ACT sasa kwachafuka, waanza kufukuzana
Mwenyekiti wa ACT,Kadawi Limbu
Dar es Salaam. Chama cha ACT-Tanzania
kimewasimamisha viongozi wa chama hicho ambao ni Mwenyekiti wa muda
Kadawi Limbu na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Leopold Mahona na kikimvua
madaraka Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Grayson Nyakarungu.
Hatua
hiyo imejitokeza baada ya maazimio ya Halmashauri Kuu iliyokutana
kujadili agenda za nidhamu ya mwenyekiti, kupokea na kupitisha mwongozo
na kanuni za uchaguzi pamoja ushiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Katibu
mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alisema jana kuwa maazimio ya
mkutano huo yaliwachagua Shaaban Mambo kuwa mwenyekiti wa muda, Mohamed
Masaga, Naibu katibu mkuu na Hassan Abdalah Omary kuwa mwenyekiti mpya
wa vijana.
“Mkutano wa jana (juzi) ulikuwa na wajumbe
65, lakini kura 57 zilipendekeza Limbu na Mahona wasimamishwe katika
nafasi zao kwa muda,” alisema Mwigamba na kuongeza kuwa: “Kwa mujibu wa
katiba ya chama, Kifungu cha 27(f) kinasema halmashauri ina mamlaka ya
kuwasimamisha kwa kipindi cha miezi sita, baada ya hapo watakuwa na haki
ya kugombea tena nafasi zao pindi uchaguzi utakapoitishwa.”
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo kama wameshawapatia na kuwajulisha wahusika, Mwigamba alisema tayari taratibu zote zilishafanyika.
“Kwanza
tuliwapa nakala ya mashtaka pia tukawaita kwenye mkutano ili kuwapatia
nafasi ya kujitetea. Limbu alikataa kujieleza,” alisema Mwigamba.
Hata
hivyo, chama hicho kwa siku za hivi karibuni kimekuwa katika mvutano
kati ya Limbu na viongozi wenzake, hasa katibu mkuu, akidaiwa kuhujumiwa
na vyama vikubwa vya siasa.
Akizungumzia uamuzi huo,
Limbu alisema siyo sahihi kwani mkutano huo hauna mamlaka ya kumwondoa
kwenye nafasi yake bali ni kamati kuu tu ndiyo ina uwezo huo.
“Sheria
ya vyama vya siasa ndiyo inatoa mamlaka. Wajumbe waliokaa hatuna
uhakika kama wamefikia akidi ya 65 kama tulivyoelezwa,” alisema Limbu.