Kafulila: Ni zamu ya wapinzani kushika dola
Mbunge wa Kigoma Kusini, NCCR-Mageuzi, David Kafulila.
Uyole. Mbunge wa Kigoma Kusini,
NCCR-Mageuzi, David Kafulila amesema kama upinzani utashindwa kuchukua
nchi mwaka huu, basi CCM itaendelea milele kuongoza Tanzania.
Oktoba
mwaka huu, Tanzania inaingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa
rais, wabunge na madiwani baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda
wake.
Akihutubia Mkutano wa hadhara uliofanyika Shule
ya Msingi, Hasanga Uyole, mkoani Mbeya, Kafulila alisema kuwa Watanzania
wataendelea kuwa maskini huku keki ya Taifa ikiliwa na vigogo wachache.
“Huu
ni wakati wa kujiangalia...watu wanalalamika kila siku, hali ya
umaskini inaongezeka na kila kukicha ni kilio, sasa ni wakati wa kufanya
uamuzi,” alisema Kafulila.
Alisema umaskini wa
Mtanzania umechangiwa kwa kiasi kikubwa na wezi wa rasilimali za nchi,
huku Watanzania walio wengi wakitaabika.
“Mimi nasema,
upinzani ukiingia Ikulu haya yote yatamalizika, kila Mtanzania
atafurahia rasilimali zake, lakini wakiing’ang’ania CCM watabakia
hivyo,” alisema.
Kafulila alisema kuwa ikiwa
watashindwa kuitoa CCM na ikafanya vizuri katika kila eneo, Watanzania
hasa wapinzani watabaki kwenye uongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji
walivyopata katika uchaguzi uliopita kwa miaka mitano mingine.
Akizungumzia
sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Escrow, Kafulila
alirudia kusema kuwa pamoja na kuibuliwa wachache, lakini kuna msururu
mrefu wa wahusika.
Kafulila alisema kuwa pamoja na Rais
Kikwete kumfuta kazi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka bado hajakata kiu ya Watanzania kuwatimua
wengine.
Profesa Tibaijuka aliondolewa kwenye wadhifa wake baada ya kujipatia Sh1.6 bilioni kutoka kwenye akaunti ya Escrow.
Akimzungumzia
Waziri wa Nishati, Profesa Sospeter Muhongo, Kafulila alisema Rais
hajakata kiu ya Watanzania kwa kushindwa kumchukulia hatua Muhongo.
“Huu mtandao wa uchotwaji fedha unafahamika, sasa kwa nini Ikulu inakuwa na kigugumizi dhidi ya Profesa Muhongo?” alihoji.
Kafulila
alielezea wasiwasi wake kuwa Profesa Muhongo huenda asiondolewe kwa
njia za kawaida, lakini anaweza kuondolewa kwa mashinikizo kwa vile Rais
hana nia ya kumwondoa licha ya kukubali kuyafanyia kazi maazimio ya
Bunge.