Mlipuko wajeruhi watoto wanne
MAJERUHI:
Emmanuel Mwingira ambaye ni mmoja kati ya watoto sita waliolipukiwa na
kitu kilichokuwa kimetengenezwa na nyaya nyingi wakati wakicheza katika
Mtaa wa Kiwandani Mbinga Mjini, akiwa amelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma. Picha na Joyce Joliga.
Mbinga.Watoto wanne kati ya sita
wamenusurika kifo, wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma baada ya kulipukia na
kitu ambacho kimeunganishwa na nyaya nyingi, kinachodaiwa kutumika
kulipulia miamba ambacho kimewajeruhi vibaya.
Taarifa
za awali ambazo zilisambaa mjini Mbinga, ilielezwa kuwa mlipuko huo
ulitokana na kitu ambacho kilidhaniwa kuwa ni bomu ambalo limetengenezwa
kienyeji, jambo ambalo siyo kweli.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Mihayo
Msikhela, alithibitisha kuwa, tukio hilo lilitokea Januari 2, saa 5:30
asubuhi katika Mtaa wa Kiwandani mjini Mbinga mkoani Ruvuma, wakati
watoto hao wakiwa wanachezea vilipushi hivyo walivyoviokota kwenye
jalala.
Msikhela alikitaja kitu hicho kuwa ni vilipushi
ambavyo vinadaiwa kuwa vinatumika na watafiti wa madini migodini au
walipuaji baruti na akieleza kuwa tukio hilo ni la bahati mbaya na
liliwakumba watoto hao baada ya kuokota kifaa hicho jalalani.
Aliwataja
watoto waliolipukiwa kuwa ni Philiberth Mbungu (10), Augustino Millanzi
(5), Geofrey Ndunguru (8) na Emmanuel Mwingira (7) ambao wote
wameumizwa sehemu mbalimbali na wengine wawili Ayubu Methew (10) na
Hassan Mapangi (5) wakiwa na majeraha ya kawaida mwilini.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Elisha Robert
alifafanua kuwa mtoto Philiberth na Augustino wamehamishiwa katika
hospitali ya mkoa iliyopo Songea kwa matibabu zaidi.
Alisema
watoto hao wamepelekwa huko kutokana na kujeruhiwa vibaya sehemu za
usoni pamoja na machoni, ambapo kuna vipande vidogo vidogo vya vyuma
vimeingia ndani yake.
“Niliamua kuchukua hatua ya
kuwapeleka hospitali ya mkoa ili wakapatiwe matibabu zaidi kutokana na
jinsi nilivyowaona hali zao siyo nzuri na mimi naendelea kufuatilia
kujua hali zao zinaendelea aje huko, lakini taarifa nilizonazo mpaka
sasa tayari wamepokewa na wamehudumiwa,” alisema Robert.
Aliongeza
kuwa Geofrey na Emmanuel wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali
hiyo ambapo nao wamejeruhiwa usoni na mikononi na hali zao zinaendelea
vizuri.
Kamanda Msikhela alisema uchunguzi unaendelea
kuhusu tukio hilo na alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwa
waangalifu na watoto wasiwaachie wakitembea hovyo, hivyo pale wanapoona
kitu chenye muunganiko wa nyaya wasikiguse bali watoe taarifa mapema
kwenye vyombo vya usalama ambavyo vipo karibu nao.