Ngono, bangi ‘nje nje’ mgodini Ihanzutwa
Ofisa
katika Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu, Robert Nselu akionyesha sehemu ya
shehena ya mawe ya madini dhahabu yanayotolewa kama mrabaha kwa Wakala
wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA). Picha na Nuzulack Dausen.
Iringa. Wengi huisikia dhahabu, sifa zake na thamani yake.
wenye fedha zao hununua vidani vya madini hayo adimu ulimwenguni na
kujirembesha, lakini wale maskini kujikuta wakivaa vidani yaliyotiwa tu
nakshi ya madini hayo, huku asilimia kubwa vikiwa vimetengenzwa kwa
bati.
Mbali ya wenye fedha kidogo, wapo baadhi ambao
maisha yao yote hutegemea ‘kupiga roba’ watu waliovaa vidani hivyo ili
kujinakshi wao pia, lakini wengi hufanya uhalifu huu kwa lengo la
kuviuza na kujipatia fedha kwa njia hii isiyo halali.
Mlolongo
wa matukio yote hayo unatokana na kasi ya ongezeko la thamani ya
dhahabu nchini na ulimwenguni kwa ujumla katika miaka karibuni. Mahitaji
makubwa ya madini ya dhahabu yameongeza msukumo katika uzalishaji wa
dhahabu kwa ujumla wake.
Uzalishaji wa dhahabu
hufanywa katika migodi mikubwa inayomilikiwa na kampuni kubwa za
kimataifa, pia migodi midogomidogo inayoendeshwa na wachimbaji wadogo
pia hutoa mchango mkubwa na madini wanayoyachimba ndiyo ambayo hutumiwa
sana na masonara wa ndani kuzalishia vidani kama pete, hereni, bangili
na vinginevyo.
Kinachotafutwa katika machimbo madogo
huwa na thamani kubwa ya kifedha na wapo waliotajirika na kubadilika
kimaisha kutokana na mafanikio walioyapata katika uchimbaji wao. Hata
hivyo, maisha katika migodi mingi ya wachimbaji wadogo siyo ya kawaida.
Hali
ya maisha katika maeneo haya siyo kama inavyofikiriwa kwani haiakisi
uhalisia wa thamani ya madini. Mgodi wa machimbo ya dhahabu wa Ihanzutwa
ni mfano halisi wa aina ya maisha waishiyo wachimbaji wadogo katika
maeneo mengine nchini.
Kama yalivyo machimbo mengine
ya dhahabu hapa nchini ni dhahiri kwamba Ihanzutwa nayo inachangia
uchumi wa nchi, upatikanaji wa ajira na biashara ya dhahabu. Hata hivyo,
matukio ya uhalifu katika eneo la mgodi huu yanatishia maisha ya watu
na mali zao. Kwa ujumla mazingira siyo salama.
Mgodi
huu uliopo kilometa zipatazo 65 kutoka Mji wa Mafinga katika wilaya ya
Mufindi mkoani Iringa umegubikwa na matukio ya wizi, ngono zembe,
biashara ya bangi na dawa za kulevya aina ya heroine na cocain. Biashara
ya dawa za kulevya inafanywa wazi wazi pasina kificho na wahusika
hawaogopi kwani hakuna usimamizi wa sheria.
Ngono yaitwa ‘show time’
Wachimbaji
wengi hutumia fedha zao katika kununua ngono kutoka kwa wanawake
waliojaa katika machimbo hayo. Wanawake wengi, wakiwamo mabinti wadogo
wenye wastani wa umri wa miaka 17 na 18 wamejazana eneo hilo kutafuta
soko la wachimbaji hao ambao kiasi kidogo cha malipo kwa huduma ni
Sh10,000.
Asilimia kubwa ya wanawake hao wanafanya
kazi katika vilabu vya pombe na kuendesha biashara ya ngono kwa saa
maarufu kama ‘show time’ na kurudi kuendelea kuuza pombe. Wapo pia
baadhi wanaojitegemea bila ya kufanya kazi katika kilabu chochote cha
pombe.
“Hapa kuna wanawake kutoka kila mkoa na
makabila tofauti kama Morogoro, Singida, Arusha, Mbeya, Bukoba, Dodoma
na kwingineko, kati yao wote ni wachache sana kama mimi tuliolewa.
“Wengi
wapo kibiashara zaidi, hata saa hizi umekuta wamepungua kwa sababu
mgodi umeyumba kidogo. Ukitaka ngono wewe waambie tu… Watakuambia ‘nipe
changu kiasi fulani halafu twende,” anasema mfanyabiashara Tatu Sanga.
Tatu,
mama wa mtoto mmoja ameolewa na anauza duka katika Kitongoji cha
Matanda, anasema asilimia kubwa ya wanawake hao wapo kwa ajili ya kuuza
miili tu.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Ofisa Mtendaji
wa Kijiji cha Ihanzutwa, Fidelis Kidasi ambaye alisema: “Wanawake wengi
wana wachumba wa mpito wasio rasmi… Hata ukiwauliza wakati wa mgogoro
watakwambia ‘sijaja kuolewa bali kutafuta riziki na nikifanikiwa narudi
nyumbani’.
Pamoja na kwamba wanawake hao na wateja
wao, ambao ni wachimbaji wadogo hufanya ‘biashara’ ambayo ndiyo maarufu
katika eneo hili kama auuzaji madini, ‘miamala’ yao hufanywa katika
mazingira hatarishi ikiwemo kutotumia kondomu.
Wachimbaji
wengi wanasema kama wametoa kiasi kikubwa cha fedha kama zaidi ya
Sh50,000 kwa mwanamke amuuzie ngono, hakuna haja ya kutumia kondomu,
kwani fedha anayokuwa ametoa inamstahilisha kupata ‘huduma kamili’.
“Kaka
wewe mwenyewe umeona mazingira tunayotafuta mshiko, baada ya wiki ndiyo
unapata gramu moja au mbili za dhahabu ambazo ukiuza unapata kama
Sh80,000, hivi unategemea nikimhonga demu (msichana) Sh50,000 nipige na
kondomu? Sahau hiyo,” anasema mchimbaji aliyejitambulisha kama Mohammed
Hamis.
Hamis, ambaye alibainisha kuwa huchimba mashimo
yaliyopo kwenye kitalu cha Msigwa, anasema amekuwa katika mgodi huo kwa
miezi tisa sasa na kwamba ikiwa unataka kutimiza tamaa yako ya kufanya
ngono lazima ununue kwa wanawake wanaojiuza.
Bila ya kujua hatari ya biashara ya ngono kwa afya
yake, Hamis anasema kwa asili ya kazi anayofanya na mazingira aliyopo ni
vigumu kuiepuka na kwamba maisha ya mgodini ndivyo yalivyo siku zote.
Uhalisia
Kauli
ya Hamis, Tatu na Mdemu zinathibitishwa katika usiku wa Novemba 25 na
26 ambapo nilijumuika na wakazi wa mgodi huo katika vilabu mbalimbali
vya pombe vilivyopo karibu na machimbo ya dhahabu na kujionea hali hali
halisi.
Usiku wa kwanza wa kukesha eneo hilo kwa
kuzunguka takriban vilabu vyote ulisaidia kubainia namna ngono zembe
zinafanywa bila ya kuogopa hatari ya magonjwa ya zinaa, ukiwamo ugonjwa
hatari wa Ukimwi.
Pamoja na kwamba migodini hujulikana
kwa uhalifu wa kutisha, wanawake hao hawaonyeshi wasiwasi kwa mwanaume
yoyote anayewaomba kufanya nao ‘biashara’ kuwa atawadhuru.
Kama
walivyo wanaume wengi nilizungukwa na vimwana na msichana wa kwanza
kuzungumza naye kwa muda saa moja nilimjulisha baadaye kuwa nilitaka
kumuoa alinijibu “Sijaja kuolewa hapa nimeacha mme wangu huko na watoto
huko si kwa kukaa maisha na wewe, nipe changu nisepe.”
Mfumo
huo wa maisha ndiyo uliotawala katika eneo lote la mgodi, lakini mbaya
zaidi ni kitendo cha wahudumu wa baa kufanya ngono kwa muda mfupi nje
bila kuoga na kurudi kuendelea na biashara za kuuza vinywaji. Hamu ya
namna ya kujua wanavyoweza kumudu uuzaji wa miili yao kwa wanaume zaidi
ya mmoja kwa siku na kuuza bia kwa kwa wakati mmoja ilinifanya siku ya
pili kuweka kambi katika moja vilabu vilivyopo eneo linaloitwa kwa
Gwasa.
Asilimia kubwa ya vilabu hivyo vimezungukwa na
nyumba za wageni zilizotengenezwa na maturubai kwa ustadi mkubwa na mara
nyingi zinatumika kwa ajili ya kuwakodishia watu wanaotaka kufanya
mapenzi ndani ya muda mfupi maarufu mgodini hapa kama ‘show’ au ‘show
time’.
Baadhi ya wahudumu waliopo katika vilabu hivyo
vilivyoiga majina ya vilabu maarufu nchini kama San Ssiro, Bilicanas,
Kabaka Classic Pub huchepuka pale wanapopata mteja na kwenda kufanya
show time na kurudi kuendelea na biashara za kuuza vinywaji.
Nikiwa
na dereva wangu wa bodaboda na mwenyeji aliyekuwa akiniongoza katika
uchunguzi huu, tuliingia moja ya vilabu hivyo na kuweka kambi usiku
mzima.
Usiku huo, nilishuhudia baadhi ya wachimbaji
waliokuwa na vumbi miilini mwao wakiingia katika vilabu hivyo na kununua
bia kwa fujo.
Baadhi wenye mavuno makubwa ya fedha
walitishia kufunga vilabu hivyo na kuwaambia wahudumu kuwa wangenunua
bia zote hivyo wateja wengine waondoke.
Kondomu bei juu
Asilimia
kubwa ya kondomu inazogawa Serikali kwa wachimbaji hao zinaisha mapema
kutokana na mahitaji makubwa. Kidasi anasema maboksi 10 ya mipira hiyo
yanaweza yasimalize wiki.
Hali hiyo husababisha baadhi
ya maduka ya dawa kupandisha bei ya kondomu hadi zaidi ya Sh500 kwa
zile zinazouzwa Sh300 kwa pakiti ambazo zinapatikana kwa wingi eneo
hilo.
“Bei ya kondomu hapa ni kubwa sana kwa pakiti
ndogo tunauziwa Sh500 wakati mjini Sh300. Hii inafanya watu wengi waone
ni gharama ya ziada na kuachana kabisa na kutumia mipira hiyo hasa pale
wanapokuwa wamelewa,” anasema Meshack Chaula.
Hata
hivyo, Sanaga ambaye huuza kondomu hizo anasema bei ni kawaida hata
mjini na kuongeza ni hulka ya watu kuacha kutumia kondomu na siyo kwa
vigezo vya bei.
“Tutaongezaje bei? Sisi hatuna mpango
mbaya na wateja wetu. Kama kuna mtu kaamua kufanya bila kondomu kaamua
tu kwa sababu yule anayejali afya hata mipira hiyo iuzwe Sh10,000
atanunua tu,” Itaendelea kesho