UHALIFU: Mbaroni kwa ubakaji Kigoma
Kigoma. Kiongozi mmoja wa dini
anayejihusisha na uganga wa jadi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za
kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Ujiji
iliyopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed alikiri kiongozi huyo anayedaiwa
ni mtoa mawaidha katika Msikiti wa Wagoma uliopo Ujiji mjini Kigoma
alikamatwa baada ya kumbaka Mtoto mwenye umri wa miaka 14.
Alimtaja
mtuhumiwa ni Hassan Bamba (42) ambaye licha ya kuwa mganga wa jadi,
amekuwa akitumia nyumba yake iliyopo Ujiji kuwabaka kina mama
wanaokwenda kwake kutafuta tiba.
Akisimulia mkasa huo,
mtoto aliyebakwa, mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa), alisema
alifika nyumbani kwa Bamba Januari 1, 2015 kuchukua dawa za kumuwezesha
kusoma kwa bidii kama walivyoelekezwa na mtuhumiwa.
Baada
ya kumtuma Shule ya Sekondari Kitongoni kuchukua mchanga katika vichupa
vidogo viwili, alipofika alimwambia aingie chumba cha kutibia wagonjwa
na kumwamuru avue nguo za ndani.
“Nilikataa,
akanikamata kwa nguvu na kunivua nguo zangu, halafu akachukua mafuta ya
mgando akachanganya na dawa nyeusi, akaanza kunibaka,” alisimulia mtoto
huyo huku akilia.
Anadai licha ya kupiga kelele lakini
sauti haikutoka kwa vile nyumba hiyo ina madirisha ya vioo yasiyopenyeza
sauti nje kwa urahisi.
Kabla ya kumbaka binti huyo
inadaiwa alitaka kumbaka ndugu yake waliozaliwa pacha, lakini alishindwa
baada ya mtoto huyo kuwahi kukimbia na kurudi nyumbani kwao.
Binti
huyo alisema siku mbili kabla ya kumbaka, mganga huyo aliwafunga kamba
kiunoni na zilitolewa Desemba 31, 2014 akidai ni sehemu ya tiba.
Baba
wa binti aliyebakwa, Athuman Omary alisema Desemba 27, 2014 akiwa na
watoto wake wakienda shule alikutana na Bamba aliyeanza kuhoji juu ya
watoto na kuomba awatengenezee dawa ya kuwafanya wafaulu mitihani kwa
daraja la juu.
“Nilimwambia hakuna tatizo kama ataweza
kwa vile ni jambo la kielimu. Akaniomba nitafute madafu sita ili wanangu
wakaanze tiba, na Jumapili ya tarehe Desemba 28, 2014, tiba ikaanza,”
alisema Omary.
Licha ya baadhi ya viongozi wa dini
kuendesha vikao vya kutaka suala hilo limalizwe nje ya mahakama kwa
madai ya kuficha aibu ya mganga huyo wa jadi, familia ya mtoto huyo
imekataa.
Bibi ya mtoto, Mwamvua Hamisi aliisema
kitendo hicho kimedhalilisha familia yao na wanaomba vyombo vya dola
vichukue hatua na kuamua kwa haki bila upendeleo wowote.