HADITHI YA KUSISIMUWA :NCHI YA WACHAWI -1

Picha za Juu mfano wa picha za bunduki za kichawi.
"Kwa jina naitwa Israeli, lakini si yule mtoa roho za watu, hili ni jina ambalo linapatikana katika utaratibu wa maisha ya kila siku duniani.

Nimezaliwa mwaka 1950, (kwa sasa 2010 ana miaka 60) wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, ni mtoto wa kwanza katika familia yenye kujiweza kidogo kimaisha, ikiwa na watoto tisa, wote wanaume. Wazazi wangu (sasa marehemu) walikuwa wacha Mungu sana.

Kama kweli kuna uhai baada ya kifo na wakayajua mambo yangu ya duniani, naamini nimewaumiza sana wazazi wangu.

Kwa sasa naishi Mbagala, jijini Dar es Salaam na familia yangu yenye mke na watoto saba, wote wa kike. Mke wangu pia kwao ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto tisa, wote wanawake.

Nimelazimika kusimulia mkasa huu wa kichawi baada ya watu wengi kusimulia mikasa yao wakidai waliwahi kuwa wachawi wakaacha kwa sababu mbalimbali ambazo wengine huzisema, wengine hufanya siri kubwa.

Naweza kusema kwamba, karibu wote waliokuwa wakisimulia maisha yao ya kichawi na mikasa yake, hakuna hata mmoja aliyewahi kufikia hata robo ya maisha ya kichawi ya kwangu.


Mimi niliishi maisha hayo kwa miaka kumi, na nilifika levo' ya mbali, mfano kuwa Mkuu wa Kikundi na kusafiri sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya mikutano mikubwa ya kimataifa ya wachawi.

Niliporudi, nilikuwa nakutana na wachawi wakubwa wa hapa nyumbani Tanzania na kuwapa maagizo ya utendaji katika makundi yao sehemu mbalimbali za nchi.


Katika kipindi chote cha kuwa mchawi nilibaini mambo makubwa mawili, kwamba, maisha ya wachawi katika ulimwengu wao hayana tofauti yoyote na maisha ya watu wasio wachawi katika ulimwengu huu wa macho ya kawaida.

Maandiko yanaposema kuwa, Mungu aliumba vitu vinavyoonekana na visivyoonekana ni kweli kabisa. Wachawi wanaamini kwamba, vitu visivyoonekana pia vilikuwa na siku sita katika uumbaji wa Mungu, siku ya saba akapumzika.

Na hiyo ndiyo sera ya mchawi mara tu baada ya kujiunga katika kazi hiyo inayolaaniwa na wengi ulimwenguni kote.


Kabla sijaenda mbele zaidi nataka kusema kuwa, kama kuna shughuli mbalimbali za binadamu zinazoonekana kwa macho ya kawaida duniani, pia kuna shughuli kama hizo hizo zisizoonekana kwa macho ya kawaida, lakini zinashirikisha wachawi na mambo yao.

Itaendelea Mukinipa 
(Like) Kazi kwenu .......

Powered by Blogger.