Mwanasheria Mkuu aahidi kuanza na mikataba tata
Rais
Jakaya Kikwete akimkabidhi vitendea kazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju baada ya kumwapisha katika hafla iliyofanyika Ikulu,
jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju amesema ataanza kuipitia mikataba yote inayodaiwa
kuwa na utata ili aweze kutoa ufafanuzi wa kina lakini akawataka
Watanzania wampe muda.
Hata hivyo, alisema hadhani kama
watu wanaosema kuwa baadhi ya mikataba iliyoingiwa na Serikali ina
utata wako sahihi na kuwataka Watanzania kuwa na imani na Serikali
iliyopo madarakani.
“Watu wanasema hivyo ila kuna jambo moja ambalo wanatakiwa kujua kuwa kuna baadhi ya mikataba ambayo ni siri,” alisema.
Masaju
aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki kuchukua nafasi ya
Jaji Frederick Werema ambaye alijiuzulu kutokana na sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Jaji Werema aliomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusu suala hilo haukueleweka na badala yake kuchafua hali ya hewa.
Kabla ya uteuzi huo, Masaju alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kuhusu
uteuzi wake, alisema; “Nina furaha kwa sababu ninalitumikia Taifa na
kuteuliwa kwangu kunaonyesha kuwa Serikali ina imani na mimi.”
Licha
ya kubanwa na wanahabari kuwa kwa nafasi aliyokuwa nayo awali anafahamu
maeneo yenye matatizo, ikiwamo na mikataba yenye utata, alisisitiza
kuwa apewe muda zaidi.
Katika mkutano wa 16 na 17 wa
Bunge uliohitimishwa Novemba 28 mwaka jana, Bunge lilitoa maazimio
manane, likiwamo la Jaji Werema kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria
kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu mabilioni ya fedha kutoka akaunti
ya Tegeta Escrow.
Maazimio mengine yalikuwa ni kuwajibisha baadhi ya mawaziri na bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Kutokana
na maazimio hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi amesimamishwa kazi, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amefukuzwa kazi na kuteuliwa kwa bodi
mpya ya Tanesco.