Rais Kikwete amteua Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amemteua
George Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akichukua nafasi
iliyoachwa na Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu Desemba 16 kutokana na
kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu uteuzi huo
ulianza rasmi Ijumaa, Januari 2, 2015 na anatarajiwa kuapishwa kesho.
Kabla
ya uteuzi wake, Masaju alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
aliwahi pia kuwa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Katika barua yake ya kujiuzulu kwa Rais, Jaji
Werema alisema kuwa alifikia uamuzi huo kwa sababu; “Ushauri wake
kuhusiana na suala la Escrow haukueleweka na umechafua hali ya hewa.”
Uamuzi
wa Werema ulitokana na maazimio ya Bunge ya kutaka yeye na baadhi ya
vigogo wachukuliwe hatua kutokana na madai ya kuhusika kwenye sakata la
uchotwaji fedha katika akaunti hiyo.
Mwanasheria huyo
alilalamikia maazimio hayo, akisema hayakuwa ya haki kwa wote
waliotuhumiwa na uamuzi huo ulifanywa kwa hasira na kufuata mkumbo.
Bunge
liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kutokana na
kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya
Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwe kwa Kampuni ya IPTL iliyo na
mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya kukata kodi.
Jaji huyo hakusalimu amri wakati Bunge likijadili tuhuma dhidi yake, akisema anaamini alichofanya na kutaka abebeshwe msalaba.