Aua, ajiua, aacha ujumbe wa kurasa nne
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela akiwaonesha wandishi wa
habari ujumbe ulioachwa na marehemu Emmanuel Moshi baada ya kumuua
mfanyabiashara mwenzake Didas Alphonce kwa kumkata na shoka kichwani na
kisha yeye kujiua kwa kujinyonga. Picha Joyce Joliga
Songea. Mfanyabiashara wa mbao Manispaa ya
Songea, Emmanuel Moshi (40), mkazi wa Marangu, mkoani Kilimanjaro
amemuua mfanyabiashara mwenzake aliyetambuliwa kwa jina la Didas
Alphonce (64), mkazi wa Kilema Kilimanjaro kwa kumpasua kichwa kwa
shoka, kisha yeye mwenyewe kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani katika
stoo ya nyumba waliyokuwa wakiishi.
Inadaiwa kuwa Moshi alichukua uamuzi huo baada ya Alphonce kumdhulumu zaidi ya Sh87.4 milioni.
Wakizungumza
na gazeti hili jana, watu wa karibu na wafanyabiashara hao ambao
hawakupenda majina yao kuandikwa kwenye gazeti, walidai kuwa
wafanyabiashara hao walikuwa wakiishi nyumba ya ndugu yake, Didas na
kufanya biashara za kuuza mbao pamoja.
Walidai kuwa,
Desemba 30 mwaka jana, wafanyabiashara hao walikuwa wakinywa pombe
kwenye Bwalo la Magereza na Moshi alikuwa akilalamika kudhulumiwa na
Didas.
Mashuhuda hao waliongeza kuwa tangu siku hiyo, wafanyabiashara hao hawakuonekana tena hadi jana.
Ilidaiwa kuwa, mwenye nyumba huyo alitumia funguo zake
za akiba kufungua nyumba hiyo na kukuta mwili wa mjomba wake ukiwa
umepigwa na shoka na tayari umeanza kuharibika.
Mtu
mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi alitoa taarifa kituo cha polisi na
walipofika waliubaini pia mwili wa Moshi aliyejinyonga.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai uchunguzi wa awali unaonyesha wafanyabiashara hao
walikuwa wanadaiana pesa.
Alisema Mosha ameacha ujumbe mrefu wa karatasi nne aliouandika kuhusiana na mauaji hayo.
Ujumbe
huo: “Kataeni wadhulumaji kati ya matajiri na maskini, nimeondoa dhambi
kubwa ya dhuluma iliyokuwa ikinitesa ulimwenguni, wadhulumaji
wasifumbiwe macho jamii iniunge mkono kuondoa watu hawa. “Dhuluma
aliyonifanyia mtu huyu imekatisha maisha yangu.”