Nyaraka za Escrow zaibwa, zazua jambo Dodoma
Dodoma. Ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya
kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya
uchotwaji wa Sh306 bilioni kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zimeibwa na kuzua mambo.
Kutokana
na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limewatia mbaroni vijana
wawili wanaotuhumiwa kusambaza mitaani ripoti ‘feki’ ya ukaguzi wa
hesabu za fedha hizo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuhusiana na kashfa hiyo.
Ripoti hiyo inadaiwa kuibwa na vijana hao katika Ofisi ya Katibu wa Bunge na kuichakachua kabla ya kuisambaza mitaani.
Vijana
hao, ambao wanadaiwa kuwa ni baadhi ya watu waliomo katika kikosi cha
waziri mmoja kilichoingia mjini Dodoma, wanadaiwa kusambaza ripoti hiyo
‘feki’ kwa kutumwa na waziri huyo.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dodoma, David Misime alithibitisha polisi kuwashikilia vijana
hao tangu juzi na kusema kuwa walipohojiwa, walikiri kupewa nyaraka hizo
na mbunge, ambaye hata hivyo alikataa kumtaja kwa sababu za
kiuchunguzi.
Pia Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah
alithibitisha kutoa taarifa polisi kuhusu vijana hao kumiliki nyaraka
zenye mihuri ya ofisi yake isivyo halali.
Kamanda
Misime alisema hadi jana walikuwa wanawashikilia vijana hao. “Jana
(juzi), tulipata taarifa kutoka kwa Katibu wa Bunge kuwa kuna watu
wanasambaza nyaraka kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge,” alisema Misime na
kuongeza: “Baada ya taarifa hiyo, tulianza msako katika mji huu wa
Dodoma na kufanikiwa kuwakamata vijana wawili.”
“Mmoja tulimkuta akiwa na nyaraka tatu, ambazo mbili zilikuwa na muhuri wa Ofisi ya Katibu wa Bunge.”
“Tulikwenda
hadi katika hoteli aliyofikia na kufanya uchunguzi na tulipombana
zaidi, alikiri kupewa na mbunge mmoja, ambaye kwa sasa jina lake
tunalihifadhi kwa sababu ya uchunguzi.”
“Hatua
tunayochukua sasa ni kuzipeleka karatasi hizi kwa mtaalamu wa maandishi
kwa uchunguzi zaidi. Swali la kujiuliza kama zilikuwa za siri, je, huyu
kijana alizipataje na kuanza kuzagaa mitaani?” alihoji Kamanda Misime.
Wakati
vijana hao wakishikiliwa na polisi, hali bado ni tete ndani ya Bunge la
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Hiyo ni utokana na kuibuka madai
kadhaa, ikiwamo kusukwa kwa mipango inayoelezwa kuwa ni ya hujuma ili
kukwamisha uwasilishaji wa ripoti sahihi ya uchunguzi wa kashfa hiyo.