Njia 10 za Kuamka Mapema Asubuhi
Kuamka mapema asubuhi kuna manufaa mengi sana. Unapoamka mapema asubuhi unaongeza ufanisi na tija katika utendaji wako wa kazi. Kumbuka pia muda wa asubuhi ndipo mtu anapokuwa na afya njema kiakili na kimwili; hivyo kuamka mapema kutakuwezesha kuutumia muda huu vyema.
Pamoja na umuhimu huu wa kuamka mapema, siyo watu wengi wanaoweza kutimiza lengo lao la kuamka mapema. Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha tatizo hili kama vile matatizo ya kiafya, kisaikolojia na hata kimazingira.
Ikiwa basi wewe ni mmoja wapo wa watu wanaotamani kuamka mapema, basi fahamu njia 10 za kukuwezesha kuamka mapema asububi.
“Ndege wanaoamka mapema ndiyo wanaopata wadudu”
1. Lala muda sahihi
Muda wa kulala ni muhimu sana katika kukuwezesha kuamka mapema asubuhi. Hakikisha unalala mapema na unapata muda wa kutosha wa kulala.
Kwa kawaida binadamu anahitaji saa 7 hadi 8 za kulala. Hivyo hakikisha unapata muda huu hadi muda ule unaotaka kuamka. Kwa mfano, ikiwa unataka kuamka saa 11 asubuhi, unatakiwa kulala saa 3 au 4 usiku. Kwa kufanya hivi mwili wako utapata muda wa kutosha wa kulala na kukuruhusu kuamka mapema asubuhi.
2. Lala katika mazingira sahihi
Siyo mazingira yote yanayofaa kwa binadamu kulala. Mazingira mengine humfanya binadamu kuwa mchovu na kutopata usingizi mzuri. Ili kuhakikisha umepata usingizi mzuri na wa kutosha, hakikisha mazingira unayolala ni rafiki. Unaweza kufanya haya yafuatayo:
- Hakikisha chumba unacholala kina hewa ya kutosha.
- Hakikisha unatumia mto na godoro bora.
- Ondoa kelele na usumbufu mwingine katika eneo unalolala.
- Zima taa au tumia mwanga hafifu wakati wa kulala.
- Tawala joto la chumba unacholala.
Kwa kuzingatia haya utapata usingizi wa uhakika na wakutosha; hivyo utaweza kuamka mapema asubuhi ukiwa na nguvu na afya.
3. Tengeneza ratiba ya kulala inayoeleweka
Kutokana na shughuli nyingi au mtindo fulani wa maisha, watu wengi hawana ratiba inayoeleweka ya kulala.
Utamkuta mtu leo analala saa nne, kesho saa tatu, keshokutwa saa sita, siku nyingine saa mbili n.k. Jambo hili hukufanya kuwa na mfumo duni wa kulala na kutopata usingizi bora; kumbuka usipolala vizuri hutoweza kuamka vyema mapema asubuhi.
Jiwekee ratiba nzuri ya kulala na kuamka leo na uifuate.
4. Epuka vitu vinavyovuruga usingizi
Vipo vitu na tabia mbalimbali zinazoweza kuvuruga usingizi wako na kukufanya kushindwa kuamka kwa wakati asubuhi. Matumizi ya vitu kama vile caffeine, ulaji wa vyakula vizito usiku au matumizi ya vifaa vya kielektroniki huweza kuvuruga usingizi wako kwa kiasi kikubwa.
Hakikisha vitu unavyovitumia au kuvifanya jioni ama usiku, havivurugi ubora wa usingizi wako.
5. Weka malengo
“Jiwekee lengo litakalokufanya uruke kutoka kitandani asubuhi”
Ni lazima ujiwekee lengo la kwanini uamke asubuhi; ni lazima pia ufahamu manufaa ya kuamka asubuhi. Hakikisha unajiwekea lengo na unafanya bidii kulitimiza.
Usikubali usingizi au mwili wako ukuponze kutokutimiza lengo hili. Kujiwekea lengo la kuamka asubuhi ni njia moja wapo ya kukuhamasisha na kukuhimiza kuamka mapema.
6. Weka alamu mbali na kitanda
Watu wengi hupenda kutumia alamu ili kuwaamsha asubuhi; lakini tatizo ni kuwa wanazima (snozee) alamu mara inapoanza kuita.
Ikiwa unataka kutumia alamu kama njia ya kukuamsha basi iweke mbali na kitanda chako; kwa kufanya hivi itakubidi uamke ili uende ukaizime.
Hili litakusaidia sana kwani utakuwa tayari umeshatoka kitandani; hivyo usirudi tena kitandani na endelea na ratiba nyingine ulizojiwekea asubuhi.
7. Usikubali kudanganywa na akili
“Nitaamka tuu baada ya muda kidogo”, “Kwanza kuna baridi”, “Nitawahi sana”, “Sitachelewa”, “Nitafanya haraka”, “Mambo mengi nilifanya jana” n.k. ni baadhi tu ya kauli ambazo watu wengi hudanganywa na akili zao ili walale zaidi.
Usikubali kushawishiwa na mawazo haya; mara muda wa kuamka ufikapo, amka kweli na usiendelee kulala tena. Njia hii itakuwezesha kuamka bila kujishauri na kuruhusu akili kukudanganya.
“Unatakiwa kuwa na ndoto ili uweze kuamka asubuhi”
8. Mwombe mtu akuamshe
Hii ni moja kati ya njia bora sana za kuamka asubuhi kama utapata mtu sahihi. Ikiwa kuna mtu anayeamka mapema kuliko wewe au anayeamka wakati unapotaka kuamka, basi mwombe akuamshe.
Unaweza kumruhusu kukunyang’anya hata shuka ikiwa utakuwa mzito kuamka. Kwa kufanya hivi utaweza kujizoesha kuamka ndani ya wakati uliopanga.
9. Badili ratiba ya kuamka
Njia hii ya kubadili ratiba ya kuamka inaweza kukusaidia kuamka kwa wakati ikiwa utafanya muda wa kuamka uwe mapema zaidi. Kwa mfano ikiwa unataka kuamka saa 11:30 asubuhi, basi jitahidi kuamka saa 11:00 asubuhi.
Kwa kufanya hivi utaufundisha mwili wako kuamka mapema hata kabla ya muda ule uliopanga kufika; hivyo hutahitaji kujilazimisha kuamka wakati wa kuamka utakapofika.
10. Panga ratiba ngumu asubuhi
“Kama unataka kufanya ndoto zako zitimie, jambo la kwanza ni kuamka”
Njiaa hii ya kupanga ratiba ngumu asubuhi itakuwezesha kukuhamasisha na kukuhimiza kuamka mapema na kwa wakati. Hii ni kutokana na sababu kuwa huna muda mwingine wa kutekeleza ratiba husika kwani zinahitajika zitekelezwe asubuhi.
Hakikisha majukumu yako mengi unayapanga kwenye muda wa asubuhi; ikiwa kuna mtu unayetakiwa kukutana naye, pia panga mkutane asubuhi.
Hakikisha unajiwekea ratiba, tena hakikisha ratiba yako inaanza mapema kabisa na unaizingatia.
Hitimisho
Ni wazi kuwa kuna manufaa makubwa sana ya kuamka mapema; Lakini tatizo ni kuwa watu wengi hawawezi kutimiza lengo la kuamka mapema. Ni muhimu kujifunza matumizi mazuri ya muda pamoja na umuhimu wa kujiwekea malengo na kuyatimiza.
Naamini njia hizi zitakusaidia sana ili uweze kuamka mapema. Amka sasa mapema; fanya majukumu yaliyoko mbele yako na kwa hakika utaweza kufikia malengo yako.