Gari la DC wa Mbozi lazua tafrani jimboni kwa Kilango
Mbunge
wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela akizozana na dereva wa mkuu
wa wilaya ya Mbozi (aliyekataa kutaja jina lake) baada ya kukuta gari la
mkuu huyo wa wilaya likipeperusha bendera katika jimbo la Same
Mashariki jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.Picha na Rehema Matowo
Same. Katika hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa
Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Dk Michael Kadege limekutwa likipeperusha
bendera katika eneo la Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na kuzua
tafrani kati ya mkuu huyo na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango
Malecela.
Gari hilo likiwa na Bendera ya Taifa,
lilionekana saa nne asubuhi likiwa limeegeshwa katika eneo la Mamba
Myamba katika Jimbo la Same Mashariki huku Dk Kadege akiwa kwenye
mgahawa.
Kitendo cha gari hilo kuonekana likipeperusha
bendera kilimfanya Kilango kulifuata akidhani ni la Mkuu wa Wilaya ya
Same, ndipo akakuta ni la Mbozi.
“Hili gari siyo la
Same na kawaida mkuu wa wilaya nyingine haruhusiwi kupeperusha bendera
kwenye eneo ambalo siyo lake, huyu amekuja kwenye mambo yake ya siasa,
anapeperusha bendera ili wananchi wamwone kuwa yuko juu na hii ni hujuma
kwenye jimbo langu,” alilalamika Kilango.
Alisema Dk
Kadege ni miongoni mwa watu wanaotaka kugombea ubunge Jimbo la Same
Mashariki lakini ni vyema akasubiri muda ukifika ajitokeze hadharani
badala ya kujenga mpasuko kwa CCM katika jimbo hilo.
“Huyu
amekuja kwa ajili ya vikao vya ndani, mwaka 2005 tuligombea wote kwenye
kura za maoni nikamshinda nikiwa na kura 389 yeye 46 akawa mtu wa nne,
mwaka 2010 mimi nilipata kura 7,900 na yeye alipata 2,200 sasa ameanza,
sikatai lakini asubiri muda wake,” alisema Kilango.
Kwa
upande wake, Dk Kadege alisema hakuwa na taarifa kuwa gari lake
linapeperusha bendera kwa kuwa yeye hahusiki kuweka bendera, akataka
dereva wake aeleze sababu za kupeperusha bendera kwenye eneo
lisiloruhusiwa.
Dk Kadege alisema yeye yuko likizo na alikwenda nyumbani
kwao Same kupumzika na hafanyi shughuli zozote za kisiasa katika jimbo
hilo kama inavyodaiwa na Kilango.
Dereva wa mkuu huyo
wa wilaya ambaye alikataa kutaja jina lake, alipohojiwa sababu za
kupeperusha bendera katika eneo lisiloruhusiwa alisema alikuwa akifanya
usafi wa gari na alipohojiwa zaidi alidai siyo msemaji wa mkuu wa
wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi alisema
kutokana na sheria, utaratibu na miongozo ya wakuu wa wilaya, kiongozi
huyo wa wilaya haruhusiwi kupeperusha bendera katika eneo ambalo siyo
lake.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa
namba 19 ya Mwaka 1997 na Sheria ya Serikali za Mitaa namba Saba na Nane
ya mwaka 1982, mkuu wa wilaya ni msimamizi wa shughuli za kimaendeleo
na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya yake tu.
Kapufi
alisema atawasiliana na Dk Kadege kama anafahamu utaratibu na miongozo
waliyopewa wakati wa kuanza kazi ili ajue kama alikusudia kufanya hivyo
au kama alipitiwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Same,
Agust Kessy alipoulizwa kuhusu hali hiyo alisema mipaka ya wakuu wa
wilaya inatambulika ni jambo la kushangaza kama mkuu huyo alikuwa ndani
ya gari na asiione bendera ikipepea.
Alisema CCM
imeweka utaratibu na kanuni zinazotakiwa kufuatwa na kila mwanachama na
kuwataka wenye lengo la kugombea wasubiri muda ufike ili kuepusha
mgongano na mtafaruku ndani ya chama. “Tuache kutegeana, tusubiri
filimbi ipigwe,” alisema Kessy.