IPTL,Tanesco sasa wagongana angani
Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Singh Sethi.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Wakati Kampuni ya kufua
umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) chini ya uongozi wa
Kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Ltd (PAP), ikitangaza
kupunguza bei ya umeme kwa asilimia 20 baada ya kufanya marekebisho
makubwa ya injini za mtambo wake, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
limesema halina taarifa yoyote.
“Tunatarajia hatua za
upanuzi kwenda haraka kuhakikisha kuwa IPTL inatoa huduma bora ya
uhakika na nafuu kwa Taifa hili. Ningependa kutoa shukrani zangu kwa
uongozi wa Tanesco kwa kukubali umeme unaozalishwa na IPTL,” ilisema
taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Singh
Sethi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,
Felchesmi Mramba aliliambia gazeti hili jana kuwa hana taarifa hizo na
kwamba kama kuna punguzo lolote, IPTL ilitakiwa kulijulisha rasmi.
“Taarifa
hizi tunazisikia tu ila hatujaelezwa rasmi. Sisi tunachokifanya sasa ni
kutekeleza maazimio yaliyotolewa na Bunge,” alisema Mramba.
Ingawa
Mramba hakufafanua utekelezaji huo, katika azimio lake la saba kati ya
manane, Bunge liliazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua
mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la
kuokoa fedha za shirika hilo.
Hata hivyo, Serikali kwa
kupitia Rais Jakaya Kikwete imesema hilo likifanywa na Serikali pekee
linaweza kuwatisha wawekezaji kuja nchini.
Hivi
karibuni baada ya Bunge kutoa maazimio yake yaliyotokana na Ripoti ya
Kamati yake ya Hesabu za Serikali (PAC), Sethi alikaririwa na gazeti
hili akisema anafikiria mara mbilimbili kuendelea kuwekeza nchini.
Punguzo la IPTL
IPTL
ilieleza kuwa ilifanya marekebisho ya mitambo hiyo kwa saa 36,000 kazi
ambayo ilikamilika mwaka jana, huku ikitangaza pia kuwa bei yake ya
umeme inatarajiwa kushuka zaidi kulingana na kushuka kwa bei ya mafuta
mazito.
IPTL pia ilisema marekebisho hayo yaliyotumia
zaidi ya Dola za Marekani 25 milioni, yameiwezesha mitambo yake kuwa
katika nafasi nzuri ya kuzalisha umeme wa uhakika kwa kufikia megawati
100 na kuingiza kwenye Gridi ya Taifa.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Sethi, kampuni hiyo imepunguza bei ya umeme wake
inaoitoza Tanesco na sasa utakuwa chini ya bei ya awali iliyokokotolewa
ya senti 23 Dola za Marekani kwa kilowati ikiwa na maana kwamba bei hiyo
imepungua kwa senti 4.6 za Dola.
“IPTL inajivunia
kutangaza kuwa imefanikiwa kufanya marekebisho makubwa ya mashine zake
kwa saa 36,000 ya kufanya kazi, zoezi lililokamilika ndani ya mwaka
2014. Nimeomba timu ya IPTL kupanga mapema jinsi wanavyoweza kuongeza
juhudi zaidi kufikia marekebisho ya saa 48,000 kwa awamu inayofuata
mwaka 2015. “Tunatarajia uwapo wa IPTL kuwa bora zaidi kwa kuwa sasa
tunajipanga kuongeza rasilimali zaidi. Hii ni sehemu ya ahadi ya PAP
kuhakikisha IPTL inaendeshwa vizuri na kwa ufanisi. Wakati sasa umefika
kwa Tanesco kuwa na uhakika wa kupata umeme wa uhakika wa megawati 100
kwenye Gridi ya Taifa wakati wowote utakapohitajika.
“IPTL
chini ya PAP haiangalii tu uzalishaji wa umeme wa kutosha, pia ipo
makini kuhakikisha umeme huo wa kutosha unakuwa nafuu. Kwa maana hiyo,
tumeamua kushusha bei zetu za umeme kufikia chini ya bei iliyokokotolewa
ya hapo awali ya Dola senti 23 za Marekani kwa uniti, ambayo sasa
inaleta jumla ya punguzo la bei la asilimia 20 kwa ile iliyokuwa
ikitozwa na IPTL kabla ya PAP kuchukua uongozi,” alisema.
Sethi
alisema Tanesco itarajie punguzo zaidi la bei ya umeme kufikia kiwango
cha chini ya Dola senti 8 za Marekani kwa uniti baada ya mitambo ya IPTL
kupanuliwa na kufikia uzalishaji wa megawati 500, mitambo yake ikitumia
gesi asilia.
Alisema mpango wa upanuzi wa mitambo hiyo
unaendelea vizuri, akiongeza kuwa ipo hatua za awali za uchanganuaji na
upimaji udongo.