Ahadi za JK zaitesa CCM
Nape asema Rais ametekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi zake, wasomi , wanasiasa wasema utekelezaji ni mdogo
Dar es Salaam.
Ahadi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi katika mikutano
mbalimbali nchini wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, huenda
zikawa mwiba kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka
huu, kutokana na nyingi kutokutekelezwa au kuwa katika hatua za mwanzo.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa nyakati tofauti
alitoa ahadi kusaidia kuwakwamua wananchi kutoka kwenye dimbwi la
umaskini, maradhi na kuboresha upatikanaji wa elimu nchini. Ahadi hizo
zilitarajiwa kukamilika kabla hajatoka madarakani.
Ikiwa
imebaki takriban miezi 10 ya uongozi wa kipindi cha pili cha awamu ya
nne kufikia ukomo, muda unakwenda haraka na utekelezaji wa ahadi hizo
unasuasua jambo linalotia shaka iwapo kila ahadi itatekelezwa kwa
wakati.
Kushindwa kutekeleza ahadi hizo ambazo zimo
katika kitabu cha ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania,
Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za urais 2010, kilichondaliwa na Ofisi
ya Waziri Mkuu, kunaiweka Serikali ya CCM katika wakati mgumu hasa pale
itakaporudi kwa wananchi kutoa ahadi nyingine kwenye kampeni za uchaguzi
mkuu ujao.
Nape
Alipoulizwa
kuhusu ahadi hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema Rais Kikwete ametekeleza ahadi zaidi ya inavyoahidi ilani ya
CCM.
“Ukitaka kumtendea haki Rais Kikwete katika
utekelezaji wa ahadi zake, lazima uangalie kitabu chote cha ahadi harafu
upate ushahidi wa viongozi wawakilishi au kuzunguka kwenye maeneo
zilizokotolewa ahadi hizo,” alisema na kuongeza;
“Kwa ufupi tu, Rais huyu amefanikiwa kutekeleza ahadi nyingi ambazo ziko kwenye ilani na zile alizotoa papo kwa papo.”
Hata
hivyo Nape alimwahidi mwandishi wa gazeti hili kutoa ufafanuzi wa ahadi
zilizotekelezwa na Rais kwa kipindi chote alichokaa madarakani wiki
ijayo.
Turuka
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka alisema ofisi yake kwa
sasa iko kwenye uchambuzi na uandaaji wa kitabu kitakachoeleza
utekelezaji wake.
Turuka alisema kazi hiyo itakamilika
kwa miezi miwili kuanzia sasa.“Yapo mengi sana aliyoyafanya rais, lakini
tutaweka wazi wala siyo siri, kazi zote alizofanya zinaonekana ila kwa
sasa itakuwa vigumu kubainisha kiwango cha ahadi alizotekeleza,” alisema
Turuka.
Rais Kikwete alipokuwa wilayani Bunda, Mkoa wa
Mara aliahidi kutokomeza ugonjwa malaria ifikapo mwaka 2015, lakini
mpaka sasa ugonjwa huo umebaki kuwa tishio na ukipoteza maisha ya
Watanzania wengi kila mwaka.
Rais Mstaafu wa Chama cha
Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema jana kuwa kwa mujibu
wa malengo ya Milenia, Tanzania imepunguza vifo vitokanavyo na malaria
licha ya kuendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa.
Alisema
kwa hali ilivyo hivi sasa nchini, ambapo dawa hazipatikani kwa kiwango
kinachotakiwa ni vigumu kufanikiwa kutokomeza ugonjwa huo kwa asilimia
100 mwaka huu.
“Kama tukipata Rais mzuri ambaye ataweka
nguvu kwenye sekta ya afya, malaria inaweza kuondoka kwa asilimia 100
baada ya miaka 15,” alisema Dk Saidia.
Akiwa wilayani
Nzega mkoani Tabora, Rais Kikwete aliahidi kuwa Serikali yake ingejenga
reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini
mpaka sasa ahadi hiyo haijakamilika ingawa tayari ameshakutana na
Kampuni ya China Railway Group Limited inayotarajiwa kutekeleza mradi
huo.
Pia, akiwa Tanga Mjini, Rais Kikwete aliahidi
kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa jiji la viwanda. Ahadi hiyo mpaka sasa
haijakamilika ingawa tayari maeneo kwa ajili ya wawekezaji
yamekwishatengwa.
Akiwa wilayani Igunga mkoani Tabora,
Rais Kikwete aliahidi kuwa wananchi wa Tabora wangeanza kutumia maji
kutoka Ziwa Victoria. Ahadi hiyo mpaka sasa haijakamilika japokuwa
akijibu swali bungeni, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge alisema
mwaka 2013/14 Serikali ilitenga Sh450 milioni kwa ajili ya upembuzi
yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni.
Ahadi
nyingine za Rais Kikwete ni pamoja na kumaliza migogoro ya ardhi
nchini, wakulima kuacha kutumia jembe la mkono na kununua meli kubwa
kuliko MV Bukoba iliyozama Mei 21, 1996.
Pia, kiongozi
huyo wa nchi aliahidi kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa Tanzania (Takukuru), kwa miaka mitatu, kuanzisha benki ndogondogo
kwa ajili ya wajasiriamali na kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa
Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalumu chenye vifaa vya kupambana na
wahalifu.
Katika orodha ya ahadi hizo, pia Rais Kikwete
aliahidi kumaliza tatizo la walimu nchini. Hata hivyo, bado walimu
wameendelea kuinyooshea kidole Serikali wakilalamikia kushindwa
kuwapandisha madaraja, malimbikizo ya madeni na mishahara midogo.
Kaimu
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema
licha ya kuwa Rais Kikwete amefanya mambo mengi tangu alipoingia
madarakani, ataiacha nchi ikiwa njiapanda kielimu.
Alisema
Rais Kikwete aliahidi kutatua tatizo la kupandishwa madaraja walimu,
lakini mpaka mwisho wa mwaka huu kutakuwa na walimu 120,000 wanaostahili
kupandishwa madaraja.
Akifafanua alisema: “Mwaka jana
walimu 40,000 hawakupandishwa madaraja, mwaka huu wengine 40,000
walitakiwa kupandishwa na Julai, 2015 wengine tena watahitaji
kupandishwa madaraja.”
Oluoch alieleza kuwa Rais
Kikwete aliwaahidi walimu kuwa angewaanzishia tume yao, lakini mpaka
sasa hakuna hata muswada uliotayarishwa.
Pia, alisema
Oktoba 5, 2010 huko Songea mkoani Ruvuma, Rais Kikwete aliwaahidi walimu
kuwa angeunda Bodi ya Taaluma ya Walimu, lakini jambo hilo bado
halijatekelezwa.
“Hili tunaliona kama ni deni, Rais asiondoke Ikulu bila kutekeleza ahadi hizo,” alisema.
Aliongeza
kuwa: “Serikali ya awamu ya nne inaiacha nchi njiapanda kielimu, elimu
haikupaswa kusimamiwa na Tamisemi inatakiwa isimamiwe na Wizara ya
elimu.”
Vilevile, Rais Kikwete aliahidi kuwajengea
nyumba waathirika wa mafuriko ya Kilosa, kununua meli mpya kubwa Ziwa
Nyasa na kujenga Bandari Kasanga.
Ahadi zingine ni
kufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, kuzuia hatari ya Kisiwa cha
Pangani kuzama, kumaliza tatizo la maji katika Wilaya ya Same, kusambaza
walimu 16,000 katika shule za sekondari zenye upungufu mkubwa wa walimu
na kununua vyandarua viwili kwa kila kaya.
Rais
Kikwete aliahidi kumaliza tatizo la ukosefu wa umeme mkoani Arusha,
kukopesha wavuvi zana za kilimo, kuwapatia maji wakazi wa Wilaya ya
Longido, kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa
ya Seregenti na kusambaza maji nchi nzima.
Kuhakikisha
Jimbo la Isimani linapata maji ya uhakika, kuweka lami barabara
inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Serikali kujenga upya
Bandari ya Mbambabay.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa
NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema Rais Kikwete anaweza kutekeleza
ahadi zake kwa asilimia zaidi ya 70 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
“Lazima
tuwe wakweli huyu Rais amefanya mengi sana, yaani ukiangalia kuna ahadi
nyingi kafanya japokuwa hawezi kumaliza zote kwa muda uliobakia,”
alisema Ruhuza.
Hata hivyo, aliongeza kuwa baadhi ya
ahadi ambazo hazijatekelezwa mpaka sasa ni pamoja na ujenzi wa barabara
za Kigoma-Nyakanazi(km330),
Lulenge-Mulungarama(km100),Karagwe-Ngara(km150).
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Watendaji wakuu wa Makampuni
nchini(CEOs Roundtable-Tanzania),Ali Mufuruki alisema ahadi
alizotekeleza n8i nyingi japokuwa hataweza kumalizia zilizobakia.
“Lakini
labda nikupatie mfano, unaweza kuahidi watoto wako zawadi na
ukawanunulia wote, inatokea wengine wanakosa kwa hivyo sioni kama ni
tatizo hilo,” alisema Mufuruki.