Matukio ya mauaji na ukatwaji viungo vya watu wenye Albinisim yameanza tena kushika kasi.
Katika
kukabilina na matukio ya mauaji na ukatwaji viungo vya watu wenye
Albinisim ambayo yameanza tena kushika kasi mwishoni mwa mwaka jana
serikali imepiga marufuku wapiga ramli ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi
kazi kwa ajili ya operesheni maalum ya kuwasaka watuhumiwa.
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh Mathias Chikawe ameyasema hayo
jijini Dar es Salaam ambapo amekiri kuongezeka kwa matukio hayo tangu
mwishoni mwa mwaka jana na kuongeza kuwa timu hiyo itaundwa na watu sita
wawili kutoka chama cha Albinisim Tanzania na wanne jeshi la polisi na
wataanza na mikoa mitano ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Geita
na baadae Sumbawanga, Kagera na Mbeya.
Akijibu maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari likiwemo la
malalamiko ya ucheleweshwaji wa kesi pamoja na watuhumiwa kuachiwa bila
kufikishwa mahakamani Mh Chikawe amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kudai
kuwa linatokana na msongamano wa kesi zilizopo mahakamani na kuongeza
kuwa kwa sasa wameanza mkakati ya kuzipa kipaumbele kesi ambazo
zinaigusa jamii moja kwa moja.
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye Albinisim nchini Bw Ernest
Kimaya amesema katika kukabiliana na tatizo la ucheleweshwaji wa kesi
pamoja na watu wanaoachiwa huru kwa kisingizio cha kukosa ushahidi wa
kutosha chama hicho kinatafuta udhamini kutoka mataifa ya nje ili wapate
fedha za kuendesha kesi kwani hadi sasa kesi zilizofanyiwa kazi ni tano
tu kati ya kumi na moja.