HISTORIA YA MUZIKI WA HIP HOP NA BONGO FLEVA NA JINSI UNAVYOONEKANA KUATHIRIWA ZAIDI NA WASHAIRI WA KIMAPOKEO KULIKO WANAUSASA
Hivyo basi
tukiwaangalia mambo yanayosisitizwa na wanajadi na wanausasa, tunakubaliana na
hoja kuwa, muziki wa Hip Hop na Bongo Fleva unaonekana kuathiriwa zaidi na
wanajadi kuliko wanausasa. Na vipengele ambavyo wanajadi wanasisitiza
kuzingatiwa katika ushairi ambavyo vinaonekana kujitokeza katika mashairi ya
Hip Hop na Bongo Fleva kama tulivyoona hapo awali ni, Mizani, vina, kituo na
kujitosheleza. Hebu tuangalie vipengele hivyo namna vinavyojitokeza katika
mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva ambavyo ndivyo vinavyotufanya kushadidia
hoja hii kuwa muziki wa kizazi kipya unaonekana kuathiriwa na wanajadi kuliko
wanausasa tukianza na;
Vina, tunaelezwa na
Amri Abeid (1952:4) kuwa ni silabi za namna moja zinazotokea baada ya kila
mizani kadha katika mstari wa shairi. Kwa upande wake, Wamitila (2003:345)
anasema vina ni, dhana inayotumiwa katika taaluma ya ushairi kuelezea silabi
zinazofanana katika sehemu sawa katika mpangilio wa ubeti wa shairi. Anaendelea
kufafanua kuwa shairi linaweza kugawika katika vipande viwili na kuwa na vina
vya kipande kimoja na kipande kingine. Hiki ndiyo kipengele kinachoonesha kuwa
wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya (Hip Hop na Bongo Fleva) kwa kiasi
kikubwa kuonekana kuathiriwa na ujadi.
Kati ya vitu ambavyo
wanajadi wanasisitiza katika mashairi ni urari wa vina na mizani, kwa mfano
Mnyampala (1962: Dibaji) anasema, Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu
kale. Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozi ya dunia kwa kutumia maneno
ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina
maalumu kwa shairi. Hapa Mnyampala pamoja na kuongelea suala la shairi kutumia
maneno ya mkato na lugha nzito lakini maneno hayo yanatakiwa kupangwa kwa urari
wa vina na mizani. Suala la urari wa vina pia linashadidiwa na Shabaan Robert (
1958) akinukuliwa na Massamba (1983:54) janaposema, Ushairi ni sanaa ya vina
inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi.Zaidi ya kuwa sanaa ya vina
ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari.
Kama tulivyoona kwa
wanajadi, vina ni kigezo kinachozingatiwa sana na wasanii wa Hip Hop/Bongo
Fleva katika tungo zao. Hiki ndicho kigezo ambacho kwa asilimia kubwa ndicho
kinatufanya kushadidia hoja hii kuwa mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva
yanaonekana kuathiriwa sana na wanajadi kuliko wanausasa. Katika muziki huu,
wasanii wasiozingatia matumizi ya vina katika tungo zao zinaonekana hazina
maana kama wanajadi wanavyoona kuwa mashairi yasiyozingatia vina kuwa si
chochote, kama anavyosema Afande Sele katika wimbo wake wa Mtazamo;
Au wengine
mmetumwa kama mamluki,
maana yake hamna
maana mnarap mradi rap,
mistari imekosa
vina yenye vina haina maana.
Aidha katika wimbo
wake mwingine, Darubini Kali Afande Sele, anawashangaa wasanii
wenzake wanaoimba bila vina kama anavyosema,
Mi nacheka sana kuna
vitu vya kuimba vyenye maana kila kona,
(Sasa) inakuwa vipi
unataja taja majina tu nyimbo nzima
Tena kwa mistari isiyo
na vina!
Kwa mtazamo wa Afande
Sele msanii asipozingatia matumizi ya vina anaonekana kama mamluki na mtu asiye
na maana kwenye sanaa. Kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya hususani wa Hip
hop, matumizi ya vina yanasisitizwa zaidi na hata wengine kujinasibisha kuwa
wao ni wataalamu wa kutumia vina kama anavyojinasibisha Solo Thang katika wimbo
wao Tumerudi Tena (Wateule) anaposema, Ona wakali wa
vina, ona tumerudi tena... msanii mwingine Juma Nature katika wimbo
alioshirikishwa na Rich One unaojulikana kwa jina la Hatuna Kitu anajigamba
kuwa yeye ni mkali wa vina anaposema, “...Juma Nature, Sir Nature a.k.a
msitu wa vina, yeah Watanzania mahili tuliokomaa kimashairi...” Hii
yote inaonesha kwa namna gani wasanii wa kizazi kipya (Hip Hop/Bongo Fleva)
wanaonekana kuathiriwa na wanajadi kutokana na kuzingatia matumizi ya vina
katika tungo zao na hata kujinasibisha kuwa ili uwe msanii mzuri lazima ujue
namna ya kuandika na kutunga mashairi yenye vina.
>>>>>INAENDELEA>>>>>>>>>>