‘Mikikimikiki ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa’
Wanachama 11 wa Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama
Dar es Salaam. Wanachama 11 wa Chama cha
Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na kesi ya kujeruhi, kuwatishia na kuwazuia maofisa wa
polisi kutekeleza majukumu yao.
Watu hao wanadaiwa
kufanya vurugu kwa nyakati tofauti wakati wa uapishwaji wa wenyeviti wa
Serikali za Mitaa katika wilaya ya Kinondoni uolifanyika Januari 6,
mwaka huu katika Hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo, Dar es Salaam,
wakipinga kuwa baadhi ya waliokuwa wakiapishwa hawakustahili.
Hali hiyo ilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Akisoma
hati ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Tumain Kweka alidai jana kuwa washtakiwa Sunday Urio (20),
Kizito Damian (35), Joseph Samky (30), Christant Luhilila (24), Karim
Ally (40), Wilfred Ngowi (30) na Kinyaiya Siriri (35) waliwatishia na
kuwazuia maofisa wa Polisi kutekeleza majukumu yao.
Kweka
alidai, Januari 6, 2015 katika eneo la Ubungo RiverSide, Wilaya ya
Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja waliwatishia na kuwazuia maofisa wa
polisi wasitekeleze majukumu yao.
Baada ya washtakiwa
hao kusomewa mashtaka hayo, waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika na wakaomba ipangwe tarehe
kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).
Hakimu
Mkazi, Devotha Kisoka aliwaambia washtakiwa hao dhamana ipo wazi na
kuwataka kila mshtakiwa kusaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh5 milioni
pamoja na kuwa na wadhamini wawili.
Katika kesi
nyingine, iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda washtakiwa
Abdul Hamis (67), Mwanaharusi Salum (42), Kizito Damian (35), Joseph
Samky(30), Sunday Urio (30), Sandro Carlos na Karim Ally wanakabiliwa na
shtaka la kumjeruhi Juma Salum na kumsababisha maumivu na majeraha.
Wakili Kweka akishirikiana na Wakili wa Serikali, Janeth Kitali walidai
kuwa Januari 6, katika Hoteli ya Landmark Wilaya ya Kinondoni
walimjeruhi Juma Salum.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao kwa
pamoja walimpiga kwa kumrushia mawe na kumsababishia majeraha Salum na
kipigo hicho kilisababisha mkono wake wa kushoto kuvunjika.
Baada
ya kusomewa shtaka linalowakabili, washtakiwa wote walikana na Hakimu
Kaluyenda aliwataka kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila
mmoja wao alitakiwa kusaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya
Sh1 milioni pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hata hivyo, Hakimu Kaluyenda aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2015 na kuwaachilia huru washtakiwa watatu.
Mhadhiri CBE kizimbani
Mhadhiri
Msaidizi wa Chuo cha Biashara (CBE) Adrew Kimbombo (52) amefikishwa
katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la kutishia kuua katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana.
Wakili
wa Serikali, Gloria Mwenda alidai mahakamani hapo kuwa Kimbombo ambaye
alikuwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kiwalani alitenda kosa hilo
Desemba 21,mwaka jana katika eneo la Kiwalani Migombani Wilaya ya Ilala
na alitishia kuua kwa maneno na hivyo kusababisha fujo.
Mwenda
alidai siku ya tukio katika eneo hilo, mshtakiwa alimtishia kumuua
Bakari Simba Mussa kwa kumwambia kuwa atampiga risasi wakati akijua kuwa
kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alikana shtaka na hakimu Juma Hassan aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, mwaka huu itakapotajwa tena.