Siri nzito uteuzi wa mawaziri
Dar es Salaam. Wakati wowote Rais Jakaya
Kikwete anatarajia kuipanga safu mpya ya Baraza la Mawaziri kwa kuteua
waziri mwingine wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya
kumwondoa aliyekuwepo, Profesa Anna Tibaijuka.
Mara
nyingi katika uteuzi wake Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa
kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri
wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao
anatokea waziri aliyeondolewa.
Profesa Tibaijuka ambaye
ni Mbunge wa Muleba Kusini mkoani Kagera anakuwa waziri wa tatu kutoka
mkoa wa Kagera kuondolewa madarakani katika uwatala wa Rais Kikwete.
Ameondolewa kutokana na kukabiliwa na kashfa ya uchotaji wa fedha
katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wengine walioondolewa
kutoka mkoa huo ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki kutokana na kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Nazir Karamagi aliyeondolewa kutokana na sakata la Richmond.
Iwapo
Rais Kikwete atazingatia utaratibu wake wa kuteua waziri kutoka mkoa
ambao waziri aliyeondoka anatoka, huenda nafasi iliyoachwa wazi na
Profesa Tibaijuka kuchukuliwa na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini),
Gosbert Blandes (Karagwe).
Assumpter Mshama (Nkenge),
Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini), Eustace Katagira (Kyelwa), Deogratius
Ntukamazina (Ngara) na Dk Antony Mbasa (Biharamulo Magharibi).
Kama
akitumia utaratibu wa kumpandisha naibu mawaziri, huenda nafasi hiyo
ikachukuliwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
George Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe au naibu mawaziri kutoka
wizara nyingine kama alivyowahi kufanya mara nyingi.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho inampa mamlaka
Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa ameshawateua wanane na kubakiza
nafasi mbili pekee.
Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza.
Wabunge
hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa) na Profesa Makame Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia).
Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo
(Nishati na Madini), na Saada Mkuya (Nishati na Madini) na Janet Mbene
(Naibu Waziri Viwanda na Biashara) na Dk Asha-Rose Migiro.
Dk
Migiro aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Wabunge ambao
wameteuliwa na Rais, lakini hakuwapa uwaziri mpaka sasa ni Zakia Meghji
na James Mbatia.
Waliowahi kupandishwa
Pia Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu waziri kuwa mawaziri.
Amefanya
hivyo kwa Dk Nchimbi ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo. Awali alikuwa
Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwingine
ni aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye
kabla ya kushika nafasi hiyo alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo wakati
huo ikiongozwa na Shamsa Mwangunga.
Kagasheki pia alipandishwa kutoka naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hadi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Rais
Kikwete alipoingia madarakani alimpandisha aliyekuwa Naibu Waziri wa
Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Anthony Diallo kuwa
Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
Mwingine
aliyepandishwa ni William Ngeleja, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, baadaye alipandishwa kuwa waziri kamili katika
wizara hiyo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kuitumikia nafasi ya naibu Waziri
wa Wizara ya Ujenzi.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami, aliteuliwa na Rais Kikwete kushika
wadhifa huo baada ya kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Celina
Kombani aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), baadaye alipandishwa na kupewa Wizara ya Katiba na
Sheria. Hivi sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), ofisi
aliyopewa kuiongoza tangu mwaka 2012.
Kwa upande wake,
aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo, kabla ya
kupewa nafasi hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Mawaziri waliohimili mitikisiko
Pamoja
na kuwapo kwa panga pangua ndani ya baraza la mawaziri, wapo baadhi yao
ambao wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo tangu Rais Kikwete aingie
madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen
Wassira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli. Wengine ni Profesa
Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia na Dk Mary Nagu.
Kauli ya wasomi
Mhadhiri
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms, alisema;
“Tatizo ni mfumo. Serikali ya awamu ya nne imekuwa na udhaifu katika
mfumo wake wa kufuatilia utendaji kazi wa watumishi wa Serikali. Rais
Kikwete alipoingia madarakani alitembelea kila wizara na kusisitiza
uwajibikaji, ila sidhani kama amekuwa akifuatilia wizara zinatenda
yapi.”
Aliongeza, “Nadhani hata watendaji wa Serikali wameshajua kuwa Rais siyo mfuatiliaji nao wanafanya mambo watakavyo.”
Alisema
jambo kubwa linaloitafuna nchi ni vigogo wa Serikali kufanya kazi kwa
kulindana, kukosekana kwa dhamira ya uwajibikaji na kupeana nafasi za
kazi kwa kujuana na akisisitiza kuwa mtumishi bora ni yule mwenye uwezo
na dhamira ya kufanya kazi.
Profesa wa sheria katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chris Maina alisema; “Ili kupata kiongozi
mzuri ni lazima anayemteua au kumpendekeza awe na uhakika kuwa mtu
hisika ni mwadilifu, hicho ndiyo kigezo kikubwa. Pili, lazima mtu huyo
awe mtendaji na utamjua kwa kutazama kazi alizozifanya awali, yaani
historia yake katika utendaji.” Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya
Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema,
“Tatizo ni mfumo. Hatuna mfumo unaowandaa watu kimaadili, hilo
limesababisha hata jamii nzima kukosa maadili ambayo ndiko wanakotoka
hao mawaziri na viongozi wengine.”
Alisema hata vyombo
vya kusimamia uwajibikaji, rushwa na maadili ni dhaifu. “Vyombo hivi
havina meno na unaweza kudhani kuwa vipo kwa ajili ya kuwalinda watu
fulani fulani tu. Nchi za Ulaya huwezi kukuta yanatokea mambo kama ya
hapa kwetu kwa sababu wana vyombo vinavyofuatilia watendaji kwa ukaribu
zaidi na kuwachukulia hatua wanaokiuka maadili,” alisema Profesa
Makulilo.