Jaji Mkuu mstaafu ‘apanda kizimbani’
Jaji
Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya
Hai, Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kupanda kizimbani na kutoa ushahidi
mahakamani hapo katika kesi ya jaribio la kutapeli viongozi wa Chadema.
Kushoto ni shahidi namba mbili wa kesi hiyo, Profesa Abdalah Safari.
Picha na Dionis Nyato
AD
Moshi. Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta jana alipanda
kizimbani kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Hai tukio
lililovuta hisia za wananchi wengi kwani ni la kwanza na la aina yake
kwa kiongozi wa juu wa mhimili huo wa dola.
Jaji
Samatta aliingia eneo la Mahakama saa 2.40 asubuhi akifuatana na Profesa
Abdallah Safari na baadaye kwenda moja kwa moja chumba cha mapumziko
kabla ya kuingia mahakamani.
Baada ya kula kiapo kutoka
kwa karani wa Mahakama hiyo, Baltazar Buretta, Jaji Samatta alianza
kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Adam Abeid (25) ya kujifanya
jaji huyo na kutaka kuwatapeli viongozi wa Chadema, akisema alishtuka
alipoelezwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa kuna mtu
ambaye amempigia simu akijitambusha kuwa ni Jaji Samatta.
Abeid pia anakabiliwa na shtaka kutaka kumtapeli Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Kesi
hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Denis
Mpelembwa ilisikilizwa chemba huku Jaji Samatta akiongozwa kutoa
ushahidi wake na Mwanasheria wa Takukuru, Susan Kimario anayesaidiana na
Furahini Kibanga akikana kumfahamu wala kuwa na uhusiano na mshtakiwa
huyo.
Jaji Samatta ambaye sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe na mjumbe wa Bodi ya Kuchuja Mahakimu na Majaji Kenya, alisema
kati ya Aprili na Mei 2012, Dk Slaa alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi
(sms) akiambatanisha na ujumbe unaodaiwa kutumwa na mshtakiwa, akimtaka
athibitishe kama ndiye aliyeutuma kwake.
Ujumbe huo
ulisomeka: “Hali yako Dk Slaa, kesho nataka nikamuone Jaji Mkuu Chande,
naomba nichangie nauli (ili) nikashughulikie yale masuala yetu.”
Jaji
Samatta alisema alishtuka na kuamua kumpigia simu Dk Slaa na kumweleza
kuwa ujumbe huo haukuwa umetoka kwake na kumtaka alifikishe suala hilo
kwenye vyombo vya dola.
“Nilimpigia pia Wakili Profesa
Safari (Abdallah) nikamuomba ahakikishe suala hilo haliishi kisiasa,
bali upelelezi ufanyike kwa sababu hadhi yangu na heshima yangu ilikuwa
at stake (shakani),” alisema.
Maswali kati ya mshtakiwa na Jaji Samatta yalikuwa kama ifuatavyo;
Mshtakiwa: Je, katika zile meseji alizokutumia Dk Slaa unazo kwenye simu yako?
Jaji Samatta: Zile meseji ziko katika simu yangu ya zamani ambayo niliacha kuitumia baada ya kuzeeka.
Mshtakiwa: Wakati Dk Slaa anakupa taarifa hizo, nani alikuwa wa kwanza kulifikisha suala hilo Takukuru?
Jaji
Samatta: Sijui kwa sababu niliwaambia Dk Slaa na Profesa Safari
walipeleke hilo suala kwenye vyombo vya dola na mimi ningeitwa kuandika
maelezo.
Profesa Safari ambaye ni shahidi wa pili,
aliiambia Mahakama kuwa kati ya Aprili na Mei, 2012, alipokea simu
kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni Jaji Samatta akiomba simu ya
Lema.
“Aliniambia anataka azungumze na Lema ili
kumsaidia kwenye kesi yake ya Arusha (ya kupinga ubunge wake). Nilimpa
na nikampigia pia Lema kuwa kuna mtu anamtafuta,” alisema.
Profesa
Safari alisema hata hivyo, alishuku kuwa mtu huyo hakuwa Jaji Samatta
kutokana na kwamba alikuwa akiifahamu sauti yake na ni mtu ambaye
wamefanya naye kazi kwa muda mrefu.
Baadaye Profesa
Safari alisema aliamua kumjulisha Dk Slaa kuhusiana na jambo hilo kwa
vile lilikuwa linaonekana kuwa na sura ya utapeli na rushwa na Chadema
hakijihusishi na mambo hayo.
Katika kesi hiyo, upande
wa mashtaka unadai kuwa mshtakiwa alijifanya ni Jaji Samatta akitaka
kumsaidia Lema katika rufaa yake namba 47/2012 ya kupinga hukumu
iliyokuwa imemvua ubunge wa Arusha Mjini.
Pia, upande
wa mashtaka unadai pia katika kipindi hicho, mshtakiwa huyo ambaye
alikana mashtaka hayo, alijifanya kuwa ni mkuu wa Takukuru Wilaya ya
Ulanga mkoani Morogoro, Abel Kibaso.Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Januari
14.