Kitabu cha ‘urais’ wa Makamba
Dar es Salaam. Ni dhahiri mpambano wa
kuwania urais ndani ya CCM unazidi kunoga, ikiwa imebakia miezi michache
kabla ya kupulizwa rasmi kipenga.
Mmoja wa makada
kutoka CCM waliotangaza nia ya kuwania kiti hicho, January Makamba
ameandikiwa kitabu kinachoeleza nia yake hiyo.
Kitabu
hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza mikakati ya mwanasiasa huyo
kijana iwapo atapitishwa na chama chake ili kuwania na hatimaye kushika
nafasi hiyo ya juu ya uongozi kitaifa.
Katika kitabu
hicho chenye kurasa 196, Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mbunge wa Bumbuli, Tanga anasema
rais ajaye lazima awe na tafakuri pana na nia ya kuendeleza nchi na siyo
kuwa na kaulimbiu nyepesi za afya bure, elimu bure zisizo na ufafanuzi
ili kuwahadaa wananchi.
Kitabu hicho kilichoandikwa na
mchambuzi na mwandishi wa makala za siasa, Padri Privatus Karugendo
kimebeba sera na mikakati yake kiundani ya kuiongoza nchi iwapo
atapatiwa dhamana na CCM kugombea urais.
Katika kitabu
hicho kinachoitwa, ‘Maswali na Majibu 40: Mazungumzo na January Makamba
kuhusu Tanzania Mpya’, mwanasiasa huyo anasema uongozi hauishii kwa
kauli za juu juu za kuongeza ajira, kuboresha elimu kwani kila mtu
anaweza kuyasema hayo.
Anamwonaje rais ajaye
Anasema
katika tafakuri zake anaona rais ajaye anatakiwa kuzitambua kwa kina
changamoto za nchi yake na kuwa na mikakati ya kuzitatua.
Changamoto
hizo, Makamba anasema ni za kiuongozi na utatuzi wake unategemea
kiongozi mwenyewe, hulka, mtazamo wake na usahihi wa uamuzi anaoufanya.
“Kuomba
uongozi wa nchi siyo harakati binafsi na wafuasi wako kupata vyeo. Ni
dhamana kubwa ya kujenga mustakabali wa nchi na kuwaunganisha Watanzania
wote. Kwa hiyo, uamuzi wa kugombea lazima uupe heshima na nafasi
inayolingana na dhamana yenyewe,” anasema Makamba kwenye kitabu hicho.
Anaongeza
kuwa rais anatakiwa kuongeza kasi ya kuondoa umaskini, kuongeza imani
ya wananchi kwa Serikali, vyombo vya dola na mahakama na hayo
yatadhihirika kwa vitendo vya kuchukua hatua dhidi ya viongozi
wabadhirifu, walarushwa na kudhibiti matumizi ya Serikali.
Pia,
Makamba anatumia fursa hiyo kuelezea mikakati yake kuhusu kutatua
matatizo ya elimu, kusimamia muungano, umoja, mshikamano na upendo,
kukuza ujasiriamali, umilikaji wa ardhi na unufaikaji wa rasilimali kwa
wananchi na jinsi alivyo tayari kuboresha hali hiyo.
Hoja ya ujana
Mwanasiasa
huyo aliyeingia kwa mtazamo wa uongozi wa kizazi kipya, anapoulizwa na
mwandishi wa kitabu kuhusu mjadala kuhusu umri na urais na kwa nini
vijana waaminiwe kwa nafasi hiyo wakati hawana uzoefu, anajibu kuwa
haamini kuwa umri pekee ni sifa ya uongozi.
“Siamini
kwenye dhana kwamba ukiwa mzee unafaa na ukiwa kijana hufai, au ukiwa
mzee hufai na ukiwa kijana unafaa. Ujana si sifa na uzee si kashfa.
Ujana si kashfa na uzee si sifa,” anasema.
Anabainisha
kuwa wanapokubaliana umri si kigezo, maana yake ni kwamba mwenye miaka
40 asionekane hawezi kutokana na miaka yake, lakini anaongeza kuwa
uongozi ni suala la rika. Anasema kila rika au kizazi kina wakati wake,
wajibu wake na ndiyo maana Mwalimu Julius Nyerere aliamua kung’atuka
urais akiwa na miaka 62 na siyo kwa kushindwa kuongoza, bali kwa ajili
ya kuachia rika na kizazi kingine kiendeleze alipoishia.
“Uongozi
ni kutengeneza kesho njema. Wenye kesho nyingi hawapaswi kukaa pembeni
na kukunja mikono na kuwaachia wenye jana nyingi kazi ya kujenga kesho
njema. “Wakifanya hivyo, uhakika wa kesho njema unaweza usiwe mkubwa kwa
sababu wenye jana nyingi wanaweza kuhangaika na masaibu ya jana zao
kuliko matumaini ya kesho,” anasema.
Uzoefu wa JK
Makamba
aliyewahi kuwa mwandishi wa hotuba wa Rais Jakaya Kikwete, anasema
ushiriki wake katika kampeni za urais mwaka 2005, akiwa msaidizi wake na
baadaye kufanya naye kazi Ikulu, ulimpatia uzoefu mkubwa uliosadia
kuyajua matatizo yanayowakabili Watanzania karibu kila eneo la nchi.
“Nilijifunza
pia kwamba matumaini wanayowekeza Watanzania kwa viongozi wao ni
makubwa na pale tunapowaangusha kwa kweli tunatenda makosa.
“Nilijifunza
kwa Kikwete kwamba unaweza kuomba kura, kuelezea dira yako, fikra zako,
sera na ilani ya chama chako bila kutumia matusi, kejeli, ulaghai na
lugha kali na bado ukafanikiwa,” anasema Makamba katika kitabu hicho.
Anaongeza
kuwa alipokuwa msaidizi wa JK wa kuandika hotuba, alijifunza namna
Serikali inavyoendeshwa kwa kuhimili msisukosuko wakati wa vipindi
vigumu na jinsi kiongozi wa juu anavyotakiwa kutotetereka.
Kwa mujibu wa Padri Karugendo, kitabu hicho ni sehemu ya
mradi walioubuni wa kutaka kuwafahamu vijana, hasa wale waliochomoza
kwenye medani za siasa na kushika nafasi za juu za uongozi serikalini
wakiwa na umri mdogo na kiu ya kuleta mabadiliko katika nchi.
Anasema
Karugendo kuwa wataendelea kuuliza maswali kwa kila kijana kutokana na
umri wake na kwamba iwapo anayo miaka 40, basi ataulizwa maswali 40,
vivyo hivyo kwa yule mwenye miaka 55 au zaidi.
Katika
maswali hayo ya kichokozi, Makamba aliulizwa na Padri Karugendo kuwa
haoni kuwa CCM imepoteza mwelekeo na inapata upinzani mkubwa na iwapo
kuna sababu ya kuendelea kuaminiwa na Watanzania?
Katika
majibu yake, Makamba anasema ni kweli ushindani umeongezeka na kwamba
hali hiyo si ya ajabu kwa kuwa ndani ya miaka 22 ya mfumo wa vyama vingi
ni lazima ushidani ungetokea, ila anapinga kuwa CCM imepoteza mwelekeo.
Anasema
zipo changamoto kadhaa zilizo kawaida kwa kila taasisi ambazo
zitatatuliwa kwa kuwasemea na kuwatetea wanyonge, kukemea rushwa na
maovu katika chama chenyewe na kutekeleza ilani na ahadi za CCM.
“Ni kweli kwamba chama kimeingiliwa na wajanja wachache ambao wanataka kununua uongozi kwa ajili ya kujinufaisha.”
Makamba,
katika kitabu hicho ambacho dibaji yake imeandikwa na Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi au Mzee Ruksa, anasema haoni mbadala wa
CCM kwa sasa katika utayari wa uongozi wa Taifa na kwamba amani,
utulivu, umoja na maendeleo na salama ya nchi ipo mikononi mwa CCM.
Akielezea
namna ya kupunguza makali ya umaskini kwa kukuza uchumi na ajira kwa
vijana, Makamba anasema kuna haja ya kuweka muswada maalumu wa matumizi
kwa uwezeshaji kiuchumi kwa vijana, utakaokuwa sheria maalumu ya
matumizi ya Sh3.6 trilioni kwa ajili ya miaka mitatu.
Anasema
sheria hiyo itasaidia kupanua ajira kwa kuchochea shughuli za
uzalishaji mali na uchumi, zikiwamo kutoa motisha kwa biashara kubwa na
viwanda vitakavyoongeza ajira rasmi 50 za kudumu kwa mwaka, pia
kupunguza kodi ya mshahara (PAYE).
Dibaji ya Mwinyi
Katika
dibaji kwenye kitabu hicho, Mzee Mwinyi anasema Makamba anaonekana
dhahiri ameandaliwa au amejiandaa vilivyo kuwa kiongozi mkubwa wa nchi.
Mzee
Mwinyi anasema kitabu hicho kimemfanya amfahamu zaidi kiongozi huyo
kuliko awali alipokuwa kama kiongozi ndani ya chama na Serikali.
“Fursa ya kusoma mazungumzo yake imenisaidia kumfahamu zaidi kama mtu, pia fikra zake,” anasema Mzee Mwinyi.
Anaeleza
kufarijika kwake kuona nchi na Rais Kikwete wameendeleza utamaduni
aliouanzisha Mwalimu Nyerere na kuendelezwa naye wa kuwaamini vijana na
kuwapatia fursa za uongozi ili kuwaanda kuongoza nchi.
Kauli ya Makamba
Akizungumzia
kitabu hicho, Makamba alisema jana kuwa kilichoandikwa na Padri
Karugendo kinaakisi mawazo yake na kwamba amewasilisha vyema mazungumzo
yao.
“Amefanya kazi nzuri na imechukua muda mrefu kama
mwaka mzima hivi. Kuna kipindi nilikata tamaa kwamba kitabu hakipo,
lakini hatimaye amekikamilisha,” alisema Makamba na kuongeza:
“Watu wanaotaka kunifahamu wakisoma kitabu hicho watanielewa January ni nani.”
Anahimiza wanasiasa wengine wafanye hivyo ili wananchi wawajue viongozi wao ili iweze kusaidia nchi kupata kiongozi bora.
“Wananchi wengi wanawajua viongozi wao kwa vyeo walivyoshika, lakini hawawajui kwa undani,”anasema.
Anapoulizwa
kwamba haoni vipaumbele vilivyomo kwenye kitabu hicho vinapingana na
zuio la CCM kwa wanachama wake kufanya kampeni za urais mapema, Makamba
anajibu kuwa hivyo ni vipaumbele vya Tanzania mpya na havihusiani na
kampeni.
“Siyo kampeni za mapema kwani ni fikra zangu
katika kuboresha nchi na jamii yetu. Haiendani kinyume na taratibu za
CCM, ambazo tumewekewa kwani haya ni mawazo yangu na ndiyo
ninayoyaamini,” alisema Makamba.
Anasema ameyaweka mawazo yake kwenye mfumo wa pamoja, hivyo mtu yeyote atakayesema hiyo ni kampeni atakuwa anafanya siasa.