Washtakiwa wa Ugaidi wapangiwa hakimu mwingine
Dar es Salaam. Kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu sasa kusikilizwa na Hakimu Mkazi Janeth
Kaluyenda.
Awali kesi hiyo ambayo itatajwa Januari
13,2015 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la
ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi, Hellen Liwa ambaye hata hivyo
alijitoa.
Ni baada ya wakili wa washtakiwa hao wa
ugaidi, Abubakar Salim kumtaka ajitoe kuisikiliza kesi hiyo ili iweze
kupangiwa hakimu mwingine ambaye atatoa uamuzi juu ya hoja zao
walizozitoa mahakamani hapo Septemba 19,2014.
Washtakiwa
wanaokabiliwa na kesi hiyo ya ugaidi ni Sheikh Farid Hadi Ahmed
ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbuyuni Zanzibar, Fundi Ujenzi
mkazi wa Koani Zanzibar, Noorid Swalehe na Jamal Nooridin Swalehe
(38).
Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally na Juma Juma.
Saidi
Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali
Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma,
Kassim Nassoro na Said Sharifu kwa pamoja wanadaiwa kuwa walijihusisha
na makosa hayo ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha sheria ya
kuzuia ugaidi ya 2002.
Wanadai kuwa kati ya mwezi
Januari 2013 na Juni 2014 walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya
kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Katika
kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, Sheikh Farid na Sheikh Mselem
Mselem wanadaiwa kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili
kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Sheikh Farid
anadaiwa kuwa kwa makusudi na akijua alitoa msaada kwa watu hao wa
kutenda vitendo vya kigaidi kinyume cha sheria na kuwahifadhi.