Askofu Shoo: Viporo escrow vinaumiza tumbo
Askofu
Mkuu wa Kanisa la kiinjili la kiluther Tanzania (KKKT), Dk Alex
Malasusa (kushoto) akimsimika Mchungaji Dk Fedrick Shoo kuwa Askofu mpya
wa KKKT Dayosisi ya kaskazini katika ibada iliyofanyika jana katika
usharika wa Moshi mjini. Picha na Dionis Nyato
Moshi. Askofu mpya wa Dayosisi ya Kaskazini
ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo
jana alitoa ujumbe mzito kwa Rais Jakaya Kikwete alipomtaka
kuwawajibisha haraka wahusika kwenye kashfa ya escrow kwa kuwa “viporo
vinaumiza tumbo”.
Dk Shoo aliyemrithi askofu Dk Martin
Shao aliyestaafu, alitoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utawala Bora), George Mkuchika ambaye alimwakilisha Rais, wakati
akihutubia kwenye ibada ya kuwekwa kwake wakfu na kusimikwa kwa msaidizi
wake, Mchungaji Elingaya Saria iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini.
Mbali
na Waziri Mkuchika, wengine waliokuwapo kwenye ibada hiyo ni mawaziri
wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, pamoja na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu. Pia walikuwapo baadhi ya wabunge
na maaskofu wa dayosisi 24.
Katika hotuba yake, Dk Shoo
alisema kanisa linasikitishwa na ufisadi mkubwa unaoendelea miongoni
mwa viongozi na watumishi wa umma na kiburi wanachokionyesha
wanapoelezwa ukweli.
“Kinachotusikitisha zaidi ni
wahusika kuonyesha jeuri kubwa na ukakamavu wa hali ya juu pale
wanapoambiwa,” alisema Dk Shoo huku akishangiliwa.
“Mimi sioni mantiki kama mtu amehusika katika mambo fulani, halafu anaanza kusema sikueleweka vizuri halafu anajiuzulu.”
Ingawa
hakumtaja kwa jina kiongozi huyo, Jaji Fredrick Werema alijiuzulu
nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu kwa kumwandikia barua Rais akieleza kuwa
ushauri wake katika suala la escrow haukueleweka na umesababisha
tafrani.
Katika sakata hilo la Escrow, Jaji Werema
ndiye anayedaiwa kuandika barua akieleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow zilipwe IPTL bila ya kukatwa kodi.
“Tunatambua
Rais ameanza kuchukua hatua dhidi ya watu kama hawa. Tunazidi kumwombea
yeye na Serikali yetu ili wamwonyeshe hatua zaidi zinazofaa
kuchukuliwa,” alisema Askofu Shoo.
“Panapohitajika
kuchukua hatua, tusiweke viporo. Unajua viporo vikishakuwa vya muda
mrefu, vinaumizaa tumbo,” alisisitiza Dk Shoo huku umati uliofurika
ukilipuka kwa furaha na makofi.
Akitangaza uamuzi wake
kuhusu maazimio ya Bunge la Muungano, Rais Kikwete alitangaza kumwondoa
kazini Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, lakini akasema amemweka kiporo Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wanasiasa kujipitisha
Askofu Shoo pia hakuwasitiri wanasiasa wanaopita makanisani na misikitini kutafuta umaarufu ili uwanufaishe kupata madaraka.
“Sisi
tunapenda kuwaasa wasaka madaraka kama hao, wanaokimbilia kusaka
umaarufu rahisi, tunawatambua na tutawatambua kwa rangi zao,” alisema
askofu huyo.
“Ningependa ijulikane kwa wanasiasa na
waumini wote kwamba nyumba za ibada ni mahali patakatifu. Si mahali pa
kufanyia usanii. Sina maana kila mwanasiasa ni msanii.
“Kanisani
ni mahali panapotakiwa kukaribiwa kwa hofu na kwa uchaji. Siyo uwanja
wa siasa. Tumpe Mungu yaliyo ya Mungu na ya Kaisari yaliyo ya Kaisari
lakini pasipo kuharamisha unabii.”
Kuhusu Panya Road
Katika
hatua nyingine, Askofu Shoo alisema kuibuka kwa kundi la wahalifu
maarufu kama Panya Road jijini Dar es Salaam ni matokeo ya vijana wengi
nchini kukosa ajira.
“Ajira kwa vijana ni changamoto
kubwa kutokana na kufungwa kwa viwanda vingi vilivyokuwapo, matokeo yake
wengi wanaokaa bila ajira, wamejiingiza katika ajira zisizofaa,”
alisema.
Dk Shoo alisema kama hali ya vijana wengi
kukosa ajira itaendelea kama ilivyo sasa, itakuwa ni hatari kubwa kwa
usalama wa nchi na kuonya kuwa watu waliokata tamaa ni vigumu
kuwatawala.
“Watu watakata tamaa na watu waliokata
tamaa hawatawaliki. Tukiendelea hivi tusishangae hao wanaoitwa Panya
Road wakajitokeza hata hapa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,” alisema.
Askofu
Shoo alisema Tanzania si masikini na kwamba nchi imejaliwa utajiri
mwingi na kusisitiza kuwa wanaosema Tanzania ni maskini na kuamini
hivyo, ni maskini wa fikra.
“Tunachohitaji ni viongozi
na watumishi wenye roho ya uzalendo. Bila hivyo ni vigumu kuhakikisha
kuwa rasilimali za nchi hii zinawanufaisha Watanzania wote,” alisema.
Mkuchika ajibu
Akijibu
hotuba hiyo iliyoonekana kuwa mwiba mkali kwa Serikali, Mkuchika
alisema Serikali imekwishachukua hatua na itaendelea kuchukua hatua
dhidi ya watu wote waliohusika na sakata la escrow.
“Tayari
wahusika wamechukuliwa hatua. Mfano Mwanasheria Mkuu wa Serikali
amejiuzulu na Waziri mmoja ameondolewa katika Baraza la Mawaziri,”
alisema Mkuchika katika hotuba yake.
Mkuchika alisema
hata Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi na kwamba uchunguzi dhidi ya
watu wengine waliotajwa bado unaendelea.
“Kwa wale
wengine ambao uamuzi bado haujafikiwa, vyombo vya dola, kama (Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa) Takukuru na Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, vinavifanyia kazi,” alisema.
Mkuchika
alimpongeza Askofu Shoo kwa kutambua tatizo la wanasiasa kutumia
makanisa na misikiti kunadi sera zao, lakini akawashauri viongozi wa
dini kutowakaribisha wanasiasa hao ili kukomesha hali hiyo.
“Endapo
viongozi wa dini watakataa, tatizo hili halitakuwepo. Msiwakaribishe
kutumia maeneo ya kanisa na misikiti kuhubiri siasa. Tusichanganye dini
na masuala ya siasa,” alisisitiza Mkuchika.
Dk Malasusa atoa angalizo
Mkuu
wa Kanisa la KKKT, Dk Alex Malasusa alisema mwaka 2015, nchi ina mambo
mengi, lakini ni vyema Serikali ikaweka kipaumbele katika mambo muhimu
zaidi, likiwamo Daftari la Wapigakura.
“Serikali
iboreshe Daftari la Wapigakura ili wananchi wengi waweze kujiandikisha
na kupiga kura. Mnasema tuendeleze amani lakini amani haiwezi kuwepo
kama haki haipo,” alisema.
Askofu Malasusa pia
alitahadharisha kuibuka kwa vikundi vya uhalifu kama Panya Road na
kudokeza kuwa Moshi kumeibuka kundi la Kanyaga Twende.
Dk
Malasusa alimwambia Mkuchika kuwa suala la utawala bora si la Rais,
bali ni la kwake na kumtaka asimamie utawala wa sheria vinginevyo,
mwisho wa kuibuka vikundi hivyo utakuwa mbaya.