Watuhumiwa 510 mtandao wa panya road wakamatwa Dar
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova
Vijana 510 wanaodaiwa kujihusisha na vitenda vya kihalifu
chini ya kundi maarufu la ‘panya road’ wamekamatwa na jeshi la Polisi
Kanda Maalum jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.
Watuhumiwa
hao wamekatwa katika mikoa ya kipolisi ya Kinondoni, Temeke na Ilala
ambapo jeshi la polisi limefanya msako mkali kuweza kuwabaini lengo
likiwa ni kuimarisha ulinzi nchini.
Kamishna wa Polisi
Suleiman Kova ametoa wito kwa wazazi wa watoto hao kutofika kwenye vituo
ambavyo wamehifadhiwa mpaka watakapo kamilisha uchunguzi wao dhidi yao.
Kamanda
Kova amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa maeneo mbalimbali ikiwamo
kwenye vijiwe huku wengine wakifuatwa katika nyumba wanazoishi baada ya
polisi kupata taarifa za kinterenjensia.
“Tulipowapekua
watuhumiwa hawa tuliwakuta na vichocheo kadhaa vya uhalifu ambavyo ni
puli za bangi 113, kete zake 676, na misokoto 294 na vinginevyo, pia
kati yao wapo wakubwa zao watatu ambao ndiyo vinara wa mgogoro”.amesema
Kova
Amesema operesheni ya kupambana na ‘Panya Road’
itakuwa endelevu hadi pale jina hilo ambalo limekuwa gumzo jijini
litakapotoka kabisa masikioni mwa watu.
Aidha kamanda
Kova amesema jeshi la polisi kwa sasa limejipanga katika kutoa mafunzo
maalum kupitia wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa mikoa yote ya
kipolisi ili kukabiliana na vitendo hivyo vya uhalifu.
“Ni
ukweli usiopingika kuwa vijana wanao fanya vitendo hivi wanafamika kwa
wananchi wa eneo husika lakini wanakuwa wasiri kufichua uovu huo hivyo
kupitia mafunzo haya yatasaidia kuondoa tatizo hili,” amesema Kamishna.
Januari
2 mwaka huu hali ya taharuki, hofu na wasiwasi mkubwa iliwakumba
wakazi wa jiji hilo kwa saa mbili baada ya kundi maarufu la waporaji la
Panya Road, kuvamia mitaa mbalimbali na kupora mali.