Kikwete: Tumedhamiria kusambaratisha uasi DRC
Alitoa
kauli hiyo jana alipokutana na Mjumbe Maalumu wa Rais wa Afrika Kusini
na Waziri wa nchi hiyo, Mapisa-Nqakula, Ikulu mjini
Zanzibar.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesisitiza kuwa Tanzania
inayo nia ya dhati ya kukabiliana na vikundi vya uasi vinavyo vuruga
amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Rais
Kikwete amesema kuna watu wanaojidai kuwa na uwezo wa kusoma na kuelewa
maoni na mtazamo wa Tanzania kuliko hata Tanzania yenyewe.
Alitoa
kauli hiyo jana alipokutana na Mjumbe Maalumu wa Rais wa Afrika Kusini
na Waziri wa nchi hiyo, Mapisa-Nqakula, Ikulu mjini Zanzibar.
“Wanadai
eti Tanzania haina nia ya kukabiliana na vikundi vya uasi. Ni watu wa
ajabu kabisa hawa kwa sababu Tanzania kama zilivyo, Afrika Kusini na
Malawi, zina askari wake DRC chini ya Umoja wa Mataifa,” alisema Rais
Kikwete.
Alisema askari wa Tanzania walianza kazi kwa
kukisambaratisha kikundi cha M-23 na wako tayari kukabiliana na kikundi
cha uasi cha FDLR. Alisisitiza kuwa Tanzania iko tayari kwa sababu bado
majeshi yake yapo DRC na masharti ya Umoja wa Mataifa ya kushiriki
katika Brigedia ya Kimataifa hayajabadilika na wala Serikali ya Tanzania
haijatoa maelekezo tofauti kwa majeshi yake mbali na yale yaliyotolewa
mwanzoni mwa operesheni hiyo na UN.
Mwishoni mwa wiki
iliyopita, wakati akiwatakia heri ya Mwaka Mpya mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao nchini katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es
Salaam, Rais Kikwete alizungumzia shutuma zinazotolewa dhidi ya
Tanzania kuhusiana na DRC kuwa ni za kupuuzwa.
Wakati
Rais Kikwete akizungumza hayo, Jarida la News of Rwanda, juzi lilidai
kuwa Tanzania haiwezi kuwashambulia waasi wa FDLR wanaofanya
mashambulizi yao Mashariki mwa DRC.
Jarida hilo
liliandikwa kuwa uthibitisho wa kauli yao unatokana na kupishana kwa
kauli kati ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Tanzania, Bernard Membe na Rais
Kikwete.
“Viongozi hao wanatoa ujumbe tofauti kuelezea
namna Tanzania inavyolishughulikia kundi la FDLR,” linasema jarida.
Lilisema kauli hizo zinakinzana na kutoa picha kuwa Tanzania haina nia
ya kuisaidia DRC.
“Rais anasema watakishambulia, Waziri anasema hawana nia, nani wa kuaminiwa,” limenukuliwa jarida hilo.
ti
huohuo, Rais Kikwete jana aliendesha Kikao cha Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwenye ofisi ya CCM, Kisiwandui
mjini Zanzibar.