Christian Bella atenga Sh68 milioni kujilipua kimataifa
Dar es Salaam. Jaribu kufikiria mwimbaji wa
nyimbo maarufu kama Safari Siyo Kifo, Yako Wapi Mapenzi, Nani Kama
Mama, Usilie na nyinginezo anapoamua kutengeneza video na watayarishaji
wakubwa Afrika nini kitatokea?
Hiki ndicho alichopanga
kukifanya mwimbaji wa muziki wa dansi ambaye mara nyingi hupenda
kusimama kama ‘solo artist’, Christian Bella kwa ajili ya kukuza soko la
muziki wa dansi Tanzania, akifuata nyayo za wasanii wa Bongo Fleva.
Bella
amesema kuwa kuanzia Februari mwaka huu, atatengeneza video kubwa
itakayoongozwa na mtayarishaji God Father nchini Afrika Kusini.
“Kwa
nafasi niliyonayo sasa, nikiendelea na video za ‘kitoto’ nitafeli,
natoa wimbo mmoja matata nitakaoanza nao mwaka, mwanzoni mwa Februari
utakuwa tayari.
Namwomba Mungu mipango yangu iende kama
nilivyopanga, ikiwamo kufanya video kubwajapokuwa zina gharama kubwa na
mimi sitaangalia suala hilo, nataka mafanikio, hivyo lazima nijilipue
ili kujitangaza kimataifa,” alisema Bella.
Bella
alisema kwa sasa ameshatenga kiasi kikubwa cha fedha ili akamilishe
mpango huo, kwani anaamini akitayarisha video kubwa, itakuwa rahisi kazi
zake kuonyeshwa katika televisheni kubwa Afrika kama MTV Base, Channel
O, Trace na kwingineko.
“Najua gharama yake inaweza
kufika kiasi cha Sh68 milioni. God Father ndiye mtayarishaji nayemlenga
kwa sasa, gharama hiyo ni video tu pasipo kuangalia mambo mengine,
ikiwamo usafiri, mavazi na vitu vingine muhimu,” alisema.
Alisema uamuzi huo umetokana uchunguzi alioufanya pamoja na ushauri kutoka kwa watu kadhaa, wakiwamo wadau wa muziki.
“Mwaka
huu sifanyi kawaida kama miaka iliyopita, kwa sababu tunakoelekea
lazima tuangalie mwelekeo wa dunia, nini kinahitajika ili kufikia
malengo ya kufanya vizuri.
“Ndoto yangu ni kutengeneza pesa, lakini hilo linawezekana kama nitafanya jitihada,” alisema Bella na kuongeza:
“Kwa mfano, leo wamemtambua Diamond Platnumz katika Channel O, Trace, BET kwa sababu ya video kubwa.
Haimaanishi
kwamba Diamond anafanya muziki mzuri kuliko wasanii wote Tanzania
hapana, lakini tunampongeza na kumuunga mkono na kumpa hongera kwa
kuthubutu vitu vikubwa kama hivi, mtu anayeanza na anayefanya vizuri
lazima umpongeze na wewe upite palepale.”
Alipoulizwa
kuhusu umahiri wake katika tungo mbalimbali za mashairi na sauti yake
yenye kuvuta hisia za mashabiki wa muziki wa dansi, Christian Bella
alisema huchukua miezi kadhaa kutunga mashairi ya wimbo mmoja.
“Sikurupuki,
inachukua muda mrefu, linaweza kuja wazo la mrindimo kwanza likakaa
kichwani, baadaye nikarekodi kidogo kwenye simu nauacha naanza kutafuta
meneno kidogo kidogo siyo kwa haraka.”
Alisema kuna
nyimbo zingine za haraka ambazo, huingia studio siku hiyohiyo
akatengeneza wimbo mara nyingi huwa ‘kolabo’ na siyo nyimbo zake.
“Nyimbo zangu zinachukua muda, natulia na wazo, nafikiria nini cha kufanya, sina haraka kufikia kutoa uamuzi,” anasema.
“Wakati
mwingine nakaa na mtu na kuanza kumuuliza hivi hapa nifanye nini ili
wimbo uwe bora nikiimba...Hivi naeleweka, nachunguza na kufanya utafiti
kabla ya kuwalisha mashabiki.”
Ingawa hutumia miezi
kukamilisha wimbo mmoja, Bella alisema anaweza kuimba mwanzo hadi mwisho
katika mtindo wa moja kwa moja ‘freestyle’.
“Naweza
kuimba ‘freestyle’, lakini linapokuja suala la kurekodi, lazima
niifikirie kwanza inapendeza, inafaa kwa jamii, mfano wimbo Nakuhitaji
niliouanza kama Rhumba, lakini kuandaa mdundo unaitwa mutwashi ndiyo
ambao unasikika katika kibao changu hicho.”