Mbinu mpya za kusafirisha dawa za kulevya
Alisema mara nyingi watu waliomeza dawa hizo hukamatwa kwa kuhisiwa na baada ya kupekuliwa huamriwa kuruka kichura au kujisaidia ili kujua iwapo wana ‘mzigo’ tumboni.
Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake wa
Kitanzania waliofungwa katika magereza ya China na Hong Kong, walishika
ujauzito kama moja ya mbinu ya kupitisha dawa za kulevya bila
kugundulika kwenye viwanja vya ndege na mipaka mingine ya kimataifa.
Mwananchi limebaini.
Watanzania wanne walio katika
magereza ya China na Hong Kong walijifungua watoto kwa nyakati tofauti
wakiwa wanatumikia vifungo na wamekiri kuwa walibeba ujauzito kama mbinu
ya kupitisha dawa hizo bila kukaguliwa.
Watoto
wanaozaliwa magereza baada ya kufikisha mwaka mmoja hupelekwa katika
vituo vya watoto yatima na kusomeshwa na Serikali ya China hadi pale
wazazi wao watakapomaliza adhabu.
Imebainika kuwa
watoto wawili wapo katika vituo hivyo, mmoja tayari yupo Tanzania baada
ya bibi yake kumrejesha na mwingine bado yupo gerezani na mama yake.
Wanawake
hao ambao wote wana umri wa kati ya miaka 20 na 30 walieleza masikitiko
yao jinsi ambavyo wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya
wanavyowarubuni ili kubeba dawa hizo kwa ahadi za kuwapa fedha nyingi.
“Tunapata
mimba makusudi kwa sababu tulijua kuwa katika viwanja vya ndege vingi
wajawazito hawakaguliwi hasa wakiwa na mimba kwa hiyo tungebeba unga na
kuupeleka China, halafu baadaye tungerudi nchini na kutoa mimba au
tukiamua tunajifungua,” alisema mmoja wa wafungwa hao.
Hata
hivyo, mbinu hiyo ilifanikiwa katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), lakini haikufua dafu katika viwanja vya ndege vya
China, Hong Kong, Macau na Guang Zhou.
Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athuman alisema hana taarifa za
Watanzania hao lakini ofisi yake inafanya taratibu za kuwasiliana na
China ili kujua hali za wanawake hao.
Mkurugenzi wa
JNIA, Moses Malaki alisema kwa kawaida kila mtu hukaguliwa kwa uangalifu
bila kujali mjamzito au la. Akielezea namna wanavyopimwa, Malaki
alisema kwanza kila msafiri hupimwa kwa mashine ya kawaida ambayo
hubaini uwepo wa kifaa chochote kisichotakiwa mwilini kwa mfano chuma
kama hereni, bangili, mikanda lakini si ndani ya tumbo.
“Iwapo
mashine ya awali itatoa mlio hata baada ya msafiri kutoa vitu vya
chuma, basi atatakiwa kwenda katika chumba maalumu cha ukaguzi wa
mikono,” alisema.
Kamanda wa kitengo cha Polisi cha
Dawa za Kulevya, (SACP), Godfrey Nzowa alisema wapo wanawake kadhaa raia
wa Zambia, Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini na Malawi ambao wamefungwa
katika magereza ya Tanzania kwa kusafirisha dawa za kulevya wakitumia
mbinu hiyo ya ubebaji wa mimba.
Alisema mbinu hizo zinatumiwa na wanawake kwa sababu
wajawazito hawakaguliwi kwa mashine za x-ray na kwamba wengi walikamatwa
kutokana na taarifa za kikachero.
“Hata magereza ya
hapa tunao na wamejifungua watoto wakiwa gerezani, lakini wajue kabisa
kuwa watakwepa mashine lakini taarifa zinatusaidia na ndiyo maana nasema
taarifa ni nguvu,” alisema.
Pamoja na kukamatwa kwa
raia wa kigeni wanaotumia mbinu hiyo, Kamishna Nzowa hakuwa na taarifa
za Watanzania waliokamatwa nje ya nchi kwa kutumia mbinu hiyo.
Septemba
mwaka jana, raia wa Canada, Tabitha Ritchie alikamatwa kwenye Uwanja wa
Ndege wa Columbia kwa kubeba dawa za kulevya kwenye mimba ya bandia,
mbinu ambayo ilibainika baada ya kuhojiwa na maofisa wa uhamiaji kuhusu
umri wa mimba yake na walipomgusa tumboni walibaini kuwa tumbo lilikuwa
baridi na gumu.
Askari mmoja wa Kitengo cha Dawa za
Kulevya wa JNIA, (jina linahifadhiwa), alieleza wazi kuwa hakuna mashine
ya kujua mtu aliyemeza dawa hizo zaidi ya kuhisi tu kwa mbinu za
kiaskari.
Alisema mara nyingi watu waliomeza dawa hizo
hukamatwa kwa kuhisiwa na baada ya kupekuliwa huamriwa kuruka kichura au
kujisaidia ili kujua iwapo wana ‘mzigo’ tumboni.
Hata
hivyo, askari huyo alisema kwa kawaida wajawazito hawawezi kurushwa
kichura au kulazimishwa wajisaidie kutokana na hali zao.
Miongoni
mwa wanawake waliobeba mimba kwa ajili ya kubeba dawa za kulevya na
wasichana maarufu nchini, mmoja wao mtoto wake sasa analelewa katika
kituo cha watoto yatima China.
Baada ya kupata taarifa
hizo, Mwananchi ilizitafuta familia za wafungwa hao ambazo hazikuwa na
taarifa kuwa na ndugu zao walikuwa na ujauzito walipokuwa wakisafiri.
Baadhi ya waliohojiwa walisema walipata taarifa za ndugu zao kuwa na watoto wachanga lakini hawakuwa na habari za ujauzito.
“Hata
hivyo, ninamshukuru Mungu kwa kuwa amepata mtoto na anaendelea vizuri,
kutokana na uwezo wetu kuwa mdogo siwezi kwenda kumchukua mjukuu wangu
huko Hong Kong, mwache akae kituoni hadi mama yake atakapoachiwa,”
alisema mama wa mmoja wa wafungwa hao.