Ngeleja,Chenge wapelekwa Maadili
Mjumbe
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za mitaa (LAAC) za Mitaa,
Kangi Lugola akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika
Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mjumbe mwenzake, Omari Nundu. Picha na
Anthony Siame
Dar es Salaam. Licha ya Bunge kuazimia kuwa
wenyeviti wa kamati zake waliotajwa kuhusika kwenye kashfa ya Akaunti
ya Tegeta Escrow wavuliwe nyadhifa zao, hali imekuwa tofauti katika
vikao vya kamati hizo vilivyoanza jana baada ya baadhi yao kuongoza
vikao hivyo. Jana, Kamati Kuu ya CCM imeamua viongozi hao, Andrew
Chenge, William Ngeleja Na Profesa Anna Tibaijuka wafikishwe Kamati ya
Maadili ya chama.
Awali, walitakiwa kuachia ngazi na
kamati zao katika mabano ni Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), Chenge
(Bajeti) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Kikao
cha 16 na 17 cha Bunge kiliazimia kuwa kamati husika za kudumu za Bunge
zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa
Bunge unaoanza Januari 27, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa
kamati husika.
Hata hivyo, jana, Ngeleja alisema anaendelea na madaraka yake, kwa kuwa hatua iliyopo sasa ni ya uchunguzi.
“Mimi
naendelea na kazi zangu kama mwenyekiti wa kamati, najua uchunguzi wa
suala hili bado unaendelea, baada ya hapo ikithibitika ndipo Bunge
litachukua uamuzi nami sitakuwa na budi kutekeleza,” alisema Ngeleja.
Aliongeza: “Ingawa ninajua kuna shinikizo kwa baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao hawapendi kutuona katika nafasi hizi.”
Kwa
upande wake, Chenge alisema: “Sikuwahi kutangaza kujiondoa katika
nafasi hii ya uenyekiti. Nimeshangaa taarifa zilizotolewa katika baadhi
ya vyombo vya habari.”
Alisema tuhuma zinazomkabili
hazimuumizi kichwa kwa sababu hazina ukweli, “Dhamira hainiumi kwa
sababu siwezi kushiriki kuiba fedha za wananchi. Mimi ni kama tumbili
hata hapa nitaruka.”
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo,
Dk Festus Limbu alisema suala la Chenge linasubiri uamuzi utakaotolewa
na Spika wa Bunge, Anne Makinda. “Kamati imeamua kwa busara Chenge akae
pembeni na makamu mwenyekiti aongoze vikao huku ikisubiri hatua
atakazozichukua Spika (Makinda)...lakini siyo taarifa kwamba Chenge
kajiuzulu, siyo kweli.”
“Unajua suala hili unaweza
kusema bado ni bichi, Chenge ni mwenyekiti mteule wa Spika, lakini
wenyeviti wengine wanachaguliwa na wajumbe wa kamati zao, labda Spika
hajaona wa kumteua au anataka kuiachia kamati ifanye uchaguzi, hili
litategemea na yeye,” alisema Limbu ambaye ni Mbunge wa Magu (CCM)
Kuhusu
wafadhili wa maendeleo ambao kamati hiyo ilikutana nao jana alisema
wametoa asilimia 50 ya Dola 558 milioni ambazo wahisani hao waliahidi.
Kikao
cha Kamati ya Nishati na Madini kiliongozwa na Makamu mwenyekiti wake,
Jerome Bwanausi ambaye alilithibitishia gazeti hili kwamba hawakufanya
uchaguzi wowote.
Alipotafutwa kwa simu Mwabalaswa na kutakiwa kuzungumzia hatima yake, alijibu kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwenye simu.
Mkurugenzi
wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Suala halipo
kikanuni, bali ni maagizo yaliyotolewa na Bunge kwa hiyo mwenye nafasi
nzuri ya kulizungumzia ni Spika.”
Hata hivyo, habari
zilizopatikana jana usiku ndani ya Kamati Kuu ya CCM zilieleza kuwa,
Ngeleja, Chenge pamoja na Profesa Tibaijuka suala lao imeachiwa Kamati
ya Maadili ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Philip Mangula.
LAAC yalishukia jiji
Katika
hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
imeitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo itoe taarifa za
kueleweka kuhusu uuzaji wa hisa zake na mikataba kwa Kampuni ya Simon
Group. Uamuzi huo umekuja baada ya Mkurugenzi wa jiji hilo, Wilson Kabwe
na Meya, Dk Didas Masaburi kujichanganya wakati wakijibu maswali ya
uuzaji wa hisa hizo kwa kampuni hiyo ambayo inamiliki Shirika la Usafiri
Dar es Salaam (UDA).
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk
Mohammed alitoa maazimio hayo baada ya kuibuka mvutano kati ya wajumbe
wa kamati hiyo na Dk Masaburi na Kabwe kuhusu uuzwaji wa hisa hizo
ambazo ni asilimia 21.
Mvutano uliibuka baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi
Lugola kueleza kuwa mmiliki wa Simons Group, Robert Kisena alitaka
kununua hisa hizo, lakini jiji lilikataa.
Kwa upande
wake, Kabwe alikiri kuwa walikataa zisinunuliwe kwa sababu alikuwa na
shaka kama Simon Group ingeweza kulipa fedha zote kama unavyoeleza
mkataba. Hisa hizo zinauzwa kwa Sh5 bilioni.
Kitendo
cha wajumbe wa kamati hiyo kulichachamalia zaidi suala hilo ambalo
liliwagawa katika Bunge la Bajeti kinatafsiriwa kuwa ni kutaka kulipa
kisasi baada ya Dk Masaburi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu UDA, Mei
mwaka jana katika kikao cha Bajeti, kutumia lugha ya kuudhi kwa wabunge.
Pia,
kamati ilihoji kwa nini Jiji la Dar es Salaam lisivunjwe na kuwa na
kitengo kidogo kutokana na kutokuwa na majukumu ya moja kwa moja kwa
wananchi.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Msalala
(CCM), Ezekiel Maige kwamba kuna haja ya kuvunjwa kwa jiji hilo na
badala yake kubakiwe watu wachache (meya, mkurugenzi na katibu muhtasi)
ambao watashungulika na masuala mtambuka.
Alisema pia
kuna haja ya kuangalia upya, sheria ambayo inaipa mamlaka halmashauri ya
jiji kukusanya ushuru wa maegesho ili kazi hiyo ifanywe na manispaa za
jiji hilo na kisha kutoa gawiwo kwa jiji.
Katika ziara
ya LAAC iliyofanya katika manispaa za jiji hilo hivi karibuni, ilipokea
malalamiko ya kutopewa fedha za maegesho kutoka jiji, jambo
linalozikwamisha kufanya shughuli za maendeleo. Manispaa zote tatu,
Ilala, Kinondoni na Temeke zinatakiwa kugawana asilimia 75 ya mapato ya
maegesho na asilimia 25 inabaki jiji.
Akijibu hoja ya
ushuru, Dk Masaburi alisema madai hayo huenda yakawa na ukweli na kuwa
tatizo lililopo ni mkataba uliokuwa umeingiwa na wakala, Nation Park
Solution (NPS).
Awali, Mbarouk aliupa uongozi wa jiji
siku 19 kuanzia leo kuhakikisha inapeleka ripoti ya tathmini ya mali kwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutokana na
kushindwa kuikamilisha kwa miaka mitatu tangu kutolewa kwa agizo hilo.
PAC yataka uchunguzi NBC
Nayo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru kuteua mkaguzi binafsi kwa ajili ya
kufanya uchunguzi wa sababu za kushuka kwa mtaji wa Benki ya NBC ambayo
inadaiwa Sh22.5 bilioni na Kampuni ya Absa Group Limited ya Afrika
Kusini.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alitaja maeneo
yaliyosababisha mtaji kushuka kuwa ni mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya
usafirishaji, utekelezaji wa sera za Benki mama ya ABCA na mfumo wa
uhasibu uliotambua mapato hewa. Iwapo Serikali itashindwa kulipa deni
hilo hadi Machi mwaka huu, itapoteza asilimia 30 ya hisa zake katika NBC
na hivyo benki hiyo kuwa chini ya Kampuni ya Absa ambayo ina asilimia
55 ya hisa za NBC.
Awali, kampuni hiyo ilikuwa na hisa
asilimia 70 za benki hiyo lakini ikauza asilimia 15 ya hisa zake kwa
Shirika la Fedha la Kimataifa.
Serikali ilikopa kiasi
hicho cha fedha ili kutekeleza agizo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
ambayo mwaka 2012 iliiagiza NBC kuongeza mtaji wa biashara wenye thamani
ya Sh75 bilioni, baada ya ule wa awali kushuka kwa asilimia 12.
Baada
ya NBC kubinafsishwa mwaka 1997, Serikali ilibaki na asilimia 30 ya
hisa na Kampuni ya Absa kuchukua asilimia 70, mtaji wa NBC ulishuka kati
ya mwaka 2010 hadi 2012 baada ya benki hiyo kutoa mikopo ya magari wa
Sh55 bilioni.
Baada ya mtaji wa NBC kushuka kwa
asilimia 12, Benki Kuu Tanzania (BoT), iliagiza wanahisa wote watatu
kuongeza mtaji. Kwa kuwa Serikali haikuwa na fedha za kuongeza katika
mtaji, ilikopa Sh22.5 bilioni kwa Absa na kuzitoa kama mtaji kwa
makubaliano ya kurejesha deni hilo ndani ya miaka miwili. Kuhusu taasisi
ya mikopo ya Pride, Msajili wa Hazina alisema baada ya ukaguzi wa CAG
walibaini kuwa taasisi hiyo iliondolewa kimakosa katika orodha ya
taasisi za umma.
Alisema kutokana na hali hiyo kuna
hasara ambayo serikali imeipata na kusisitiza kuwa watapokea taarifa
rasmi ya uchunguzi wa taasisi hiyo uliofanywa na CAG na wataiwasilisha
katika vikao vya Bunge vinavyoanza Januari 27.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Beatrice Moses.