Escrow yalamba vichwa saba TRA
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (kulia), akimjulia hali aliyejifungua watoto pacha katika Hospitali ya Mwananyamala, Mwamvita Kilasi wakati waziri huyo alipokwenda hospitalini hapo kutoa misaada mbalimbali katika wodi ya watoto. Waziri huyo alikuwa akisheherekea siku yake ya kuzaliwa. Picha na Venance Nestory.
Dar es Salaam. Sakata la ufisadi wa Sh306
bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow limewang’oa wafanyakazi saba wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wafanyakazi hao
wamesimamishwa kazi ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa maazimio
manane ya Bunge kuhusu ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), kuhusu kashfa hiyo.
Wengine ambao tayari
wameshawajibika katika kashfa hiyo ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyefukuzwa kazi na Rais
Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi aliyesimamishwa kupisha uchunguzi.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema pia
Serikali imetoa siku 30 kwa walionufaika na mgawo wa mamilioni ya fedha
kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering Ltd, James
Rugemalira kulipa kodi kulingana na kiasi walichopokea.
Hatua TRA
Akizungumzia
hatua zilizochukuliwa kwa wafanyakazi wa TRA waliohusika na sakata hilo
Nchemba alisema; “Mpaka sasa wafanyakazi saba wamesimamishwa kazi ili
kupisha vyombo vinavyohusika viweze kuchukua hatua zaidi na mimi
nilikuwa nasema wachukue hatua zaidi kwa kuwa haiwezekani badala ya Dola
milioni 20 mtu anaweka fedha za Tanzania Sh20 milioni, hii ni makusudi
au njama za kutekeleza wizi huo.
“Ukisema ulikuwa
unajua ni njama, hivyo hustahili kuwapo na ukisema ulikuwa hujui pia
hustahili kuwapo. Huwezi kusomeshwa kwa kodi ya Watanzania halafu
unapopewa fursa ya kusimamia makusanyo ya kodi ukafanya unavyojua,”
alisema Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM).
“Mtu
hawezi kuiba Sh30 bilioni halafu ukamfukuza kazi pekee, hii utakuwa
unampa likizo ya kwenda kutumia fedha hiyo, ifike mahali mtu anapoiba
anafilisiwa mali zake ili kuwa fundisho kwa wengine.”
Nchemba
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) alisema kitendo cha
mtumishi wa umma kufanya vibaya na kisha kuhamishiwa sehemu nyingine
haitakiwi kuwapo kwa kuwa hiyo ilikuwa inatokea wakati watumishi wakiwa
wachache.
“Unajua zamani unakuta wahandisi ni wachache
unapomfukuza moja kwa moja unakosa wa kukaa nafasi hiyo lakini sasa
watumishi na wataalamu ni wengi mtu akikosea ni kumwondoa akatafute kazi
sehemu nyingine kwani hatutakiwi kufumbia macho vitendo hivi,” alisema
Nchemba.
Waliopata mgawo
Kuhusu
walionufaika na mgawo huo, Nchemba alisema “TRA imeshawatumia fomu za
mahesabu ya kodi wanazotakiwa kulipa na wao sasa wakae na wahasibu wao
waseme wanatakiwa kulipa kiasi gani ndani ya siku 30 kuanzia Januari
Mosi mwaka huu.
Baadhi walionufaika na mgawo huo na
kiwango walichopokea katika mabano ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni),
Profesa Tibaijuka (Sh1.6 bilioni), Mbunge wa Sengerema (CCM), William
Ngeleja (Sh40.4 milioni), aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini,
Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul
Kimiti (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos
Bukuku (Sh161.7 milioni).
Majaji walioingiziwa fedha ni Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji A.K Mujulizi (Sh40.4 milioni).
Siku ya kuzaliwa
Aidha,
jana ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa, Nchemba alifanya kazi mbalimbali
za kujitolea na akisema: “Sasa nimetimiza miaka 40 ya utumishi, zamani
nilikuwa natimiza miaka ya utegemezi lakini hii ni ya utumishi.”
Alipoulizwa
kama kauli hiyo ina uhusiano na mchakato wa kuwania urais alisema:
“Sasa nina kazi moja ya kumsaidia waziri wangu (Saada Mkuya) na Rais
Jakaya Kikwete. Licha ya kuwa naibu waziri bado ni naibu katibu mkuu
ambaye natakiwa kusimamia kanuni, miongozo na maadili ya chama changu
lakini muda utakapofika kama ni mto tutavuka pamoja,” alisema Nchemba.
Katika
kuadhimisha siku hiyo, Nchemba alitoa misaada kwa wajawazito katika
Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Chakuwama
Sinza na kuchangia damu katika Kituo cha Mpango wa Taifa wa Damu
Salama.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala,
Dk Sophinias Ngonyani alimweleza Nchemba changamoto wanazokutana nazo
ikiwamo upungufu wa wodi na vitanda ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa
wanaopokewa.