Nnauye ashushia tuhuma Ukawa kuwa chanzo cha vurugu


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM , Nape Nnauye, ameutuhumu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwa ndicho chanzo cha vurugu zinazotokea wakati wa  kuapishwa viongozi wa serikali za mitaa.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wanahabari,  akiihusisha Ukawa na vurugu hizo zilizoripotiwa katika mikoa mbalimbali.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakiyachukua makundi ya watu kwa ajili ya kuvunja sheria.

Nnauye alisema CCM inalaani vikali vurugu zilizofanywa ba wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF)  kwa viongozi wa serikali za mitaa wa maeneo kadhaa ikiwamo  Mwanza, Dar es Salaam, Kilimanjaro  na Mbeya.

“Vurugu hizo zilisababisha baadhi ya viongozi wetu kujeruhiliwa katika mkoa wa Mwanza ambapo walivamiwa na kupigwa wakati wanaapishwa,” alisema Nnauye

Jijini Dar es Salaam, Sulta  Jeta wa mtaa wa Ukwamani katika jimbo la Kawe alifanyiwa fujo na wafuasi hao na katika Mtaa wa Msisiri A kata ya Mwananyamala katika Jimbo la Kinondoni Juma Mbena alipigwa na kuvunjwa mkono.

Alisema mkoani Mbeya katika wilaya ya Kyela na Rungwe zoezi la kuapishwa viongozi  wa serikali za mitaa lilishindikana na kuahirishwa kutokana na vurugu za kurushiwa mawe zilizofanywa na wafuasi wa Chadema.

Aliziita kuwa  mwendelezo wa tabia  na mazoea ya vyama vya upinzani kutokuheshimu na kufuata sheria na taratibu za nchi.

Aidha, Nnauye alisema katika suala hilo hapakuwa na haja ya kufanya vurugu kwani walitakiwa kufuata sheria hata kama mtu akiapishwa inawezekana kuvuliwa baada ya taratibu kufuatwa.

Wakati huo huo, Nnauye alisema leo sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM itakutana kuandaa ajenda za mkutano wa kamati kuu ya chama hicho utakaofanyika Jumanne ijayo visiwani Zanzibar chini ya Mwenyekiti  Rais Jakaya Kikwete.



CHANZO: NIPASHE

Powered by Blogger.