SIMULIZI YA KUJIFUNZA


STORY YA KUSISIMUA SANA NI NDEFU LAKINI  CHUKUA MUDA WAKO KUISOMA ITAKUSAIDIA NA ISIPOKUSAIDIA WEWE BASI ITAKUWA MSAADA KWA JIRANI YAKO.*
Ilikuwa ni mwaka 1979, nikiwa nasafiri kutoka Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12:30 jioni. Wakati huo mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, siyo kama siku hizi. 
Nilikuwa nakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo, sikurizishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili. 
Tulifika mji unaoitwa Korogwe, ambao wakati ule ulikuwa ndiyo mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika Korogwe, basi lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba, ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo. 
Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba, sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo.
  “Abiria wengine wahuni bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu.” Mwenye hoteli alisema kwa kudhamilia hasa.
Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hotel akisema ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha polisi ili nishughulikiwe. Hapo hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na mtoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile, alimtuma mhudumu mmoja aniiite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kwenda kwa yule bwana. 
Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Niliwasalimia na waliniitikia. Yule mtu aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili kama nilikuwa nimeibiwa fedha zote, na ningerudi vipi Dar es salaam. Nilimwambia nilikuwa napanga kuangalia namna ya kurudi Dar es salaam, kama huko polisi ningeaminika.
Kama mzaha, bwana yule aliniambia angenipa fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar es salaam, nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90(Kwa wakati huo ilikuwa niyngi sana) kwa ahadi kwamba nikirudi Dar es salaam, nimpelekee pesa zake ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkurumah na kuniambia kwamba, ameamua kunisaidia kwa sababu, kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko. 
Nilishukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukuwa muda kabla basi letu halijapata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe. Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu. 
Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti mbili. 
Nilijua ni maiti kwa sababu, walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana, kakiwa kamefugwa kanga kichwani.
“Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitalini, ameumia, ingawa siyo sana”. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. Kalikuwa kameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka, wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka. 
Baada ya kutoa msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale, tulipanda basini kuanza safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Landrover ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili. 
Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili, niliponunua gazeti ndipo nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni Yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la Kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana kama mtoto. 
Nilishindwa kujua ni kwa nini ilikuwa afe. Nilijiuliza ni nani sasa ambaye angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu nap engine ya kijinga pia. Nilijua kwamba, nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki mbili za sasa. Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu Yule aliniamini na kuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu. 
Nilikata kipande kile cha gazeti la kiingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukua kipande hicho na kukiweka kwenye diary yangu. Deni, ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nkipiga magoti na kuomba. Niliomba Mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema. “Kwa njia yoyote Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa kwa sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu.” Niliomba. Nilirejea Dar es salaam siku hiyohiyo. 
Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule kuwa mabaya kwangu, nilijikuta nimekuwa na mambo mengi na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia. Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya kwenda kusoma Chuo cha Saruji na baadaye chuo cha Ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda Uingereza. Mwaka 1991, nilianza shughuli zangu. 
Ilikuwa ni mwaka 1995, nikiwa ofisini kwangu pale jengo la Nasaco, Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa na seketari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa anatalkka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa kijana mdogo wa miaka 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende, yaani hovyohovyo huku afya yake ikiwa hairidhishi sana. 
Nilimkaribisha ili mradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba, sikuwa mtu mwenye huruma sana na nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza, “nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao baada ya muda mfupi.” Nilisema na sikuwa na kikao chochote, lakini nilitaka tu aondoke haraka. 
“Samahani mzee, nilikuwa na shida. Nina..nimefukuzwa shule na sina tena mtu wa kunisaidia kwa sababu…Nime…nko kidato cha pili na hivyo natafuta tu kama atatokea mtu…” 
Nilimkatisha, “sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule, si nitarudi kwetu kwa mguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie…Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe…Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezio, wanataka sifa?” 
“Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shuleni. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa hivi sasa hata kazi hafanyi…” Alianza kulia. 
Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi ni kwa nini nisiwe mwema, angalau kwa mara moja tu. “Baba na mama wamekufa lini?” Niliuliza nikijua kwamba watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo kila anayekufa alihesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi. 
“Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndiyo shangazi yangu alinichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa.” Yule kijana alilia zaidi. Naomba niwaambie wasomaji kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba, ziko nguvu nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua. 
Kitu Fulani kilinipiga akilini paa! Nilijikuta namuuliza yule kijana. “Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?” Yule kijana alisema “nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, ndiyo nimejikuta nikiingia hapa, sijui…sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa,” alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso. 
Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani, halafu niliona kama vile nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa anaitwa nani?” “Alikuwa anaitwa Siame…Cosmas Siame…” Niliinuka ghafla hadi yule kijana alishtuka. Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye droo moja na kutoka na diary. Mikono ikitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti kutoka ndani ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi. 
“Ndiyo, alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.” Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali. “Mungu wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba, kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani.” Halafu nilinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa analofanya. 
Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilijihisi kuwa mtu mwingne kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku bado nikiwa ninalia. “Mimi ni baba yako mdogo, ndiye nitakayekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi mwisho.” Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita. 
Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la Maziwa ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyu dada yake Cosmas alifurahi hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Hata hivyo alifariki mwaka mmoja baadaye, lakini akiwa ameridhika sana. 
Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na kwenda Australia kufanya kazi. Ukweli ni kwamba, ni mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile walichokipanda miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado, ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza, ni kitu gani kilimvuta mwanaye Siame hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine zote?
UJUMBE
=>Usiwe mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu.
=>Usimdharau mtu yeyotekatika hali yoyote na kwa namna yoyote maana hujui nani ataishi na wwe.
=>Jifunze kusaidia haswa uwapo na nafasi maana wanadamu sisi ni mavumbi na mavumbini tutarudi.
=>Mali tunazozikusanya ni kwa ajiri ya matumizi so kusaidia ni moja ya matumizi
=>Toa msaada kwa mtu yeyote maana hujui kesho, kama leo yako ni nzuri basi huenda kesho yako ikawa SHUBIRI.
Powered by Blogger.