Membe: Siwaonei wivu maswahiba wa mafisadi
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hapendi ufisadi na
anajua mafisadi hawampendi lakini, hawaonei wivu watu wanaopendwa na
mafisadi.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya
Dayosisi ya Dar es Salaam ya Kanisa la Anglikana Tanzania, ambayo
alikuwa mgeni rasmi, Membe alitumia nafasi hiyo kuwataka waumini wa
kanisa hilo kupambana na ufisadi katika ngazi zote nchini.
“Ninatosheka
kupendwa na wale wenye mapenzi mema na Taifa letu. Sipendi rushwa na
ufisadi. Ninashukuru Mungu kuwa rushwa, ufisadi na mafisadi hawanipendi
zaidi,” alisema Membe.
Membe ambaye ni mbunge wa Mtama
mkoani Lindi, alisema si jukumu la viongozi pekee au chama fulani pekee
kupambana na ufisadi, bali ni wajibu wa kila mmoja kwa kuwa mafisadi
wako katika ngazi zote.
“Ninaamini, mwaka huu, wengi
wetu tukisema hivyo, tukasimama katika mstari huo na tukaenda hivyo,
ufisadi hauwezi kutushinda. Kila mmoja asipuuze udogo wa sauti yake au
uchache wetu dhidi ya wale waovu, maana hata mwale mdogo wa mshumaa
hufukuza giza,” alisema Membe na kuongeza:
“Wako wanaotoboa mtumbwi wetu tunaosafiria pamoja na jitihada zetu za kupiga makasia.”
Kuhusu
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Membe ambaye pia anatajwa kuwania urais,
alisema mwaka huu ni wa kipekee si tu kwa dayosisi hiyo inayoadhimisha
miaka 50, bali pia kwa Watanzania wote: “Mwaka huu una mambo makubwa
mawili yaliyo mbele yetu, yaani kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa
na Uchaguzi Mkuu.
“Uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu
kwani tunachagua rais mpya atakayeunda Serikali mpya ya awamu ya tano
ambaye anatarajiwa kuendeleza mema ya awamu ya nne na awamu zilizopita
na kutoa majawabu kwa changamoto za sasa na zijazo.”
Nchi majaribuni
Membe
alisema nchi inapita katika majaribu na mitihani mikubwa kutokana na
tatizo la mmomonyoko wa maadili katika ngazi zote kuanzia familia,
shule, ofisini na serikalini.
“Tunalo tatizo la
ufisadi, ukatili dhidi ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi na
tunalo pia tatizo la umaskini. Tunalo tatizo la kupoteza uvumilivu wa
kidini na kisiasa.”
Aliongeza kuwa Watanzania wengi wamefika mahala wanaanza
kukata tamaa na kupoteza matumaini: “Kimsingi, waumini wamekata tamaa
na kupoteza hofu ya Mungu kiasi cha wengine kukimbilia kwenye nguvu za
giza, uganga na unajimu. “Tunahitaji kutoka hapa. Tunajiuliza wote,
tunatokaje”.
Aliliomba Kanisa na waumini waliombee
Taifa ili Mungu awaongoze kuchagua viongozi wenye uwezo, busara na
hekima ya kutatua changamoto zinazolikabili Taifa.
“Tuchague
viongozi waadilifu, wazalendo, wachapa kazi, wasio na uchu wa madaraka
kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi na marafiki zao.
“Ninawasihi
viongozi wa dini muongeze juhudi za kuhubiri umoja na kutoa mafundisho
ya kuhimiza udugu na mshikamano miongoni mwa waumini na Watanzania kwa
jumla. Watu wapendane na washirikiane bila kujali itikadi za vyama vyao
au ushabiki kwa wagombea. “Tukumbushane kuwa chaguzi zinakuja na
kuondoka lakini amani yetu, usalama wetu, udugu wetu na umoja wetu ndiyo
nguzo kuu za uwepo wa Taifa letu.
Askofu Mokiwa
Askofu
wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa
alisema ni wakati mwafaka kwa vijana kujitambua na kutokubali kutumiwa
na baadhi ya wanasiasa kwa masilahi yao binafsi.
Dk
Mokiwa alisema kuwa vijana wanatumiwa na wanasiasa kwa sababu wengi wao
hawana ajira, hivyo wanasiasa hao wanatumia mwanya huo kuwarubuni ili
kutimiza malengo yao kisiasa ambayo hayana faida kwao.
“Vijana
ndiyo wenye hii nchi, hivyo ni wakati wenu kusimama imara ili Taifa
hili lisonge mbele, pia msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa hasa
wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu,” alisema askofu huyo.
Alisema
katika siku za karibuni vijana wamegeuka walinzi wa masilahi binafsi
tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita ambayo walijitoa kwa ajili ya
kutetea na kuilinda nchi.
Dk Mokiwa aliwataka wananchi
wasikubali kugawanywa kwa misingi ya tofauti za kiitikadi hasa katika
mchakato wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu.
“Tusikubali
makundi haya yakavunja umoja wetu,” alisema Dk Mokiwa na kuongeza kuwa
umoja ukitoweka hata hawa ‘panya road’ wataendelea kufanya maovu.