‘Hatufukuzi mgombea urais CCM’
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akifungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM , mjini Unguja , Zanzibar jana. Kushoto ni Makamu wake (Zanzibar), Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein . Picha na Emmanuel Herman
Zanzibar. Wakati Kamati Kuu ya chama
tawala, CCM ikimaliza vikao vyake mjini hapa, Katibu Mkuu wa chama
hicho, Abdulrahman Kinana amesema mambo mengi yanayozungumzwa kuhusu
baadhi ya wanachama wanaotajwa kuwania urais hayana ukweli, wala hakuna
atakayefukuzwa uanachama.
Kinana aliyasema hayo jana
mjini hapa kuhusu mambo yaliyojitokeza kwa wagombea wa nafasi za urais
kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba.
Kamati Kuu ya CCM hadi jana jioni ilikuwa ikiendelea na kikao chake kwenye ofisi kuu ya chama, Kisiwandui, Zanzibar.
Kauli
ya Kinana imekuja baada ya kuwapo kwa minong’ono kuwa baadhi ya makada
waliojitokeza kutangaza ama kuonyesha nia kuutaka urais watachukuliwa
hatua, zikiwamo kutimuliwa.
“Mambo yanayozungumzwa ni
mengi kuwa baadhi ya wagombea majina yao yatakatwa. Hayo ni majungu ya
kisiasa, yamelenga kuwachokoza viongozi na chama ili wapate cha kusema.
“Chama kina utaratibu na uamuzi unaofanyika kwa vikao maalumu, hizi ni propaganda, ni uchokozi kwa chama chetu,” alisema Kinana.
Wakati
Kinana akijaribu kuwaondoa hofu vigogo wanaowania nafasi hiyo, tayari
wagombea hao wamepiga kambi mjini hapa, baadhi yao wakiendesha kampeni
za chini chini, tangu kumalizika kwa sherehe za Mapinduzi visiwani hapa
juzi.
Wagombea hao wamekuwa wakipishana kuingia
visiwani na kukutana na baadhi ya wajumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM na
mkutano mkuu kila upande ukijiimarisha kisiasa kabla ya mchakato wa
kumpata mgombea wa urais kupitia chama hicho Mei mwaka huu.
Vikumbo mitaani
Katika
hoteli kadhaa mjini hapa baadhi ya makada wamekuwa wakipigana vikumbo
ikiwa ni hatua ya kuweka mikakati ya kutengeneza mazingira, hasa ya
kukubalika katika chama hicho.
Hata hivyo, tofauti na
vikao vingine vya chama hicho tawala, idadi ya wapambe wa makundi
yanayotajwa kuwania urais waliofika mjini hapa imekuwa ni ndogo.
Uchunguzi
katika baadhi ya hoteli juzi na jana umezishuhudia zikiwa na nafasi,
viongozi waliofika kwa ajili ya sherehe za Mapinduzi wakitengewa nafasi
kwenye Hoteli ya Serena.
Habari kutoka ndani ya chama
hicho, zinasema kuwa makada hao walianza kuwasili mjini hapa siku moja
kabla ya sherehe za Mapinduzi na kikubwa kwa baadhi yao, kilikuwa
kutafuta kuungwa mkono na wenzao wa Zanzibar.
“Wengine
waliondoka jana (juzi) baada ya sherehe. Waliobaki bado wapo katika
hoteli wakijaribu kuwasiliana na watu wanaofikiri watawasaidia katika
safari yao,” alisema mmoja wa wanachama wa chama hicho.
Mmoja
wa wapambe wa mmoja wa makada wanaowania urais, alisikika akizungumza
kwa simu katika moja ya mgahawa mjini hapa juzi usiku baada ya kutakiwa
na mmoja wa wagombea kutoka Kanda ya Ziwa wakutane.
“Mheshimiwa (akimtaja), uko wapi?, haya nakuja sasa hivi.” alisema na kisha kwenda katika hoteli aliyofikia mgombea huyo.
Makada
kadhaa wanatajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Uhusiano na Uratibu)
Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, mawaziri wakuu wa
zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye.
Wengine ni
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala, Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Tibaijuka akosekana CC
Aliyekuwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anne Tibaijuka
ni mmoja kati ya wajumbe wawili walioshindwa kuhudhuria kikao cha Kamati
Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Kisiwandui.
Mjumbe mwingine ambaye hakuhudhuria ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Akizungumza
jana kabla ya kuanza kikao hicho kilichoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM
Taifa, Rais Jakaya Kikwete, Kinana alisema wajumbe hao waliomba udhuru.
Hata
hivyo, Prof Tibaijuka ni mmoja wa wana CCM waliotajwa kupewa mgawo wa
fedha wa Sh1.6 bilioni katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Waziri
huyo alivuliwa wadhifa wake na Rais Jakaya Kikwete mwisho wa mwezi
uliopita ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge waliyoyatoa
mwezi Novemba baada ya kujadili ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC) kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Waziri
mwingine ambaye Bunge lilipendekeza avuliwe madaraka, Profesa Sospeter
Muhongo wa Nishati na Madini bado anaendelea na wadhifa wake.
Miongoni
mwa ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa kwenye kikao hicho cha siku moja
ni pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwezi uliopita ,
hali ya kisiasa nchini na hatima ya wanachama wanaodaiwa kugawiwa fedha
hizo.
Utulivu
Tofauti
na vikao vingine ambavyo hufanyika Dodoma, mji wa Unguja ulionekana
kuwa tulivu bila pitapita za wana CCM waliovalia sare za chama, hata
katika maeneo yaliyo karibu na ofisi hiyo, Kisiwandui.
Mapambo
yaliyokuwa yakionekana mtaani na katika ofisi za CCM yenye rangi ya
kijani na njano, yaliwekwa kama sehemu ya shamrashamra za sherehe za
Mapinduzi. Pia, wajumbe wa kikao hicho wengi wao waliokuwa wamevalia
sare za chama chao, walionekana wakiingia moja kwa moja katika jengo
hilo kuanzia saa 3.00 asubuhi baada ya kusalimiana na wenyeji wao.
Pia,
magari na misafara ya viongozi ilifanya maeneo hayo kuwa na ukimya
mwingi kama vile hakuna kitu kilichokuwa kinachoendelea kwenye ofisi
hizo.
Nje ya ukumbi kulikofanyika kikao, askari polisi
na usalama wa Taifa walijipanga kwa mstari karibu na mlango na magari
yalikuwa yakiwashusha viongozi mbalimbali.
Hadi saa 11.30 jioni jana, wajumbe walikuwa hawajatoka kwa ajili ya chakula cha mchana au kupumzika.
Hata
hvyo, wajumbe wa kamati hiyo walimaliza kikao chao baadaye usiku na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa suala kubwa
lililozungumzwa ni kashfa ya Escrow, hali ya kisiasa nchini na maadili.
“Nitazungumza zaidi kesho (leo) kwa kirefu, kwa kifupi tumezungumzia hayo kwa leo,” alisema Nape akiondoka Kisiwandui.
Chanzo
cha habari kutoka ndani ya kikao hicho, kilipasha kuwa Mwenyekiti wa
CCM, Rais Jakaya Kikwete, kimsingi amekubali kufanya uamuzi kuhusiana na
masuala mbalimbali ikiwemo la Escrow kabla ya kuanza kwa kikao cha
Bunge mjini Dodoma Januari 27.
Kikao hicho cha CC ni
cha kwanza kufanyika mwaka huu ambao Tanzania itachagua rais, wabunge na
madiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba. Tayari
makada kadhaa wametajwa kuwania nafasi hiyo ambapo mwaka jana chama
hicho kiliwaadhibu baadhi yao kwa madai ya kufanya kampeni kabla ya
wakati.