesema katika Mkoani Mbeya pia vurugu za aina
hiyo zimetokea katika wilaya za Kyela na Rungwe ambapo wilayani Kyela
zoezi la kuapisha viongozi wa serikali za mitaa lilishindika na
kuahirishwa kutokana na vurugu za kurushiwa mawe zilizofanywa na wafuasi
wa Chadema walioletwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Aliongeza
kuwa katika Kijiji cha Ilundo wilayani Rungwe wafuasi hao wa Chadema
waliwapiga mawe viongozi na wanachama wa CCM na baadae kufyeka mashamba
yao ya migomba na kusababisha vijana sita kujeruhiwa na kulazwa katika
hospitali ya wilaya ya Rungwe kwa sababu ya hasira za kushindwa
uchaguzi.
“Vurugu hizi ni mwendelezo wa tabia na mazoea
ya vyama vya upinzani nchini kutoheshimu na kufuata sheria na taratibu
za nchi, tabia hizi si za kiungwana na ni uthibitisho wa kuharibikiwa
na kufa kwa vyama vya upinzani nchini. Mara zote wamekuwa wakikataliwa
na wananchi kwa kura, wao hukataa uamuzi huo wa wananchi kwa kufanya
fujo na vitimbi, ”amesema Nnauye.
Wakati haya ya kijiri
kesho Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
itakutana Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kupanga ajenda
zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya Chama hicho itakayokutana Zanzibar Januari 13.
Aidha
msemaji wa jeshi la Polisi SSP Advera J. Bulimba amesema jeshi hilo
halitawaonea huruma wale wote watakaohusika katika vurugu, kwani
litawachukulia hatua kali za kisheria, badala yake limewaasa wananchi
ambao hawakuridhika na uchaguzi huo kufuata taratibu husika.-