Mapya yaibuka vurugu za Panya Road
Ayubu Mohamed maarufu Diamond enzi za uhai wake.
-
Dar es Salaam. Baada ya saa 24 kupita tangu
kundi maarufu la waporaji la Panya Road, kuvamia na kusababisha
shughuli mbalimbali kusimama kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, chanzo
cha uhalifu huo kimebainika.
Hali hiyo iliwafanya wakazi wa jiji hilo kusitisha shughuli mbalimbali kutokana na kuhofia usalama wao, huku usafiri ukiadimika.
Tukio
hilo linaelezwa lilitokea ikiwa ni ishara ya kundi hilo kumuenzi
mwenzao aliyefikwa na mauti akidaiwa kutaka kuiba pikipiki.
Mkazi
wa Magomeni Kagera, Mohamed Chalamira alisema, “Wakati wakitoka kuzika
walikuwa wakiambiana kuwa mwanajeshi hawezi kuuawa na kuzikwa bila
kupigwa mizinga hivyo tutakwenda kulianzisha ili polisi wapige mabomu na
ndicho kilichotokea.”
Aliongeza: “Ni tukio
lililotuacha tukishangaa, kwani polisi mmoja aliyekuwa na silaha alitaka
kumkamata mwenzao, lakini alipotoa panga tu yule polisi alikimbia, hii
haiwezekani yaani polisi anakimbia mhalifu? Ilikuwa saa 9 vijana
waligeuza eneo hilo (Magomeni Kagera) kama eneo lao.”
Kuhusu
vijana waliokamatwa Chalamira alisema: “Hao vijana wawili waliokamatwa
mmoja kweli anahusika, lakini mwingine ni hahusiki kwani dereva, huyo
mshikaji atasota huko wakati hahusiki, polisi wafanye uchunguzi wao
kwani haiwezekani kundi hili likasababisha mtafaruku...Mimi mwenyewe
juzi nimepoteza simu na nimeumia hapa katika goti.”
Familia yazungumza
Kaka
mkubwa wa marehemu, Mohamed Ayubu maarufu ‘Diamond’, Moshi Hamadi
alisema mdogo wake huyo alizaliwa mwaka 1995 Magomeni Kagera na kukulia
kwenye familia hiyo, lakini aliondoka kutokana na tabia zake kuanzia
kubadilika.
Alisema Ayubu hakubahatika kumaliza elimu
ya msingi kutokana na kujiingiza katika makundi ya wavuta bangi akiwa
darasa la nne na alipoonywa hakukubali na alichukia na kuamua kuondoka
nyumbani kwao.
“Huyu alikuwa ni mtoto wa pekee kwa mama
yake, hakuwahi kupata mtoto mwingine, ndiyo maana hawezi kuzungumza
presha imempanda,” alisema Hamad baada ya mwandishi kuomba kuzungumza na
mama yake mzazi na alijibiwa hivyo.
Kauli ya Hamadi
iliungwa mkono na mama mkubwa wa marehemu Ndam Moshi ambaye alisema
Ayubu hakutaka vitendo vyake vijulikane na alipokuwa akienda kuwasalimia
walipomgusia kwamba siku hizi anajihusisha na masuala ya wizi alikuwa
anakataa na kulia kutwa nzima.
Kuhusu taarifa za kifo
chake, Hamadi alisema walipigiwa simu na vijana wasiowafahamu
kuwataarifu kuwa Diamond amefariki dunia kwa kukatwa mapanga eneo la
Tandale kwa Mtogole ambako kulikuwa na mkesha wa Mwaka Mpya.
Mkazi
wa Tandale karibu na eneo walipouona mwili wa Ayubu ambaye hakutaka
kutajwa jina lake alisema: “Tuliamka asubuhi juzi (Januari Mosi) na
kuambiwa kuna mwili umetupwa pale darajani (Daraja la Kwa Sindano
linalotenganisha Tandale na Sinza-Yemen).”
Aliongeza:
“Hapo ilikuwa kama saa tatu asubuhi, tuliukuta mwili wa kijana huyo
ukiwa uchi wa mnyama huku tofali kubwa likiwa limewekwa kichwani
kwake...Polisi walikuja na kuondoka nao mwili wa marehemu hatukujua
walipokwenda kuuhifadhi.”
Hamadi alisema mwili wa
marehemu waliukuta katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ukiwa umekatwa
kwa mapanga maeneo ya kichwa na kuufanya kuharibika na miguu ikiwa kama
imechomwa moto na ukiwa hauna nguo.
Mama mkubwa wa
marehemu Ndam alisema kuwa hajawahi kukaa msibani kwa wasiwasi kama
msiba huo, alisema kilichokuwa kinatokea nje katika msiba huo kilitaka
kusababisha mauti ya mama yake Ayubu kutokana na presha, kwani kulikuwa
na idadi kubwa ya vijana ambao hakuwafahamu.
Kwa nini msiba huo umehusishwa na Panya Road?
Hamadi
alisema walipokuwa wanarudi na mwili wa marehemu kutoka Muhimbili
walikuta kundi kubwa la wahuni limetanda maeneo ya jirani na nyumbani
kwao na kadiri walivyokuwa wakisogea ndiyo walizidi kukuta umati wa
wahuni.
Alifafanua hakuwa akimfahamu hata kijana mmoja
kati yao wala ndugu zake hakuna aliyekuwa akiwafahamu kila mtu kwenye
familia hiyo alikuwa anashangaa.
“Baada ya kufika
waliupeleka mwili wa marehemu moja kwa moja Msikiti wa Magomeni Kagera
uitwao Masjid Rahman kwa ajili ya kuswalia, kwani kila kitu kuosha na
kuuandaa mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi ilifanyika Muhimbili,”
alisema Hamadi.
Hali ilikuwaje msikitini hadi makaburini
Tofauti
na kauli zilizokuwa zikitolewa na wengi kuwa maziko ya kijana huyo
yalitawaliwa na vitendo vya kihuni, Shekhe Hassan Khamisi Majaliwa
ambaye ni babu wa marehemu na ndiye aliyeongoza mazishi ya kijana Ayubu
alisema hakukuwa na vurugu hadi walipomaliza kuzika.
“Baada
ya kupokea mwili uliswaliwa kabla ya swala ya saa kumi na baada ya
kuuswalia na kutoka nje ndipo vijana hao ambao kwa miaka 40 niliyoishi
hapa sikuwahi kuona umati wa vijana kama hao...Vijana hao waliupokea
mwili na kuubeba wenyewe kistaarabu na kumkataza mtu yeyote kushika
jeneza kwa madai kuwa hawamfahamu kama wanavyomfahamu wao.”
“Walipofika
katika makaburi ya Kihata (nyuma ya msikiti huo) aliwataka watulie na
wao kwa wao wakawa wanatulizana isipokuwa mmoja wao alikuwa kalewa na
alishika betri ya simu alikuwa akifanya kama vile anachukua picha, baada
ya kisomo wakati mwili unafukiwa akalirusha hilo betri likafukiwa na
udongo hicho ndiyo kitu pekee kilichowekwa ndani ya kaburi hilo,”
alisema Sheikh Majaliwa.
Alisema baada ya mazishi
kumalizika aliwataka vijana wasifanyie fujo za aina yoyote katika eneo
hilo kwa sababu lawama itakua kwao.
“Walikubali, lakini
nilikuwa nasema kujifurahisha, kwani sura zao zilivyokuwa nilifahamu
lazima watafanya fujo na kweli walifanya hivyo,” alisema.
Aliongeza:
“Tulipokuwa tunatoka makaburini saa 11.45 jioni tuliwakuta polisi
wametanda maeneo haya na walipoona kundi la watu waliwatawanya vijana
hao kwa kufyatua risasi.”
Mashuhuda wazungumzia
Vijana
waliokuwa kwenye kijiwe cha Magomeni Kagera ambao hawakuwa tayari
kutaja majina yao waliliambia gazeti hili kuwa hali ilikuwa mbaya kwani
kila mtu alikuwa anakimbia kunusuru roho yake.
Walisema
Polisi wakiwa ndani ya gari waliloegesha eneo hilo kuna dada aliibiwa
simu na hao Panya Road, lakini vijana wa eneo hilo wakawakimbiza na
kuwanyang’anya simu na kumrudishia mwenyewe huku, Polisi wakitizama
tukio hilo.
Vijana waliokuwa kijiwe eneo la Tandale kwa
Mtogole walisema walikuwa wanamfahamu Ayubu wakati wa uhai wake, lakini
hawakuwa wakijua kijiwe chake maalumu ni wapi kwa sababu alikuwa
anafahamika kila kona.
Kaniki
Katika
hatua nyingine makamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam, akiwemo
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, wametakiwa
kutodharau taarifa za uhalifu zinazotolewa na wananchi kwa kisingizio
cha madai ya uvumi.
Taarifa toka ndani ya Jeshi la
zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa hayo yalielezwa na Naibu
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Abdulrahman Kaniki alipokutana na
makamanda hao katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya
jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Naibu IGP,
alisisitiza kwa makamanda hao umuhimu wa kuthamini na kuzifanyia
uchunguzi wa haraka taarifa za uhalifu zinazotolewa na wananchi.
Panya road 36 mbaroni
Kamanda
wa Kanda Maalum ya Dar es Sala Seleima Kova alisema tangu tukio hilo
lilipotokea wameendelea na msako mkali na kufanikiwa kuwatia nguvuni
vijana 36.
“Tunawashikilia vijana 36 na msako huu
unaendelea, tunawakamata wale wote wenye rekodi ya kufanya
uhalifu...tunawaomba wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuepuka
kutuma taarifa ambazo hawana uhakika nazo ambazo kwa namna moja au
nyingine zinahatarisha usalama,” alisema Kova
Baadaye,
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,
Advera Bulimba alisema, “Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa vijana hao
wanaojihusisha na vikundi hivyo kuacha tabia hiyo mara moja. Tumejipanga
vizuri katika mikoa yote kuhakikisha kwamba nchi inaongozwa kwa kufuata
utawala wa sheria, hatutamwonea mtu yeyote ama kikundi cha watu
wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na kutia hofu wananchi.”
Kamanda
wa Polisi wa Ilala, Mary Nzuki alisema kijana mmoja ameuwawa eneo la
Kipunguni-Mombasa jijini Dar es Salaam saa 10 alfajiri ya kuamkia jana