Wanawake ‘wapiga jaramba’ urais 2015
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba .
Dar es Salaam. Wakati joto la kisiasa
likiendelea kupanda kila siku, makundi mbalimbali ya wanawake
yanaendesha kampeni za chinichini nchi nzima kuhakikisha kuwa
anapatikana rais mwanamke katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba
mwaka huu.
Makundi hayo yanayoongozwa na wanawake
wasomi na wanasiasa yamo katika kinyang’anyiro hicho ambacho hatima yake
ni Oktoba mwaka huu.
Kampeni zinazofanyika sasa, ni kuhakikisha jina la mwanamke linapitishwa na wanawake wote bila kujali itikadi, kumpigia kura.
Umoja
wa Wanawake Wanasiasa nchini (Ulingo), Mtandao wa Wanawake na Katiba,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wadau wengine ndiyo walio
mstari wa mbele kuhakikisha kuwa azma hiyo inafikiwa.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba
alisema kuwa walikwisha kuanza kampeni hizo tangu Septemba 2014 kupitia
mradi wa ‘Wanawake na Uchaguzi’ huku wakiwa tayari wamefika kwenye mikoa
15.
“Uzoefu wetu unaonyesha kuwa mwaka huu wa uchaguzi una nafasi kubwa kwa mwanamke ikilinganishwa na 2005/10,” alisema Bisimba.
Dk
Bisimba alitaja mikoa waliyofanikiwa kuendesha mradi huo kuwa ni
Mtwara, Mwanza, Dar es Salaam, Mara na Ruvuma. Aliongeza kuwa mwaka
2000, CCM iliwakatisha tamaa wanawake walioonyesha nia ya kuwania urais.
“Mwaka
huu ngoja tuangalie, maana kuna wanawake wengi wenye uwezo kama
tulivyoshuhudia kwenye utendaji wao, uadilifu, uzoefu na busara za
kuongoza hata taifa hili,” alisema Dk Bisimba na kuongeza:
“Kwa hivyo tunaratajia kuona vyama vikubwa vikitoa nafasi sawa kwa wanawake bila upendeleo au kuendekeza rushwa.”
Aliyekuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya
alisema atakuwa tayari kuendesha kampeni hizo kwa mwanamke yeyote
atakayejitokeza bila kujali itikadi za chama anachotokea.
Naye
Mwenyekiti wa Ulingo, Anna Abdallah alimwambia mwandishi wa gazeti hili
kuwa, umoja huo umeshajiandaa kuendesha kampeni ya pamoja na kwamba
unasubiri kupulizwa rasmi kwa kipenga cha kampeni.
Mama
Anna alisema katika uchaguzi huo, wanawake hawatakuwa tayari kuendelea
kubakia kwenye majukwaa kuwapigia kampeni wanasiasa wanaume peke yao,
badala yake wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na uwezo na utashi wa
wanawake uliopo hivi sasa.
Mama Anna Abdallah aliyewahi
kuwa kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT), alisema kwa miaka
mingi wanawake wamekuwa wakiwawezesha wanaume kuingia Ikulu, lakini
mwaka huu hali itakuwa tofauti.
“Miaka yote sisi
wanawake ndiyo tumekuwa na mchango mkubwa wa kuwaingiza madarakani,
lakini kwa mwaka huu lazima tupate nafasi ya mwanamke ambaye atasimama
kuonyesha uwezo wa kushika madaraka katika nafasi hiyo ya juu,” alisema.
Alisema:
“Kwa kutumia wingi na ushawishi wetu kama ilivyokuwa kwenye Bunge
Maalumu la Katiba (BMK) ndiyo tutakavyoendeleza kampeni hizo kwenye
uchaguzi mkuu.” Alisema na kuongeza; Ulingo itashirikiana na mtandao wa
wanawake na Katiba kufanya kampeni hiyo.
Alipoulizwa ni
majina gani mpaka sasa wameshayapendekeza, Mama Anna alisema kuwa bado
hawajafanya tathmini hiyo, lakini endapo majina yatapatikana watamuunga
mkono kwa nguvu zote mwanamke mwenye uwezo.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya alisema
bila kujali itikadi za vyama, atakuwa tayari kuunga mkono mwanamke
yeyote atayejitokeza kuwania nafasi hiyo ya urais mwaka huu.
“Ulingo
inaunganisha wanawake wa vyama karibu vyote vya siasa nchini, kwa hivyo
endapo watafanikiwa kwa umoja huo, jamii itakuwa tayari kuunga mkono
harakati hizo, kwani mwanamke ni zaidi ya uchumi katika taifa lolote
linalohitaji kupiga hatua,” alisema Sakaya.
“Pia kuna
baadhi ya taasisi na mashirika mengi tu ambayo yameshaanza harakati za
kuwainua wanawake, kuwajengea ujasiri kwa hivyo tumaini lipo kubwa,
lakini vyama ndiyo vinatakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha. CUF iko
tayari na vyama vingine vijipange kuwaunga mkono watakaojitokeza.”
Nafasi ya wanawake Tanzania
Kwa
mujibu wa sensa ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa idadi ya Watanzania ni
milioni 45, kati yao wanawake ni milioni 23 na wanamume ni milioni 21.9.
Tanzania Bara ina wanamume milioni 21.2 na wanawake milioni 22.4 na
Zanzibar ina wanamume 630,677 na wanawake 672,892.
Idadi hiyo inadaiwa kuwa ni mtaji mkubwa kwa wanawake katika harakati walizoanzisha kuelekea uchaguzi huo.
Kutokana
na nafasi hiyo, harakati hizo kupitia kwa wabunge wote wanawake kutoka
CCM, wanachama, wanaharakati na taasisi zinazounga mkono mapinduzi ya
mwanamke nchini, wamedhamiria kuleta changamoto kubwa ya kushawishi
jamii ikubaliane na harakati hizo.
Anna Senkoro alifungua pazia
Katika
uchaguzi wa urais na ubunge mnamo Desemba 4, 2005, Anna Senkoro,
(PPT-Maendeleo), alikuwa mwanamke pekee aliyeingia kwenye kinyang’anyiro
hicho.
Anna aliyeshika nafasi ya nane kati ya wagombea
10 waliokuwa wakiwania kiti hicho na kuambulia asilimia 0.17 ya kura
zote zilizopigwa.
Akizungumzia hali hiyo, Malya alisema mfumo kandamizi uliopo nchini ndiyo sababu ya wanawake kushindwa katika chaguzi.