Mufti: Mataifa ya Magharibi yanatugombanisha
Tanga. Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Bin Simba
amewataka Watanzania kutoichezea amani iliyopo na kusema wengi hawaioni
thamani yake kwa kuwa wamezaliwa na kuikuta.
Aidha,
amewataka wasikubali kufarakana kama baadhi ya mataifa ya Magharibi
yanavyotaka kwa kubuni mbinu za kuwagombanisha ili yafanye biashara ya
silaha.
Akihutubia kwenye mkesha wa Maulid ya
kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye
Uwanja wa Shule ya Msingi Mazoezi, Korogwe, Mufti aliwaasa Waislamu
kumuenzi kiongozi huyo kwa kuimarisha mshikamano na amani.
Alisema
Mtume Mohammad (S.A.W) alipozaliwa alikuta dunia ikiwa imevurugika kwa
kukosa amani na hakukuwa na utaratibu maalumu, lakini alitumia juhudi
kubwa kuleta amani kwa kujenga ustaarabu kwa kuyakutanisha makundi
yaliyokuwa yakigombana na kuyasuluhisha.
“Mtume
Mohammad (S.A.W) alisawazisha sera za watu ambao kazi yao kubwa ilikuwa
kuwagombanisha wanadamu, pia aliwakutanisha mahasimu ndipo amani
ikapatikana,” alisema Mufti Simba.
Alisema njia pekee
ya kudumisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Mohammad (S.A.W) ni kwa Waislamu
kuepuka mbinu chafu za kufarakanishwa ili waonekane wavurugaji wa amani
wakati ukweli ni kinyume chake.
Mufti Simba aliwataka
waumini hao kujenga moyo wa kujitolea kifedha kwa ajili ya kueneza dini
yao pia aliwataka kuchangia elimu akisema hakuna ya bure kuanzia ile ya
dunia hadi ya dini.
Makamba
Akihutubia katika Maulid hayo, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliwataka Watanzania
wasifanye majaribio kwa kumchagua rais anayetoa fedha kusaka wadhifa
huo.
“Kiongozi wa namna hiyo, hataongoza kwa haki, watu
wanaotoa fedha nyingi kusaka uongozi na wanaotumia makundi kamwe
hawataongoza kwa haki. Tuwakatae viongozi wa namna hii,” alisema Makamba
ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania urais, huku akisisitiza kuwa
Watanzania watafanya kosa la mwaka kumchagua rais ambaye atakuwa amepita
kwa kutoa fedha nyingi katika kusaka wadhifa huo.
Akihutubia
umati mkubwa wa waumini wa Kiislamu Makamba alisema: “Msikubali
kuwachagua hawa wanaotumia fedha na mbinu nyingine za kuwagawa kwa
makundi, kwani hao si viongozi wanaohitajika kuliongoza Taifa la
Tanzania,” aliongeza: “Tanzania inahitaji kiongozi atakayewaunganisha
wananchi wote kuwa kitu kimoja, mwenye busara na subira lakini si
anayeutaka uongozi kwa njia yoyote hata kama ni kuwagawa kwa makundi au
kutumia fedha ili mradi aweze kuchaguliwa.
Makamba
ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), aliwataka Watanzania kuhakikisha
kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba unapita salama, kwani nchi nyingi hasa za
Afrika zinakuwa kwenye migogoro na mapigano wakati wa uchaguzi.
“Uchaguzi
Mkuu unaokuja ni moja ya jaribio la nchi yetu, ili kufanya uchaguzi
vizuri, itabidi tukumbuke urithi tulioachiwa, nao ni amani.
“Ili kufanikisha hili, kila mwanasiasa ni lazima ahubiri amani. Pili viongozi wa dini waendelee kuuombea uchaguzi huo,” alisema.
Makamba
aliwataka Waislamu kuwasomesha watoto wao elimu dunia kwa kuwa
itawasaidia kuwa wataalamu hivyo kwenda sanjari na ulimwengu wa sayansi
na teknolojia, huku akinukuu kitabu kitukufu cha Quran kuwa waitafute
elimu hata ikibidi mpaka China.
Naibu waziri huyo
aliwaomba masheikh kutochoka kuliombea Taifa ili livuke mtihani mkubwa
wa kupiga kura za maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu,
mambo ambayo yote yamepangwa kufanyika mwaka huu.
Baraza
la Maulid kitaifa, lilifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri mjini hapa
na mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk
Abdallah Kigoda ambaye aliwataka Waislamu kuwasomesha elimu zote watoto
wao ili waweze kuwa na ujuzi mbalimbali.