Dk Slaa kupanda ‘kizimbani’ leo
Moshi. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibroad Slaa, leo anatarajiwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya
Wilaya ya Hai kutoa ushahidi katika kesi ya jinai inayomkabili kijana
aliyejifanya Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Dennis Mpelembwa alisema jana kuwa Dk Slaa amethibitisha kuitikia wito huo wa Mahakama.
Katika
ushahidi uliotolewa mahakamani, Dk Slaa akiwa Mtendaji Mkuu wa Chadema,
ndiye anayedaiwa kushughulikia suala la mshtakiwa kutaka kuwatapeli
viongozi wa Chadema.
Tayari Jaji Samatta na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema wamekwishatoa ushahidi wao katika kesi hiyo
inayoendeshwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
Katika ushahidi wake, Jaji Samatta alikana
kumfahamu mshtakiwa Abeid Adam Abeid (22) na kwamba namba ya simu
iliyotumiwa kujitambulisha kwa Dk Slaa na Lema kuwa ni Jaji Samatta siyo
yake.
Kwa upande wake, Lema alidai mshtakiwa huyo
alimtumia meseji mbalimbali akijitambulisha kwake kuwa ni Jaji Samatta
na kwamba angemsaidia katika rufaa yake ya kuvuliwa ubunge ya mwaka
2012.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa
Takukuru, Susan Kimaro ulidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya
Aprili na Mei 2012. Mtuhumiwa alikana mashtaka hayo na leo upande wa
mashtaka unatarajiwa kufunga ushahidi wao baada ya Dk Slaa na shahidi
mwingine ambaye hajatajwa, kutoa ushahidi wao.